http://www.swahilihub.com/image/view/-/4782502/medRes/2124995/-/b7mv3s/-/usailko.jpg

 

Ni muhimu kulitafakari soko la ajira msimu wa kuhitimu

Usaili wa ajira

Usaili wa ajira. Picha/FOTOSEARCH 

Na PROFESA HONEST NGOWI

Imepakiwa - Thursday, November 8  2018 at  13:10

Kwa Muhtasari

Katika utafiti wa soko la ajira imejitokeza mara nyingi kuwa pamoja na utaalamu unaofundishwa darasani, waajiri hutafuta na kuhitaji sifa za ziada kutoka kwa wahitimu.

 

KILA mwaka tunashuhudia wanafunzi wakihitimu katika ngazi mbalimbali za elimu nchini.

Kuanzia shule za msingi, kidato cha nne, sita na vyuo hata vyuo vikuu.

Kwa wahitimu wa vyuo jambo muhimu baada ya kuhitimu ni kuingia katika soko la ajira ambalo lina sura kuu mbili; kuajiriwa au kujiajiri.

Wahitimu wanahitaji elimu kuhusu soko la ajira ambayo ni muhimu kwao kwa sababu baadhi yao watataka kuajiriwa na wengine kujiajiri. Hata hivyo sio wote watafanikiwa kuajiriwa au kujiajiri.

Ni vizuri kwa wahitimu, wazazi, walezi na taasisi za elimu kuelewa kwa nini kuna ukosefu wa ajira katika soko.

Kimsingi na kadiri ya kanuni za uchumi, ajira zinategemea uhitaji huduma au bidhaa sokoni.

Pale uhitaji wa nguvukazi unapokuwa mkubwa kuliko ugavi kwa maana ya kuwa na wahitimu wachache kuliko wanaotakiwa sokoni kunakuwa hakuna tatizo la ajira.

Hii hutokea pia idadi ya wahitimu inapokuwa sawa na mahitaji sokoni.

Hata hivyo, wahitimu wanapokuwa wengi kuliko mahitaji basi kunakuwapo na tatizo la ajira. Ieleweke kuwa uhitaji huu ni wa idadi na ubora.

 

Waajiri

Jambo muhimu katika kuelewa kwa nini kunakuwa na ukosefu wa ajira ni kuelewa sababu za waajiri kuajiri.

Kiuchumi, waajiri wataajiri tuu kunapokuwa na uhitaji wa bidhaa au huduma zinazozalishwa na waajiri husika.

Bidhaa na huduma zinazozalishwa ndizo huuzwa ili kupata fedha za kulipia gharama za uzalishaji. Hivyo hakuna mantiki ya kiuchumi kwa waajiri kuajiri kama hamna uhitaji wa bidhaa na huduma wanazozalisha.

Kwa upande mwingine uhitaji wa bidhaa na huduma hutegemea uwezo wa wateja kununua. Uwezo huu nao hutegemea kipato cha wateja kinachopatikana kutoka, pamoja na vyanzo vingine, kwenye ajira.

Hivyo ni mzunguko mpana ambao unaweza kufanya kukosekana kwa ajira na kipato katika awamu moja kusababisha kukosekana fedha ya kununua bidhaa au huduma hivyo kupungua uhitaji wa bidhaa na huduma.

Waajiri hutazama mambo mengi kwa wanaojitokeza kutafuta ajira. Lengo lao sio kuajiri bali kupata nguvukazi itakayowawezesha kumudu ushindani uliopo sokoni. Hivyo, wanataka watu madhubuti wenye ubora wa hali ya juu.

Miongoni mwa mambo wanayotazama ni pamoja na utaalamu uliosomewa darasani ambao unaweza kuwa uchumi, uhasibu, uhandisi, rasilimali watu au mawasiliano.

Sifa za ziada

Katika utafiti wa soko la ajira imejitokeza mara nyingi kuwa pamoja na utaalamu unaofundishwa darasani, waajiri hutafuta na kuhitaji sifa za ziada kutoka kwa wahitimu.

Kwa tafsiri isiyo rasmi sifa hizi ni ujuzi laini au kama unavyoitwa, (soft skills). Sifa hizi zinatofautiana kutoka mwajiri mmoja hadi mwingine.

Hata hivyo sifa za msingi zinazotakiwa ni pamoja na uwezo wa kufanya kazi na kushirikiana na wengine kimtazamo, kiumri, kiujuzi, au kimaumbile. Hii ni pamoja na uwezo wa kuwa katika timu mbalimbali.

Pia wanataka wahitimu wanaojiamini na wenye uwezo wa kuwasiliana. Katika uwezo wa mawasiliano mambo ya msingi sio kuzungumza tu bali uwezo wa kusikiliza, kuandika na kuwa na lugha sahihi ya mwili katika mazingira tofauti.

Mawasiliano yanajumuisha yafanywayo na viongozi na wafanyakazi wengine sehemu ya kazi, wateja, mamlaka kama Serikali, watoa huduma au vyombo vya habari.

Waajiri wanataka ubunifu, uvumilivu, ujasiri, kujituma, uwezo wa kufanya mambo mengi kwa wakati mmoja, kujitoa, kuwa na mitazamo mipana, kuwa na mitandao na uwezo wa kubadilika kulingana na mazingira.