http://www.swahilihub.com/image/view/-/4752016/medRes/2104914/-/yjr4u0/-/teleza.jpg

 

Nyota wa kuteleza kwenye barafu

Gideon Mutua

Gideon Mutua ni nguli wa mchezo wa kuteleza katika barafu. Picha/CHRIS OMOLLO 

Na PAULINE ONGAJI

Imepakiwa - Monday, September 10  2018 at  09:48

Kwa Muhtasari

Gideon Mutua, kijana ambaye mbali na kuwa mmojawapo wa wachezaji wakuu wa mchezo wa kuteleza kwa viatu vya magurudumu, anapigiwa upatu kuwa mmojawapo wa wanaspoti maarufu wa mchezo wa kuteleza kwenye barafu (ice-skating) nchini.

 

WENGI watakubaliana nami kuwa mchezo wa kuteleza kwenye barafu hauko miongoni mwa spoti maarufu sio tu hapa Kenya, bali barani Afrika kote.

Lisilowezekana kwa wengi limekuwa kawaida kwa Gideon Mutua, kijana ambaye mbali na kuwa mmojawapo wa wachezaji wakuu wa mchezo wa kuteleza kwa viatu vya magurudumu, anapigiwa upatu kuwa mmojawapo wa wanaspoti maarufu wa mchezo wa kuteleza kwenye barafu (ice-skating) nchini.

Ni mchezo ambao amekuwa akiushiriki kwa miaka mitatu sasa ambapo alianza kwa kujihusisha na speed skating, mchezo unaohusisha kuteleza kwa viatu vya magurudumu barabarani.

Na ustadi wake tayari umeanza kujitokeza kwani katika umri mdogo wa miaka 18, mwanafunzi huyu wa kidato cha pili katika shule ya upili ya Golden Light, mtaani Huruma, jijini Nairobi, ameanza kujiundia jina katika ngazi za kimataifa.

Huu sio utani kwani majuma mawili yaliyopita aliwakilisha mtaa wake wa Kariobangi na taifa la Kenya kwa jumla katika mashindano ya hockey ya kuteleza (Ice Hockey Championship) nchini Canada majuma mawili yaliyopita.

Lakini usione ufanisi wake ukapumbazwa kwani shughuli hii inahitaji bidii na nidhamu ya hali ya juu. Kwa hivyo siku tatu kwa wiki utampata na wenziwe wakifanya mazoezi kwa uwanja wa pekee wa kuteleza kwenye barafu wa Panari, katika barabara ya Mombasa Road, Nairobi.

“Lazima nifanye mazoezi kila Jumatano usiku, Jumamosi asubuhi na Jumapili mchana kutwa. Nimechagua siku hizi ili shughuli hii isiathiri ratiba yangu ya kawaida shuleni,” anaeleza.

Na uamuzi huu wa kuwa na siku hususan za mazoezi umemwezesha kusawazisha majukumu yake kama mwanaspoti na mwanafunzi kwani masomo yake hayajaathirika.

Ari yake ya kujihusisha na mchezo huu ilianza tokea utotoni huku akifurahishwa na baadhi ya watoto mtaani ambao walikuwa wamekumbatia mchezo wa kuteleza kwa viatu vya magurudumu.

“Nilikuwa mdogo kulikuwa na vikundi vya watoto wenzangu ambao walikuwa wakishiriki mchezo wa kuteleza kwa viatu vya magurudumu ambapo nilitamani sana kujiunga na ni wao walionifanya nitamani hata mimi kushiriki,” anasema.

Alikuwa mmoja wa vijana walionufaika na mradi wa Hope Raisers ambapo walikuwa na mazoea ya kufanya mazoezi barabarani. Ni hapa ndipo alijiunga na Hope raisers, mradi wa kuimarisha michezo, sanaa na muziki mwaka wa 2012 ambapo alishiriki kwa mwaka mmoja. 

Ni akiwa hapa ndipo aikutana na kocha Yunus Ali ambaye baadaye alimtambulisha kwenye mradi wa Sky skaters unaohusika na mchezo wa kuteleza kwenye barafu mwaka mmoja baadaye.

“Baada ya muda alinisaidia kujiunga na kikosi cha timu ya mchezo wa kuteleza kwenye barafu upande wa watoto,” anaeleza.

Ufanisi wake umemuongezea umaarufu sio tu shuleni, bali pia mtaani anakoishi huku wazazi wake ambao awali walikuwa na tashwishi kuhusu kujihusisha kwake na mchezo huu wakimshabikia pakubwa.

Changamoto

Hata hivyo, haimaanishi kwamba hakuna changamoto huku tatizo la kutokuwa na vifaa vya kutosha kwenye mchezo huu likiwa kizingiti cha jitihada zake.

“Mchezo huu unahitaji vifaa vingi ambapo vingi ni vya bei ghali na havipatikani kwa urahisi. Kwa mfano viatu maalum vya kuteleza” anaeleza.

Kadhalika haijakuwa rahisi kwa mvulana huyu kukabiliana na dhana za watu kuhusiana na mchezo huu.

“Sio wengi wanaoninichukulia kwa makini kila mara nikipita mtaani na begi kubwa la vifaa vyangu vya mchezo huu,” anaeleza.

Hii kamwe haijazima ndoto yake ya kuimarisha kipaji chake katika mchezo huu ambao kwa wengi sio wa Kiafrika, na hivyo kubadilisha mtazamo wa wengi na kuwashawishi vijana zaidi nchini kuushiriki.