http://www.swahilihub.com/image/view/-/3082466/medRes/1259689/-/na64pvz/-/DNCOASTARREST1312G.jpg

 

Nguvu zaidi zinahitajika hili suala la mauaji ya watoto

Visu

Visu. Picha/MAKTABA 

Na MHARIRI - MWANANCHI

Imepakiwa - Tuesday, January 29  2019 at  10:30

Kwa Muhtasari

Ni jambo la kusikitisha na kuhuzunisha kwamba watoto 10 wamechinjwa katika mji wa Njombe kisha waliotekeleza mauaji hayo kuondoka na baadhi ya viungo vya miili ya marehemu.

 

NI jambo la kusikitisha na kuhuzunisha kwamba watoto 10 wamechinjwa kisha waliotekeleza mauaji hayo kuondoka na baadhi ya viungo vya miili ya marehemu.

Hakuna namna nyingine ya kulielezea jambo hilo zaidi ya kusema ni ukatili na unyama uliopitiliza.

Hilo limetokea katika Halmashauri ya Mji wa Njombe ambako watoto sita wamefanyiwa ukatili huo huku katika Halmashauri ya Wilaya ya Njombe watoto wanne wakikumbwa na mkasa huo.

Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Christopher Ole Sendeka anasema mauaji hayo yanahusishwa na imani za kishirikina na visasi. Ni jambo la kushangaza na kustaajabisha watu kufanya ukatili wa aina hiyo kwa watoto wanaoelezwa kuwa na umri wa kati ya miaka miwili hadi sita. Hata kama ni kulipiza kisasi iweje roho zao ziwe jambo la ahueni kwa aliyekosewa ama na mzazi au ndugu wa mtoto husika.

Hali hiyo haipaswi kuvumiliwa wala kupewa muda wa kusubiri. Ingawa Serikali kupitia kwa Mkuu wa Wilaya ya Njombe, Ruth Msafiri imesema juhudi mbalimbali zinaendelea kuchukuliwa na mamlaka husika kukabiliana na matukio hayo, bado kuna maswali ambayo majibu yake yanaweza kuwa msaada ama kwa matukio hayo au mengine yanayopangwa kutekelezwa na watu wenye mtazamo kama huo.

Kwa nini kunatokea tukio la kwanza hadi la tatu la ukatili kama huo na kuripotiwa katika vyombo vya ulinzi, lakini kunakuwa na kujivuta miguu kuchukua hatua za kudhibiti na kunusuru maisha ya watoto wasiokuwa na hatia?

Hivi ni kweli tumefikia mahali ndani ya Tanzania hii wazazi wawawekee ulinzi binafsi watoto wao kwa kuwapeleka na kuwafuata shuleni baada ya masomo?

Bila shaka vyombo vya ulinzi na usalama vinao uwezo wa kuchunguza, kung’amua na kuwabaini wahusika wa matukio hayo na kama ni mtandao ukawekwa wazi na hatua kuchukuliwa.

Ni muhimu kwa vyombo hivyo kuongeza kasi ya kushughulikia matukio yasiyo ya kawaida mara yanapotokea katika jamii ili kuepusha madhara makubwa kama ilivyo Njombe ambako wazazi wanakabiliwa na changamoto kubwa ya ulinzi wa watoto wao.

Aidha, jamii nayo inapaswa kuwajibika katika kuwalinda watoto kwani hakuna namna yoyote ambayo watekelezaji wa matukio hayo wanaweza kufanikiwa bila ya kushirikiana na baadhi ya watu ndani ya jamii.

Kama sababu ikiwa ni imani za kishirikina, wapo wanaowaaminisha wengine kuwa watafanikiwa kwa njia za mkato na zisizo halisia. Watu hao hasa kama ni waganga wa jadi wanapaswa kuacha utapeli na kutambua wajibu wao wa kuimarisha upendo, ushirikiano na kuhimiza uwajibikaji ili kila mmoja afanikiwe kwa kutumia jasho lake.

Viongozi wa dini nao waongeze mahubiri na ili kuimarisha imani kwa waumini wao kwani kufanya hivyo  kunaweza kuwapa mwanga wa kubaini matukio yasiyo ya kibinadamu ambayo si njia sahihi ya kufanikiwa kimaisha.

Ingawa mkuu wa wilaya, amesema wameanza kukaa na makundi mbalimbali kwa ajili ya kukumbushana jukumu la kila mmoja katika kushiriki kuzuia matukio zaidi ya aina hiyo, lakini jambo hilo pia linapaswa kufanyika katika maeneo mengine ili kutengeneza nguvu kubwa zaidi kwani mauaji na upotevu wa watoto vimekuwa vikiripotiwa pia katika wilaya na mikoa mingine ya nchi yetu.

Tahariri ya Mwananchi,

Mwananchi Communications Limited (MCL)

S.L.P. 19754 Dar es Salaam-Tanzania

SIMU +255222450875 au +255754780647