Mvutano wa serikali na madaktari haufai

Ouma Oluga

Katibu Mkuu wa Chama cha Madaktari (KMPPDU) Dkt. Ouma Oluga (kulia) na Mwenyekiti Dkt. Oroko Samuel walipohutubia wanahabari awali. Picha/KEVIN ODIT 

Na MHARIRI - TAIFA LEO

Imepakiwa - Wednesday, January 11  2017 at  09:13

Kwa Mukhtasari

Mvutano unaoendelea kati ya serikali na madaktari unachukua mkondo mpya kila uchao huku Wakenya wakiendelea kuhangaika katika maeneo mbalimbali kwa kukosa huduma muhimu za matibabu.

 

MVUTANO unaoendelea kati ya serikali na madaktari unachukua mkondo mpya kila uchao huku Wakenya wakiendelea kuhangaika katika maeneo mbalimbali kwa kukosa huduma muhimu za matibabu.

Leo ni siku ya 39 ya mgomo huo na bado hakuna matumaini yoyote ya Wakenya kuendelea kupata huduma bora za afya.

Inasikitisha kwamba viongozi wa kisiasa wamesalia kimya na badala yake wamekuwa wakizunguka katika maeneo mbalimbali kujitafutia kura kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu ujao, bila kujali iwapo wapiga kura wenyewe watajaliwa kufika Agosti 2017.

Juhudi za Rais Uhuru Kenyatta kuleta upatanisho ziligonga mwamba na inaoenekana ameinua mikon na kwenda zake India kwa ziara ya siku mbili.

Kwa kusalia kimya, ni bayana kwamba viongozi wetu wa kisiasa wanajali masilahi yao wenyewe kwani mishahara yao minono inawaruhusu kwenda kutibiwa katika hospitali za kibinafsi au mataifa ya kigeni.

Mgomo wa madaktari haujashughulikiwa kwa kasi inayostahili haswa ikizingatiwa kwamba madhara yake ni makubwa kwa idadi kubwa ya wananchi.

Kikao cha mwisho kati ya magavana na Wizara ya Afya kiliafikia kuwafuta kazi madaktari wanaoshiriki mgomo huo. Vitisho vya aina hii havifai na vinatatiza juhudi za kutafuta mwafaka.

Sharti pande husika zilegeze misimamo yao ili mwafaka upatikane na huduma za matibabu zirejelewe katika hospitali za umma.

Uamuzi wa serikali kuwaajiri madaktari kutoka mataifa ya nje haitakuwa suluhu kwani mchakato huo unachukua muda zaidi.

Utaratibu

Utaratibu wa kuwaajiri madaktari kutoka nje unahusisha kusajiliwa na Bodi ya Madaktari nchini ambayo imeunga mkono kuboresha kwa mandhari ya kufanyia kazi ya wahudumu wa humu nchini.

Pia, lazima madaktari wa kigeni wafanye kazi kwa muda fulani, chini ya wataalamu wa humu nchini ambao pia wamegoma.

Ukweli mchungu ni kuwa hatua hiyo haitasaidia hali ilivyo na sharti serikali imakinike zaidi.

Madaktari pia wanakiuka kiapo chao cha utendakazi kwa kuwatelekeza wagonjwa katika hospitali za umma na kuanza kufanya vibarua katika hospitali za kibinafsi.