http://www.swahilihub.com/image/view/-/2758636/medRes/1040993/-/hpl66o/-/nyonyesha.jpg

 

Nguvu ya wengi inahitajika utelekezaji wa watoto

Mwanamke amnyonyesha mtoto

Mwanamke amnyonyesha mtoto. Picha/MAKTABA 

Na MHARIRI – MWANANCHI

Imepakiwa - Friday, April 13  2018 at  10:03

Kwa Muhtasari

Mwananchi hatutetei vitendo vibaya vya utelekezaji wa watoto, wanawake au wanaume.

 

KWA siku nne mfululizo wakazi wa Dar es Salaam hasa wanawake wamekuwa wakijitokeza kwa wingi katika Ofisi za Mkuu wa Mkoa kwa ajili ya kuwasilisha madai ya kutelekezwa na wenza wao.

Wanawake hao wamekuwa wakilalamika hapo kuitikia wito wa Mkuu wa Mkoa Paul Makonda ambaye alitangaza kwamba ana dhamira ya kuwasaidia wanawake ambao ni wakazi wa mkoa wake.

Awali wito huo uliitikiwa kwa nguvu kubwa na wanawake waliojitokeza kwa mamia katika viwanja vya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wakidai kutelekeza ya Mkuu wa Mkoa lakini kadiri siku zinavyokwenda baadhi ya wanaume nao wamejitokeza kudai kutelekezwa.

Ukiondoa wanaume kujitokeza kudai wanatelekezwa kuna mambo mengine yasiyo ya kawaida yamekuwa yakijitokeza ikiwamo ya wanawake wenye umri mkubwa kujitokeza wakidai kutelekezwa na baba zao.

Kinachoendelea katika ofisi hizo limewashtua watu wengi hasa kwa kuwa desturi za Watanazia ni kuwa masuala mengi ya kindoa na uhusiano ama hushugulikiwa faragha au hutafutiwa ufumbuzi kupitia vyombo vya sheria kama Mahakama, Ofisi za Ustawi wa Jamii na viongozi wa dini.

Kama wadau muhimu kwa jamii, Alhamisi tukalazimika kuweka bayana masuala 10 yanayoakisi mitazamo ya watu wengi kuhusu uendeshaji wa michakato wa kusikiliza kero za wazazi hao.

Kwa muhtasari baadhi ya maswali yetu yalihusu uhalali wa kisheria wa kinachoendelea, haki za binadamu, uwezekano wa kuwepo kwa migongano wa kitaasisi, usawa wa kusikiliza , kuwepo kwa ajenda nyuma ya kampeni hiyo na namnabgani mila na desturi za Kitanzania zimezingatiwa katika masuala ya malezi.

Mwananchi hatutetei vitendo vibaya vya utelekezaji wa watoto, wanawake au wanaume. Ni vitendo vinavyotakiwa kupigwa vita na kila mmoja wetu. Tatizo tunaloliona ni namna mamlaka husika inavyoendesha mchakato huo, huku ikijiweka kando na mitazamo ya wengi kama inavyoonekana kupitia masuala haya.

Hatupaswi kulichukulia jambo la mtu mmoja au chombo kimoja cha Serikali. Ni suala mtambuka hivyo vyombo husika vilitakiwa kushiriki kikamilifu kutafuta dawa ya tatizo. Vyombo hivi ni vile vya kiserikali, asasi za kiraia, mashirika ya dini na kadhalika. vilipaswa kushiriki ili kutafuta dawa ya tatizo hili.

Kwetu sisi ushiriki wa taasisi nyingi sio tu ungeufanya mchkato uwe na tija lakini pia unaweza kusaidia kuepusha athari zinazoweza kujitokeza ikiwamo  kuongezeka kwa mitafaruku kati ya wanandoa, kukomoana, utapeli,kuumizana, kuumizana kisaikolojia  na athari nyinginezo.

Tahariri ya Mwananchi,

Mwananchi Communications Limited (MCL)

S.L.P. 19754 Dar es Salaam-Tanzania

SIMU +255222450875 au +255754780647