http://www.swahilihub.com/image/view/-/4885584/medRes/2191515/-/9pi6qkz/-/ngege.jpg

 

MAPISHI: Ngege wa kukaanga kwa vitunguu na nyanya

Ngege

Ngege wa kukaanga kwa vitunguu na nyanya. Picha/SAMMY WAWERU 

Na SAMMY WAWERU

Imepakiwa - Friday, December 7  2018 at  13:19

Kwa Muhtasari

Ngege ni samaki wa maji yasiyo ya chumvi.

 

NGEGE ni aina ya samaki ambaye wakazi wengi Afrika Mashariki hupenda akiwa amepikwa.

Eneo la Nyanza linafahamika katika uvuvi wa samaki hawa kwa sababu ya kuwepo kwa Ziwa Victoria.

Hata hivyo, wanafugwa katika maeneo mengine nchini Kenya hasa katika vidimbwi na wanahitaji maji safi ila si ya chumvi.

Upishi wa tilapia mmoja, muda wa maandalizi yake ni karibu dakika 40.

Vinavyohitajika

-Samaki aina ya tilapia

-Nyanya nne na vitunguu viwili

-Kifungu kimoja cha dania (kwa hiari)

-Mafuta

-Chumvi

Matayarisho

Mwoshe samaki vizuri ikiwamo kuondoa shombo. Weka mafuta kwenye kikaango kisha umchome hadi akauke.

Shughuli hii ni ya karibu dakika 20, dalili zake kukauka zikiwa kubadili rangi kuwa hudhurungi. Muepue ili kuandaa viungo vya kumkaanga.

Jinsi ya kumuunga

Katakata vitunguu na kuvitia kwenye kikaango tofauti au ulichotumia kumchoma baada ya kuondoa mafuta yaliyosalia.

Vipande vya vitunguu vikiiva, ongeza nyanya na dania. Miminia mafuta kiasi na kugeuzageuza mchanganyiko wa viungo hivi na uupe muda wa dakika 10 uive kikamilifu.

Mchuzi ukiwa mzito, weka tilapia halafu uache atokote kwa dakika 10 hivi na usisahahu kutia chumvi kwa kipimo.

Epua samaki wako, andaa kachumbari ili kuongeza ladha. Ngege huyu tayari kuliwa kwa ugali.