http://www.swahilihub.com/image/view/-/4880254/medRes/2188272/-/vgjmdwz/-/mjiji.jpg

 

MAPISHI: Omena au dagaa

Omena

Omena zilizopikwa zikapikika; hapa kuna ugali. Picha/SAMMY WAWERU 

Na SAMMY WAWERU

Imepakiwa - Tuesday, December 4  2018 at  11:46

Kwa Muhtasari

Omena au dagaa ni chakula kinachopendwa sana na wakazi wa eneo la Nyanza; sababu kuu ikiwa kwamba huko zinapatikana kwa urahisi.

 

OMENA ni aina ya samaki wadogo maarufu kama dagaa.

Dakika 10 zinatosha kuandaa viungo, na mapishi ya dakika 30.

Vinavyohitajika

  • Omena zilizokauka (kiwango ni kwa mujibu wa idadi ya walaji)
  • Nyanya
  • Fungu moja la giligilani
  • Vitunguu vya mviringo
  • Mafuta
  • Chumvi
  • Maziwa au maji kiasi

Namna ya kuziandaa

Baada ya kuchambua omena, zioshe mara kadha kwa maji fufutende. Zikamuliwe na kutiwa kwenye sufuria au kikaangio kilichoinjikwa mekoni, zikaushwe kwa karibu dakika 20 hivi.

Wakati shughuli hiyo inaendelea, nyanya na vitunguu viandaliwe. Dagaa zile zikikauka zitiwe mafuta, na kuzigeuza mara kadha.

Kwa kutumia kijiko, zisongeshwe pembezoni mwa kikaangio kisha viungo; mchanganyiko wa nyanya na vutunguu utiwe sehemu ile na kumimina hapo mafuta kiasi.

Viungo hivyo viive hadi vibondeke, halafu omena ziwekwe juu yake na kuchanganywa kwa kuzigeuzageuza. Mpishi anashauriwa kupunguza kiasi cha moto.

Tia vipande kadhaa vya giligilani, kisha maziwa kiasi na yakikosekana maji yatachukua mahala pake.

Ongeza chumvi na uwe makini kutopitisha kiasi chake.

Zinapokuwa tayari hubadili rangi kuwa kahawia.

Kachumbari itaongeza ladha kwa mlo huo unaoliwa sana na ugali.