http://www.swahilihub.com/image/view/-/4840268/medRes/2162968/-/dh6m59z/-/pichatu.jpg

 

Mwonekano wetu utakaokuvutia zaidi

Mwananchi

Gazeti la Mwananchi; toleo la Novemba 7, 2018. Picha/JENITHA KIMAMBO 

Na MHARIRI - MWANANCHI

Imepakiwa - Wednesday, November 7  2018 at  06:32

Kwa Muhtasari

  • Kwa huu mwonekano mpya wa gazeti la Mwananchi tunaamini kwamba wasomaji wetu watatupokea vizuri, huku tukitarajia kupokea maoni yao na kuyafanyia kazi
  • Mabadiliko ya kimsingi hasa ni maudhui na makala ambazo zimeongezeka

 

BILA shaka utakuwa umeyaona mabadiliko kadhaa katika toleo la leo la gazeti la Mwananchi.
Hili halikufanywa kwa bahati mbaya, bali limelenga kukidhi matakwa na mahitaji ya wasomaji wetu.
Baada ya kupokea maoni na ushauri mbalimbali kutoka kwa wasomaji juu ya nini wanachokihitaji katika gazeti hili, uongozi wa Kampuni ya Mwananchi Communications (MCL), umefanya mabadiliko kadhaa katika kurasa zake hususan za majarida yake ya Spoti Mikiki, Maarifa ambalo sasa linaitwa Elimu, Siasa, Uchumi, Afya, Starehe na Johari.
Katika mabadiliko hayo, tumeongeza idadi ya habari ili kumpa msomaji wigo mpana zaidi wa kupata taarifa kutoka katika kila pembe ya nchi na nje ya mipaka yetu.
Habari hizo sasa hazitapatikana katika kurasa zetu za kawaida pekee, bali hata katika majarida yetu. Kuanzia sasa kila jarida mbali ya kuwa na makala, maoni na uchambuzi, litabeba habari zilizofanyiwa utafiti wa kina katika eneo mahsusi.
Mathalan, leo tumefanya mabadiliko haya siku ya Jumatano ambayo tunachapisha Jarida la Siasa hivyo, makala nyingi zaidi, maoni na uchambuzi vinahusu masuala ya kisiasa.
Kadhalika, kesho Alhamisi itakuwa ni Uchumi, Ijumaa itakuwa siku ya Afya ikifuatiwa na Starehe na Johari, Spoti Mikiki na Elimu mtawalia.
Hata hivyo, mbali ya kuwa na majarida haya yatakayokuwa yakijikita katika maeneo mahsusi, tumeimarisha pia jarida letu la Ndani ya Habari ambalo msingi wake ni kufanya uchambuzi wa kina wa habari pamoja na makala za kijamii na uchambuzi.
Aidha, kwa kuzingatia kwamba asilimia kubwa ya Watanzania ni wakulima, tumeelekeza nguvu kubwa hasa katika siku za Jumamosi ambako tumeimarisha Jarida la Mbegu ya Dhahabu ambalo linazungumzia masuala muhimu ya kilimo na ufugaji tukiamini kwamba ushauri unaokusanywa kutoka kwa wataalamu wa kilimo na mifugo, utawezesha wananchi wakulima kupata tija kwenye shughuli zao.
Ili kufanikisha hayo, pamoja na kupokea maoni ya wasomaji juu ya nini wanachokipenda, wasichokipenda, wanachotaka kubadilishwe na wanachotaka kisiguswe katika gazeti lao, uongozi wa MCL uliitisha kongamano kubwa la wanahabari wake pamoja na wafanyakazi wake wengine kujadili suala moja kubwa; uandishi makini wa kiweledi, unaozingatia weledi ili kukidhi mahitaji ya dunia ya sasa.
Tuliwaalika wataalamu watatu; Jenerali Ulimwengu, mwandishi wa habari mkongwe ambaye pia ni mwanasheria, Fausta Musokwa kutoka Mfuko wa Habari Tanzania (TMF) na Harold Sungusia ambaye ni mwanasheria, chini usimamizi wa Mhariri wa Jamii wa MCL, Ndimara Tegambwagwe.
Wasomi hawa walitoa mada zilizolenga kuwajengea uwezo waandishi wetu juu ya kuandika habari zinazoendana na hali halisi ya mwelekeo wa dunia ya sasa ambayo inapita katika mabadiliko kwenye kila nyanja.
Kwa hiyo, tunaamini kuwa hata uandishi wetu utakuwa makini zaidi na wenye lengo la kubadilisha maisha ya wasomaji wetu na jamii kwa ujumla kama malengo yetu yanavyoonyesha.
Imani yetu ni kuendelea kuwapatia wasomaji wetu habari za kina bila woga lakini kikubwa zaidi bila ya kumuonea yeyote.
Tunaamini pia kwamba wasomaji wetu watatupokea vizuri, huku tukitarajia kupokea maoni yao na kuyafanyia kazi.

Tahariri ya Mwananchi,

Mwananchi Communications Limited (MCL)

S.L.P. 19754 Dar es Salaam-Tanzania

SIMU +255222450875 au +255754780647