Uvuvi: Operesheni zizingatie haki za binadamu

Na MHARIRI – MWANANCHI

Imepakiwa - Friday, February 1  2019 at  10:49

Kwa Muhtasari

Mambo si shwari katika sekta ya uvuvi nchini Tanzania hasa kwenye mikoa inayopakana na Bahari ya Hindi.

 

MAMBO si shwari katika sekta ya uvuvi kwenye mikoa inayopakana na Bahari ya Hindi. Katika maeneo mengi samaki kama kitoweo kikubwa kwa watu wengi wameadimika. Moja ya sababu ya hali hii ni kusuasua kwa shughuli za uvuvi.

Wavuvi wana malalamiko yao. Hivi karibuni wavuvi hao kupitia umoja wao walitangaza kufanya mgomo ili kuishinikiza Serikali kukomesha vitendo vya unyanyasaji kutoka kwa baadhi ya maofisa wake.

Wanachokisema wavuvi ni kile wanachokabiliana nacho katika shughuli zao za kila siku. Ni wajibu wa mamlaka husika kusikia kilio chao na kukifanyia kazi ili utendaji wa sekta ya uvuvi irejee katika hali yake.

Tunatambua kuwa hivi sasa Wizara ya Mifugo na Uvuvi inaendesha Operesheni Sangara inayolenga kuzuia vitendo vya uvuvi haramu vilivyokithiri katika maeneo mengi nchini. Lakini pia kuna operesheni ya kukagua leseni za uvuvi. Pamoja na umuhimu wake, michakato hii yote haina budi kufanywa kwa kuzingatia misingi ya haki za binadamu, sheria na ustaarabu.

Tungependa harakati za kupambana na uvuvi haramu ziwe endelevu ili kuiepusha jamii ya Kitanzania na madhara yatokanayo na uvuvi wa aina hiyo. Hata hivyo, tunawiwa kuvisihi vyombo husika vikiwamo vile vya dola kutafuta namna bora zaidi ya kuendesha harakati hizi.

Isifike mahala sasa Watanzania wakajenga akilini mwao kuwa kila inapoanzishwa operesheni fulani, basi ndio wakati wao wa kukaa roho juu. Haya tumeyaona katika operesheni kadhaa siku za nyuma. Zipo ambazo Serikali ililazimika kuunda tume kuchunguza baada ya kuendeshwa kwa njia tunazodiriki kusema zilikuwa za kinyama.

Ni vyema kila operesheni ilenge kurekebisha na kuboresha suala husika, isiwe kama vyanzo vya kukiuka haki za binadamu.

Hatudhani kwa mfano, Operesheni Sangara inayoendelea sasa ije kuibua hofu na sintofahamu kwa wananchi. Hili litukumbushe Mei 2018 pale Kamati ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi ilipohoji utekelezwaji wake ikisema umegubikwa na ubabe na vitisho.

Ifike mahali watendaji serikalini wajifunze kutokana na makosa ya zamani, kwa nini kila kunapokuwapo operesheni fulani hakukosi kuwapo manung’uniko na hata vilio?

Huko nyuma tumewahi kushuhudia operesheni kadhaa ambazo pamoja na dhamira njema ziliishia kuibua matatizo zaidi kwa wananchi na hata Taifa.

Tunasisitiza kuwa pamoja na nia njema ya wizara na Serikali kwa jumla katika kudhibiti vitendo vya uvuvi haramu, uendeshaji wa operesheni hii hauna budi kujali haki za msingi za raia ikiwamo ile ya kuishi.

Maelekezo

Katu hatuamini kwamba kinachofanywa na baadhi ya maofisa katika operesheni hizi ni maelekezo ya viongozi wa Serikali.

Huu ni udhaifu wa kiuwajibikaji wa baadhi ya watendaji hao waliokabidhiwa jukumu hilo.

Kuwafumbia macho watendaji hawa kuna athari nyingi ikiwamo ya wananchi kujenga hisia ya chuki na hata kukosa imani na Serikali yao ambayo kimsingi inapaswa kuwa mtetezi na mlinzi wa haki zao.

Kwa sasa na hata baadaye, tunahitaji operesheni ambazo utekelezwaji wake utawagusa na kuwakosha Watanzania wengi zaidi, badala ya kila mara kuacha majeraha na vilio kwa wananchi. Operesheni hizo lazima zizingatie miiko ya kisheria, staha na ustaarabu wa Kitanzania.

Tahariri ya Mwananchi,

Mwananchi Communications Limited (MCL)

S.L.P. 19754 Dar es Salaam-Tanzania

SIMU +255222450875 au +255754780647