Ni wakati wa kupitia upya mikataba yote

Nehemiah Osoro

Mwenyekiti wa Kamati ya Madini Profesa Nehemiah Osoro (aliyesimama) akifuatiwa na Spika wa Bunge Job Ndugai, Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan na baadaye Rais Magufuli. Picha/MWANANCHI 

Na MHARIRI - MWANANCHI

Imepakiwa - Tuesday, June 13   2017 at  10:12

Kwa Mukhtasari

Tumefuatilia kwa umakini mkubwa uwasilishwaji wa ripoti za kamati maalumu zilizoundwa na Rais John Magufuli kuchunguza biashara ya mchanga inatofanywa na Kampuni ya Madini ya Acacia.

 

TUMEFUATILIA kwa umakini mkubwa uwasilishwaji wa ripoti za kamati maalumu zilizoundwa na Rais John Magufuli kuchunguza biashara ya mchanga inatofanywa na Kampuni ya Madini ya Acacia.

Kamati ya kwanza iliyopewa jukumu la kuchunguza makinikia yaliyomo katika makontena ya mchanga wa madini kutoka migodi ya Buzwagi na Bulyanhulu iliwasilisha ripoti yake mwezi uliopita.

Kamati ya pili ya kuchunguza masuala ya kisheria na kiuchumi kuhusiana na mchanga wa madini  unaosafirishwa kwenda nje ya nchi iliwasilishwa Jumatatu.

Kamati zote mbili zimebainisha kwamba kumekuwa na udanganyifu mkubwa katika utoaji ripoti za kiasi cha madini yaliyomo kwenye makontena, sio yale 277 yaliyozuiwa na Serikali bali biashara ya mchanga huo kwa jumla.

Aidha, ripoti ya Jumatatu imefafanua kwa kina kwamba chimbuko la udanganyifu mkubwa katika utangazaji wa mapato liko kwenye sheria. 

Kwamba haukufanywa na wahalifu au wageni bali na Watanzania wenzetu tena  waliopewa majukumu ya kulinda rasilimali hizo kwa njia ya sheria.

Kwa mfano, wakati kamati inaangalia uhalali wa kisheria wa Kampuni ya Acacia Mining nchini Tanzania imedai kuwa kwa mujibu wa nyaraka na maelezo kutoka Ofisi ya Msajili wa Kampuni (Brela), kuwa Kampuni ya Acacia Mining haikusajiliwa nchini Tanzania na wala haina hati ya utambuzi kwa mujibu wa Sheria ya Kampuni, Sura 212.

Pia, kamati imebaini kuwa Kampuni ya Acacia  Mining  ambayo inajinasibisha kuwa  mmiliki wa Kampuni ya  Bulyanhulu Gold Mines Ltd, North Mara Gold Mines Ltd na Pangea Minerals Ltd haikuwahi kuwasilisha nyaraka wala taarifa yoyote kuonyesha kuwa kampuni hiyo ni  mmiliki wa Kampuni hizo na kuwa na hisa katika kampuni hizo.

Hata hivyo inahitaji mjadala mrefu kuhusu hilo kwani inashangaza kuona kuwa kampuni kubwa kama hiyo ifanye biashara kwa muda wote huo, ilipe kodi na iwepo kwenye soko la hisa bila kuwa na usajili.

Kama haina leseni basi itakuwa inafanya biashara ya madini hapa nchini kinyume na sheria za nchi.

Hata hivyo tunaunga mkono mapendekezo yote yaliyotolewa na Kamati.

Kuchenjua

Serikali ianzishe utaratibu utakaowezesha ujenzi wa kiwanda cha uchenjuaji wa makinikia ili kuondoa upotevu wa mapato na kutengeneza ajira kwa Watanzania.

Pia, Serikali ifanye uchunguzi na kuchukua hatua  za kisheria dhidi ya waliokuwa mawaziri, wanasheria na manaibu wao, wakurugenzi wa idara za mikataba na makamishna wa madini, wanasheria wa wizara ya Nishati na Madini.

Vilevile watumishi wengine wa Serikali na watu wote waliohusika katika kuingia mikataba ya uchimbaji madini na kuongeza muda wa leseni, watumishi na wamiliki wa kampuni za madini.

Mwisho, kutokana na madudu haya yaliyobainika baada ya nia njema ya Rais Magufuli kuhakikisha rasilimali za nchi zinatumika  kwa manufaa ya taifa, tunasubiri Serikali ipitie na kufumua mikataba yote inayohalalisha rasilimali zetu kuibwa kwa kigezo cha uwekezaji.

Tunaamini kuwa suala la mikataba mibovu liko katika  sekta mbalimbali za Serikali na pengine huu uwe ni mwanzo wa mikataba hiyo  pia kuangaliwa upya.

Baadhi ya mikataba hiyo ni ile ya vitega uchumi, sekta ya utalii na maliasili. Huu ni wakati wa kuhakikisha mgogoro uliopo Loliondo unamalizika na ikiwezekana  ziundwe kamati maalumu kama  ilivyouwa kwa kamati ya madini.

Tahariri ya Mwananchi,

Mwananchi Communications Limited (MCL)

Tanzania.