http://www.swahilihub.com/image/view/-/3880152/medRes/1609258/-/vfhrsk/-/asa.jpg

 

Mwasisi wa Mebongo anayefananishwa na Diamond

Nassizu Murume

Mwanamuziki Nassir Marete al-maarufu Nassizu Murume au ukipenda King Nassizu, Mwasisi wa Mebongo anayefananishwa na Diamond Platnumz. Picha/PAULINE ONGAJI 

Na PAULINE ONGAJI

Imepakiwa - Thursday, April 6  2017 at  21:27

Kwa Mukhtasari

Amefananishwa kwa njia tofauti na mfalme wa Bongo Flava nchini Tanzania, Diamond Platnumz huku mtindo wake wa kuimba ukikaribiana na mdundo huu na hivyo kujiundia kitambulisho cha kipekee nchini.

 

AMEFANANISHWA kwa njia tofauti na mfalme wa Bongo Flava nchini Tanzania, Diamond Platnumz huku mtindo wake wa kuimba ukikaribiana na mdundo huu na hivyo kujiundia kitambulisho cha kipekee nchini.

Huu ukiwa mwaka wake wa pili pekee kama mwanamuziki, Nassir Marete al-maarufu Nassizu Murume au ukipenda King Nassizu tayari anawaonyesha kivumbi magwiji wa muziki nchini.

Kwa nyimbo kama vile Mawazo na kibao chake cha hivi majuzi Siwezi, haina shaka kuwa mfalme wa Watanashati kama anavyojitambua tayari ashaonyesha himaya yake katika tasnia ya muziki nchini.

Japo anaheshimu kazi ya Diamond anasisitiza kuwa nia yake sio kutaka kufananishwa na nyota huyu wa Tanzania.

“Hatuwezi pinga kuwa Diamond ni msanii mzuri na amewakilisha nchi yake vilvyo. Hiyo haimaanishi kuwa nanakili sifa zake au kujifananisha naye,” aeleza huku akiongeza kuwa kufananishwa kwake na msanii wa haiba ya juu kama vile Diamond ni ishara kuwa kazi yake ni ya kiwango cha juu.

Anasisitiza kuwa kama msanii ana mtindo wake wa muziki anaouita Mebongo yaani Meru Bongo.

Mvuto wake kwa mdundo wa Bongo ulianza zamani.

“Nimekuwa shabiki wa mdundo huu tokea kitambo. Bongo ni mtindo unaokubalika na kudumu kwenye nyoyo za watu na wala sio mziki wa kusikika leo na kesho hauna ladha tena,” aeleza.

Tayari mng’ao wake umetambuliwa sio tu na mashabiki bali pia mashirika ambapo mwaka jana aliteuliwa kama mjumbe wa kinywaji cha 8 Vodka.

“Mkataba wangu na Tihan Company Limited ambao ndio wenye kinywaji 8 Vodka ni kwamba sasa mimi ndiye mjumbe wa hii kampuni hii. Kuna vinywaji vingine vinavyoundwa na kampuni hii ila tulitumia 8 Vodka kuwakilisha pia hizo zingine,” asema.

Anasema kuwa ili kutambulika kimuziki sio lazima uwe umetunga na kurekodi nyimbo nyingi, bali kazi na nidhamu yako kama msanii zinapaswa kukubalika katika jamii.

“Sio lazima uwe na nyimbo nyingi ndio ufaulu, upate shoo au mikataba na kampuni kwani wimbo mmoja tu waweza badilisha maisha ya mtu. Pia inategemea na mvuto wako kwani msanii ni kioo cha jamii na hujui nani anaangalia kazi yako,” aeleza.