http://www.swahilihub.com/image/view/-/4924490/medRes/2217456/-/mf5dbrz/-/msefundi.jpg

 

Mzee ajutia uamuzi wake wakati wa shamrashamra 2018

John Fundi

John Fundi. Picha/MWANGI MUIRURI 

Na MWANGI MUIRURI

Imepakiwa - Monday, January 7  2019 at  12:47

Kwa Muhtasari

Baadhi ya watu wana mazoea ya kufuja pesa kukidhi haja zao wakati wa shamrashamra za Desemba.

 

JOHN Fundi anasema hatasahau sikukuu za Krismasi Desemba 2018 na sherehe za Mwaka Mpya 2019 kwa kuwa ndizo katika maisha yake yote ya hadi sasa katika safu ya riziki alijitekelezea kwa hiari ujinga mkuu wa kufuja pesa zake.

Mfanyabiashara na mkazi wa Mji wa Maragua ambapo huchuuza mikoba ya kubebea vitabu vya wanafunzi, anasema kuwa aliamua kujipa likizo ya kibiashara tarehe 23 Desemba ili aanze kujiandaa kusherehekea sikukuu.

“Nilikuwa na Sh53,000 ambazo Sh20,000 zilikuwa za kununua mikoba ya kurejelea biashara yangu Januari 2, 2019. Sasa sikiliza nikueleze ni kwa nini sitaki mtu anikumbushe kuhusu sikukuu za Desemba 2018,” anasema Bw Fundi.

Anasema kuwa alikuwa na busara ya kimatumizi pesa zake Desemba 23 kwa kuwa alimwandama mpangishaji nyumba anayokaa na akamlipa Sh4, 000.

“Mimi naishi kwa nyumba ya Sh2,000 kwa mwezi. Nikijua kuwa Januari ya kila mwaka huwa na changamoto za kifedha, niliamua kulipa hata mwezi wa Januari ndio nijipe afueni ya mapema,” anasema.

Kutokana na hali hiyo, alibakia na Sh49,000 na ambapo aliefululiza hadi katika duka la huduma ya Mpesa na akatumia bibi yake Sh10, 000 za kugharamia mavazi mapya kwa watoto wake watatu.

“Mimi nikiwa katika mji huu wa Maragua, mke wangu huishi katika Kaunti ya Meru katika boma la babangu mzazi na ambapo hushiriki kilimobiashara. Nilipotuma hizo pesa, nilimpigia simu na nikamuahidi kuwa Desemba 25 asubuhi ningekuwa nimefika katika boma hilo tushiriki sherehe ya Krisimasi pamoja na hatimaye nitulie huko hadi Januari 1, 2019,” anasema.

Anasema kuwa bibi yake alifurahia kujitolea kwake na akamwahidi kuwa pamoja na watoto walikuwa na furaha tele na walikuwa wanamngoja kwa hamu kuu.

“Nilitabasamu yangu yote huku nikiwa na kiburi cha ajabu kuelewa kuwa nilikuwa nimewajibikia majukumu yangu kama mzee wa boma. Nikiwa na miaka 41 kwa sasa, nilijihisi kama mzee mstaarabu wa miaka 60, na hata nikaanza kuota ndoto ya jinsi ningenunua gari jipya na niwasili nalo nyumbani ndio watambue bidii yangu,” anasema.

Lakini akifahamu kuwa mfukoni mwake alikuwa na Sh39,000 pekee na ambazo Sh20,000 zilikuwa mtaji 3wa kurejelea biashara yake Januari, kumaanisha alikuwa na Sh19, 000 pekee za matumizi na ambazo hata hazingetosha kununua pikipiki.

"Lakini nilijipa moyo kuwa  bado maisha yangu ni marefu mbele yangu na hatimaye nikitia bidii ya kimaisha, ningeishia kutimiza ndoto yangu ya kujinunulia gari. Ndipo niligundua kuwa katika miaka mitano ambayo nimekuwa katika biashara hii, sikuwa nikijiwekea akiba, bali nilikuwa natuma pesa tu nyumbani na kutumia zingine katika maisha yangu ya raha,” anasema.

Hapo ndipo aliapa kimoyomoyo kuwa kuanzia Januari 2019, atakuwa akijiwekea akiba katika benki ili kuafikia ndoto hizo ambazo zilikuwa zimeanza kumnyemelea maishani.

“Sasa, udhaifu wangu mkuu ni kuwa mimi ni mtumizi wa pombe na sigara. Na sio kwa ku8penda kwangu,  bali nilijipata nimetekwa nyara na ulevi na uvutaji wa sigara. Lakini nimekuwa nikifanya bidii kupunguza gharama za uraibu huu wangu,” anasema.

Alikuwa amefikiria kuweka zile pesa za kurejelea biashara yake Januari katika akaunti yake ya M-Pesa kuzihifadhi lakini anasema kuwa haelewi vile aliishia kutkotimiza wazo hilo.

