http://www.swahilihub.com/image/view/-/4878538/medRes/494035/-/fakau5/-/Laptop.jpg

 

Uchambuzi: Ongeza ujuzi ushindane katika soko la ajira

Laptop

Kujua jinsi ya kutumia kipakatalishi ni njia mojawapo ya kujiimarisha na kuongeza uwezekano wa kufaulu kazini. Hii picha ni ya watoto wakifurahia teknolojia mpya. 

Na KALUNDE JAMAL

Imepakiwa - Monday, December 3  2018 at  08:04

Kwa Muhtasari

Kitu pekee kitakachokutofautisha na wengine ni kuwa na ujuzi wa ziada tofauti na fani uliyosomea, bila kusahau masuala yote yanayohusu teknolojia uwe na uelewa nayo hata kidogo.

 

VIJANA wengi wamekuwa wakilalamika kuitwa kwenye usaili na kisha kutoitwa tena kwa ajili ya ajira.

Wapo wanaolalamika kufanya hivyo zaidi ya mara tano na kufikia kukata tamaa.

Kabla hujakata tamaa jiulize kwanza unakosea wapi, inawezekana kuna vitu vinakukwamisha kufikia malengo yako.

Inakupasa kuwa mbunifu zaidi hasa wakati huu ambapo zaidi ya wahitimu 700,000 wanaingia kwenye soko la ajira kila mwaka.

Ndiyo maana zinapotangazwa nafasi za kazi mbili wanakuja waombaji 2000, hivyo unapawa uwe na kitu tofauti miongoni mwa hao wote.

Kitu pekee kitakachokutofautisha na wengine ni kuwa na ujuzi wa ziada tofauti na fani uliyosomea, bila kusahau masuala yote yanayohusu teknolojia uwe na uelewa nayo hata kidogo.

Waajiri mbali na vyeti vya fani unayoomba kuna vitu tofauti wanavipa nafasi ambavyo kama muombaji kazi kijana unapaswa kuwa navyo.

Inawezekana siyo waajiri wote wanataka anayeomba kazi kwao awe na sifa za ziada zaidi ya fani husika aliyosomea na kuombea kazi, lakini walio wengi hupenda kupata mfanyakazi wa aina hiyo.

Pamoja na kuwa na ujuzi tofauti na vyeti husika unapaswa kujitahidi kuhakikisha mwajiri wako anajua kuwa na una sifa ya ziada.

Jambo hilo hakikisha unalifanya wakati wa mahojiano ya kazi, siyo lazima kila kitu ukijaze kwenye wasifu wa kuomba kazi.

Miongoni mwa vitu vitakavyokupa nafasi tofauti na wenzako ni kuwa na uwezo wa kuwasiliana, kwa maana ya kuandika kwa ufasaha na mtiririko unaoeleweka, kuzungumza kwa staha na vituo.

Inajulikana licha ya Kiswahili kupigiwa debe kitumike hapa nchini, usisahau kwenye masuala ya kazi lugha inayotumika ni Kiingereza, hivyo ukiweza kuwasiliana kwa kuandika, kusoma lugha hiyo utakuwa kwenye nafasi nzuri.

Muhimu ni kuwa msikilizaji mzuri, licha ya kufahamu lugha ukiwa unazungumza wewe tu bila kusikiliza hutapata nafasi wataona wanaajiri mtu mbishi.

Sidhani kama kuna mwajiri atamuajiri mfanyakazi hata kama ni kiwandani anayechanganya maneno kwenye R anaweka L na kwenye L anaweka R.

Jambo lingine ni kuwa na uwezo wa kufanya kazi zaidi ya moja. Teknolojia imekuwa sana na waajiri wanapunguza gharama kwa kuajiri wafanyakazi wachache wanaboresha miundombinu na kuwaacha wafanye kazi zaidi ya moja.

Si vibaya pia ukiijua kompyuta kwa sababu siku hizi vitu vingi vinatumia mtandao. Usibweteke kutokana na kozi uliyosomea kutohitaji utaalamu huo, ukiijua unakuwa kwenye nafasi nzuri ya kuajiriwa na ukipata kazi hutokuwa mzigo kwako mwenyewe na unaofanya nao kazi.

 

Kuwasha kipakatalishi ni balaa!

Haitakuwa busara unafika kazini hata kuwasha laptop hujui, kufungua barua pepe yako mwenyewe hadi uwaite watu wa kitengo cha Tehama, wafanyakazi wenzako watakudharau na mwajiri kabla ya kukupa kazi ataliangalia hilo.

Hivyo jifunze vitu muhimu kama kuwasha kompyuta, kuzima, kuandika kwa haraka bila kubabaika babaika, kufungua mahali pa kuandikia (Microsoft Word) na matumizi ya namba na maandishi kwa kutumia kompyuta (Microsoft Excel).

Hivi ni baadhi ya vitu vitakavyokutofautisha na wengine katika ajira, bila kusahau kuijua vema fani uliyosomea na kuwa na uwezo wa kujieleza.

Takwimu zinaonyesha kuwa kwa wastani soko la ajira nchini lina uwezo wa kuzalisha ajira zipatazo 300,000 kwa mwaka katika sekta rasmi ukilinganisha na wastani wa wahitimu 600,000 hadi 800,000 wanaoingia katika soko la ajira nchini.

Anayepaswa kukabiliana na tatizo hili la ajira ni kijana mwenyewe kwa kuhakikisha anajipanga kwa ajili ya kujiajiri siku za usoni tangu akiwa masomoni.

Wakati umefika wa vijana kuachana na mawazo mgando kuwa ukiwa msomi lazima ufanye kazi ofisini kwenye kiti cha kuzunguka badala yake maamuzi yafanyike mapema kwa kuliondoa hilo kichwani.

Kwa kufanya hivyo kijana anapaswa kujiandaa kujiajiri kwa kutumia taaluma yake.