Mwanahabari anayelenga kuangazia masaibu ya walemavu

Eunice Musau

Kwa miaka minne uchunguzi mbovu wa kimatibabu ulimfanya Bi Eunice Musau, 20, kutembea kwa mikongojo. Picha/PAULINE ONGAJI 

Na PAULINE ONGAJI

Imepakiwa - Thursday, February 16  2017 at  12:50

Kwa Mukhtasari

Kwa miaka minne uchunguzi mbovu wa kimatibabu ulimfanya Bi Eunice Musau, 20, kutembea kwa mikongojo. 

 

KWA miaka minne uchunguzi mbovu wa kimatibabu ulimfanya Bi Eunice Musau, 20, kutembea kwa mikongojo. 

Hilo halikuzima ndoto yake ya wakati mmoja kutembea tena kwa miguu miwili huku sasa akiendelea mwanafunzi wa uanahabari katika chuo cha Mahanaim Educational College.

Huu ukiwa mwaka mmoja tangu arejeshe uwezo wake wa kutembea vizuri, Bi Musau ameonyesha ukakamavu na ujasiri badala ya kupoteza matumaini hasa ikizingatiwa masaibu aliyopitia maishani.

Kwanza kabisa Bi Musau hakuzaliwa akiwa kilema kwani kwa miaka saba ya mwanzoni maishani mwake, kama watoto wengine umri wake, maisha yalikuwa ya kawaida.

Mambo yalibadilika mwaka wa 2007 akiwa na umri wa miaka 10 baada ya kuteleza na kuanguka kwenye ukingo wa mto alipokuwa ameenda kuteka maji.

Kwake jeraha hilo lililkuwa la kawaida na mawazoni mwake alidhani kuwa baada ya muda hali ingerejea na kuwa ya kawaida.

Mwanzoni alikumbwa na maumivu ya nyonga kabla ya kuanza kuchechemea na hapa ndipo wazazi wake waligundua na kumpeleka hospitalini ambapo alianza kupewa dawa za kukabiliana na maumivu.

Mwaka wa 2010 akiwa na umri wa miaka 13, baada ya kwenda hospitalini mara kadhaa, madaktari walitambua kuwa alikuwa na uvimbe kwenye goti lake na hivyo wakapendekeza atumie mikongojo.

"Mamangu hakufa moyo; alinisaidia kujifunza kutembea kwa kutumia mikongojo na mwaka mmoja baadaye nikajiunga na shule ya upili walemavu ya Joytown mjini Thika,” aeleza.

Amani

Japo huu ulikuwa mwanzo wa uhalisi wa kuwa kwa kweli hangeweza kutembea, anasema kuwa katika mazingira haya alipata amani tofauti na huko nje alikolazimika kustahimili macho ya watu.

Desemba 2014, baada ya miaka minne ya kutumia magongo wakati huo akiwa katika kidato cha nne, madaktari katika hospitali ya St. Mary’s, mjini Nakuru, waligundua kuwa uchunguzi wa kimatibabu aliokuwa amefanyiwa awali haukutoa matokeo ya kweli.

Japo utelekezaji kwa upande wa wahudumu wa afya wa awali ulimkasirisha, sasa alikuwa na matumaini ya kutembea tena.

Ni matumaini ambayo yalianza kwa kufanyiwa upasuaji na kuanza rasmi safari yake ya kurejea hali yake ya kawaida. Lakini hata kabla ya kupata nafuu, matumaini yake yalipata pigo wiki chache baadaye ambapo mguu wake wa kulia uligunduliwa kuwa mfupi zaidi ya wa kushoto ambapa alilazimika kuvalia kiatu kimoja kilichoinuliwa.

“Moyo wangu ulikufa hasa ikizingatiwa kuwa nilikuwa najiandaa kujiunga na chuo cha mafunzo ya juu,” aeleza.

"Ni changamoto iliyojitokeza hasa wakati wa masomo tekelezi chuoni hasa ikizingatiwa kuwa nasomea uanahabari. Nilikuwa na tatizo la kushika kamera au kusimama kwa muda mrefu, mbali na tatizo la kuunda mahusiano ya kirafiki," aeleza.

Kama wasemavyo kuwa hakuna lisilo na mwisho, matatizo yake yaliisha mwaka wa 2016 baada ya madaktari kugundua kuwa mguu wake ulikuwa umenyoka vya kutosha kiasi cha kumfanya sasa asitumie kiatu kilichoinuliwa.

Sasa ikiwa mwaka mmoja tangu aache kutumia magongo katika matembezi, Bi Musau anapanga kuwa sauti ya wanyonge pindi baada ya kukamilisha masomo yake ya uanahabari ambapo anasema kuwa taaluma aliyopata itakuwa ya kuangazia masaibu ya walemavu.