http://www.swahilihub.com/image/view/-/4904896/medRes/2204370/-/me8gnr/-/meiki.jpg

 

Mwislamu na Radhi za Mola wake

Sheikh Muhammad Issa

Sheikh Muhammad Issa. Picha/MAKTABA 

Na SHEIKH MUHAMMAD ISSA

Imepakiwa - Friday, January 11  2019 at  12:04

Kwa Muhtasari

Katika kuishi maisha yake duniani, Mwislamu hujikuta njiapanda anapojiuliza amridhishe nani, Muumba wake au viumbe wenzake?

 

KWA muumini wa kweli Mwislamu, shabaha yake kubwa katika kila akifanyacho maishani mwake ni kutafuta radhi za Mola wake. Mwenyezi Mungu anasema;

“Na wanalisha chakula juu ya mapenzi yake (Mola wao) masikini na yatima na mateka wa vita. Hakika si vinginevyo, tunakulisheni kwa ajili ya kutafuta radhi za Mwenezi Mungu. Hatutaki kutoka kwenu malipo wala hata shukrani” (Qur’an 76:8-9).

Muumini huyapima matendo yake

Kwa Muislamu mwenye imani ya kweli, kila jambo alifanyalo hulifanya akitafuta kwalo radhi za Mola wake tu wakati wote. Daima hafanyi kutafuta radhi za watu kwa sababu anajua fika ni vigumu kuzipata radhi za watu.

Katika kulinda lengo hili, muumini wa kweli hujikuta anawakwaza watu wengine pale anaposhikilia msimamo wa haki na ukweli kwa kutafuta radhi za Mola wake na akawaudhi wanadamu.

Muumini hufanya hivyo akifuata uongofu wa Mtume Muhammad (rehma na amani ziwe juu yake) pale aliposema;

“Yeyote mwenye kuzitafuta radhi za Mwenyezi Mungu kwa kuwaudhi watu yeye atamtosheleza vitimbi vya watu. Na mwenye kutafuta radhi za watu kwa kumuudhi Mwenyezi Mungu basi atawafanya watu wamkasirikie” (Imepokewa na Tirmidhy).

Kipimo cha matendo ya muumini ni radhi za Mwenyezi Mungu. Muumini hupima matendo yake kwa kuangalia je nikifanya kitendo hiki nitapata radhi za Mwenyezi Mungu au nitamkasirisha?

Na ili kitendo kiwe na radhi za Mwenyezi Mungu, inabidi kiwe na sifa mbili- Mutaaba’a na Ikhlaasi.

Mutaaba’a ni pale muumini anapokifanya kitendo vile alivyofundishwa katika Qur’an na Sunnah yaani kwa kufuata hivyo viwili pasina kuongeza kitu wal akupunguza kitu au kutia maana aijuaye yeye (Ta’wiili).

Ikhlaasi ni pale anapokifanya kwa nia safi ya kumuabudu Mweneyezi Mungu pasina kumshirikisha na chochote yaani anapojiepusha na Shirki kubwa na Shirki ndogo katika vitendo vyake.

Shirki kubwa ni kuamini kwamba kuna Mola mwingine pamoja na Mwenyezi Mungu naye anazo sifa kama za Muumba na anastahiki kuabudiwa.

Shirki ndogo ni pale Muislamu anapofanya ibada au kitendo kisha akakusudia watu wamuone au wamsikie au wamsifie na kadhalika. Muumini wa kweli atajiepusha na yote hayo kwa kujua kuwa yatamfanya akose radhi za Mwenyezi Mungu.

Anasema Mola Muumba “Na hakika ulipewa wahyi wewe na wale waliokutangulia ikiwa utamshirikisha Mwenyezi Mungu hubatilisha matendo yako na utakuwa miongoni mwa waliopata hasara” (Qur’an 39:65).

Kwa hiyo muumini wa kweli Muislamu hafanyi mambo kwa Ria au kujioyesha kwa watu wala kwa Sum’a au kutaka asikiwe na hivyo asifiwe na watu bali hufanya ili apate radhi za Mola wake tu.

Na kwa mwenendo huu, mizani ya kupimia mambo ya muumini Muislamu ni tofauti kabisa na mizani za wanadamu wengine.

Wakati wengine wakiyapima mambo kwa jisni yatakavyowapa faida au kuwajengea hadhi mbele za walimwengu, yeye huyapima mambo kwa mizani ya radhi za Mwenyezi Mungu dhidi ya radhi za viumbe.

Katika zama hizi, Waislamu tulio wengu tumepoteza mizani hii. Na sisi tumezama katika kupima mambo kwa vipimo vya kidunia zaidi pasina kujali kutafuta radhi za Mwenyezi Mungu.

Ni wangapi kati yetu tunaweza kumtii Mwenyezi Mungu katika jambo moja na kumuasi katika jingine, au kuharamisha jambo katika hali fulani lakini tukalifanya katika hali nyingine?

Kwa mfano, utakuta Muislamu anaswali swala tano kila siku tena bila kukosa jamaa msikitini, lakini utamkuta huyo huyo akisema uwongo, akisengenya, akidhulumu watu, hata akizini tena na wake za watu.

Anayafanya haya pasina khofu moyoni kwa sababu amesahau mizani yake ya kuyapimia mambo kabla hajayafanya ni je nikilifanya hili litapata radhi za Mwenyezi Mungu au nitamuudhi?

Wengi wetu tunaishi maisha ya undumilakuwili au “slip personality” ambao ni ugonjwa wa akili unaowasibu wanadamu wengi, lakini unapohamia katika masuala ya imani, hapo madhara yake huwa mabaya mno kwa mustakbali wa muumini mbele ya Mola wake. Undumilakuwili kiimani, humfanya mtu akiwa mbele ya Mola wake utadhani ni swahaba Abubakar Swidiiq lakini akiwa mbele za watu katika harakati zake za maisha utadhani ni Abu Jahli.

Nyuso mbili

Mtu kama huyu anaitwa Dhul Wajhayni yaani mtu mwenye nyuso mbili. Mtume Muhammad (rehma na amani ziwe juu yake) aliwaonya Waislamu juu ya madhara ya undumilakuwili huu pale aliposema;

“Utakuta miongoni mwa watu waovu zaidi siku ya kiama mbele ya Mwenyezi Mungu ni Dhul Wajhayni ambaye anawaendea watu fulani kwa uso fulani na watu wengine kwa uso mwingine” (Bukhari na Muslim).

Tunapowaona Waislamu msikitini wakiswali wanyenyekevu kisha tukikutana nao sokoni, ofisini, shambani, shuleni au chuoni, mtaani au majumbani kwao wakiishi kinyume na mafundisho ya Uislamu;

Basi tujue kuwa tatizo ni kutokujua kuwa maisha yote ya Muislamu anapaswa kuishi akitafuta radhi za Mwenyezi Mungu, na muumini wa kweli hawezi kufanya hivyo kwa sababu hajui sekunde, dakika, saa, siku na wakati wa kufa kwake.

Nasaha zangu kwanza kwangu mwenyewe na kwa ndugu zangu Waislamu, hebu tumrudie Mwenyezi Mungu. Tuishi maisha ya kuzitafuta radhi zake hata kama itasababisha kuwaudhi wanadamu wenzetu.