“Pesa saa zingine huwa na ushetani wa kipekee ambapo ukiwa nazo, huwa unaingiwa nay ale majivuno ya kutaka kuianika kwa wote waone kuwa wewe umejiweza. Hakuna raha kuu inayobishana na ile ya ukiwa na mkoba uliojaa manoti na unapolipa bili zako, unaanika kwa wote walio karibu ili wakutambue kuwa wewe sio mzembe na huwezi ukajumuika ndani ya umasikini,” anasema.

Hivyo ndivyo Bw Fundi anasema kuwa alifululiza hadi baa moja ya mji wa Mragua usiku huo wa Desemba 23 na akaagiza kileo chake.

“Sijui ni raha  gani iliyonikumba kwa kuwa nilijipata nikinunulia hata wateja wengine pombe. Mazingara ya baa hiyo yalikuwa ya raha tupu kwa kuwa hata  ngoma ambazo zilikuwa zinachezwa zilikuwa zikitupagaisha na warembo sijui walikuwa wameagizswa kutoka wapi…. Wacha raha itambe…” anasema.

Kile anachojua ni kuwa asubuhi ya Desemba 24 alikuwa ametumia Sh5,000, hivyo basi kupunguza pesa zake za ujumla hadi Sh34,000.

Alifanya hesabu yake ya haraka na akajua kuwa mtaji wake wa Sh20,000 ulikuweko bado lakini za kusafiri hadi nyumbani kwake Meru zilikuwa zimepungua hadi Sh14,000.

“Niliamua kuwa ningesafiri hiyo asubuhi hadi Meru na kwa uhakika, niliabiri gari hadi Mjini Murang’a nikiwa na wazo la kuabiri lingine la kunifikisha Sagana na ndipo niabiri sasa la kunipeleka hadi Makutano na hatimaye la kunifikisha kwetu Meru. Cha kuharibika lazima kiharibike kwa kuwa ile njia ya haraka ilikuwa niabiri gari hadi Mji wa Kenol na hatimaye niabiri la kunipeleka moja kwa moja hadi Meru,” anasema.

Kulewa

Bw Fundi anasema kuwa alipotua Mji wa Murang’a, aliingia na tamaa ya kunywa chupa mbili na ambapo aliingia kwa baa moja.

“Hizo chupa mbili sijui ilikuwa namna gani kwa kuwa  nilijipata nikiwa ndani ya baa hiyo asubuhi ya Desemba 25, nikiwa mlevi na bila hata hamu ya kufika kwetu nyumbani. Desemba 26 iliniapata katika mji huo pia na sikuwa hata nikijibu simu za bibi yangu akiwa nyumbani,” anasema.

Desemba 27 ndio alifika Meru akiwa na Sh8,000 mfukoni, pesa ambazo zilikuwa hata hazitoshi mtaji wa kurejelea biashara yake.

“Mambo yakiharibika, huwa hayakupi ilani... Nilimpa mke wangu Sh5,000 huku nikimpa hadithi za uongo za rejearejea za jinsi nilikamatwa na polisi katika mji wa Sagana na nikaachiliwa asubuhi hiyo ndio nifike nyumbani saa 12 jioni,” anasema.

Akiwa na Sh3,000 kwa mfuko, aliamua kuwa ni lazima angesaka afueni ya haraka kwa kuwa alikuwa anategemewa atoe Sh8,000 za karo Januari 3, 2019.

“Asubuhi ya Januari 31, niliabiri gari hata bila ya kuaga familia yangu na nikarejea hadi Mji wa Maragua. Nilimwendea bwanyenye mwingine ambaye ni rafiki yangu wa Mji huu na nikamdanganya kuwa nilikuwa na shida ya kinyumbani ambayo ilikuwa inahitaji ufadhili wa Sh30,000,” anasema.

Anasema kuwa bwanyenye huyo alikubali kumpa mkopo wa Sh30,000 na ambapo alijihakikishia kurejelea kazi yake ya biashara, akapata uhai tena wa kulipa karo ya watoto wake lakini kwa sasa ako na mkopo wa kulipa.

“Mtu ambaye alikuwa na Sh53,000 zilizokuwa zimetosha kugharamia hayo yote, kupitia maamuzi butu ya kimaisha, nikajipata nimeufunja kwa siku tatu tu na kuzidisha masaibu kwa kujitwika mkopo ambao sina budi kuulipa kabla ya Machi, 2019,” anasema.

Anasema kuwa hatakoma kunywa pombe, lakini atahakikisha amejipa uthibiti na adabu za kimsingi katika uraibu huo kiasi kwamba hatawahi tena kujipata ndani ya maamuzi ya kujisambaratisha kwa kasi na kwa kiwango hicho cha Desemba 2018.