http://www.swahilihub.com/image/view/-/4837110/medRes/1907423/-/ju6g7/-/yanga.jpg

 

Nanyi Yanga chagueni watu wa kuiongoza klabu

Yanga

Shabiki wa klabu ya Yanga. Picha/MAKTABA 

Na MHARIRI - MWANANCHI

Imepakiwa - Monday, November 5  2018 at  07:03

Kwa Muhtasari

Mojawapo ya maelekezo ya Serikali kupitia Baraza la Michezo la Taifa (BMT) ni kwamba klabu ya Yanga inatakiwa kujaza nafasi zilizoachwa wazi.

 

KLABU mbili kongwe nchini Tanzania ziko katika mchakato wa uchaguzi ambapo kwa upande wa klabu ya Simba, Jumapili walifanya uchaguzi wa viongozi wao watakaokuwapo kwa miaka minne.

Kufanyika kwa uchaguzi, malengo ni kupata viongozi ambao watawawakilisha wanachama katika safu mpya ya uongozi itakayoungana na safu kutoka upande wa mwekezaji.

Hali ni tofauti kwa upande wa Yanga ambapo uchaguzi wao ni ule wa mfumo wa uongozi wa zamani wa vilabu hivi, kupata wanachama ambao wataongoza klabu kwa kipindi kijacho ambao matarajio ni kwamba wataipeleka klabu kwenye mfumo wa uongozi wa hisa kama ilivyo kwa watani wao wa Simba.

Maelekezo ya Serikali kupitia Baraza la Michezo la Taifa (BMT), yapo katika nyanja kuu zifuatazo:

Klabu ya Yanga inatakiwa kujaza nafasi zilizoachwa wazi

Kulingana na maelezo ya BMT, wapo wajumbe sita waliobaki kati wajumbe 13 wa Kamati ya Utendaji, hivyo kuhitajika wanachama wapya saba akiwamo Mwenyekiti wa klabu. Katika hili, ushauri wangu ni kwamba ni vyema wanachama wa klabu wakawa makini katika kuwachagua wajumbe hao wapya kwa sababu kulingana na taarifa za mkutano mkuu wa wanachama uliopita, uamuzi ni klabu ya Yanga kwenda kwenye mfumo tofauti wa uendeshaji wa klabu, ule wa kuwa na hisa baina ya mwakezaji na wanachama.

Kwa sababu hiyo, viongozi watakaochaguliwa sasa lazima wawe ni wale ambao watarahisisha na kufanya kwa umakini mchakato wa kubadili mfumo wa uendeshaji wa klabu. Kama wanachama hawatakuwa makini na kutochagua viongozi sahihi, wanaweza wakajikuta wanaanzisha mgogoro mpya kwa sababu matarajio ya wanachama na wapenzi wa timu hiyo hayatafikiwa na hivyo timu kuendelea kuendeshwa kwa ukata mkubwa, jambo ambalo litasababisha vurugu kwenye klabu kwa sababu hali hiyo itakuwa kinyume na matarajio ya wanachama ambao wanataka klabu yao iende kwenye mfumo wa uendeshaji wa timu wa hisa.

 

Utata kuhusu suala la kadi za wanachama

Moja ya eneo ambalo huleta mpasuko wakati wa chaguzi za klabu hizi kongwe huwa ni kuwatambua wanachama gani wanaostahili kupiga kura.

Uzoefu unaonyesha kwamba mwafaka usipofikiwa, vurugu kubwa hutokea. Jambo kama hilo huwa halitarajiwi kwa sababu aina zote za kadi hizo huwa zimetolewa na viongozi walioko madarakani kihalali.

Ni vyema basi ushauri uliotolewa na BMT ukazingatiwa ambao ni kwamba wanachama wenye utambulisho wowote halali wa wanachama waruhusiwe kushiriki kwenye uchaguzi ili kuleta umoja kwenye klabu.

Ninaamini kwamba wanachama nao watafuata maelekezo ya BMT ambayo yameelekeza kwamba wanachama wote wenye utambulisho wowote wa wanachama, waende kujiandikisha kwenye rejista ya matawi yao, kwani kutofanya hivyo, ‘mwanachama’ hataruhusiwa kupiga kura ya kuchagua viongozi wake.

Ushauri wote uliotolewa na Serikali umezingatia katiba na mazingira ya hali halisi ya wanachama yaliyopo sasa ili kuleta umoja. Ni vyema wanachama wawashawishi wanachama ambao wanaamini kwamba wataivusha klabu salama katika kuleta mfumo mpya wa uongozi (hisa) na viongozi hao watakuwa na uwezo wa kumshawishi mwekezaji makini.

Hakuna mwekezaji ambaye atawekeza fedha zake atakapoona kwamba viongozi waliochaguliwa hawaamini kutokana na sifa zao katika uongozi wa mpira au katika shughuli za kijamii.

Kwa kulitambua hilo, wanachama wa Yanga wanayodhamana kubwa kuhakikisha kwamba pamoja na utambulisho wa wanachama kuhuishwa, wakichagua viongozi wasio weledi na waadilifu, wanaweza wakajikuta kwamba hawapati mwekezaji waliyemtarajia.

Tahariri ya Mwananchi,

Mwananchi Communications Limited (MCL)

S.L.P. 19754 Dar es Salaam-Tanzania

SIMU +255222450875 au +255754780647