http://www.swahilihub.com/image/view/-/3500632/medRes/1523070/-/gfqxap/-/polia.jpg

 

Polisi hawakustahili kupelekwa bungeni

Lori la maafisa wa polisi

Lori la maafisa wa polisi laondoka karibu na majengo ya Bunge baada ya Spika wa Seneti kushauri umuhimu wa vikao vya seneti kuendeshwa bila kiwewe Desemba 28, 2016. Picha/JEFF ANGOTE 

Na MHARIRI - TAIFA LEO

Imepakiwa - Thursday, December 29  2016 at  09:18

Kwa Mukhtasari

Bunge la Seneti lilipokutana Jumatano, kulikuwa na matumaini makubwa miongoni mwa Wakenya kwamba lingetoa suluhu kwa mzozo kuhusu Marekebisho ya Sheria za Uchaguzi.

 

BUNGE la Seneti lilipokutana Jumatano, kulikuwa na matumaini makubwa miongoni mwa Wakenya kwamba lingetoa suluhu kwa mzozo kuhusu Marekebisho ya Sheria za Uchaguzi.

Kikao cha asubuhi kilikumbwa na taharuki kutokana na hatua ya serikali kutuma maafisa wa polisi katika majengo ya bunge.

Maafisa hao waliokuwa na sare rasmi na silaha, pia walikuwa na malori matatu yaliyojaa maji yenye pilipili, ambayo kawaida hutumiwa wakati wa ghasia na maandamano.

Jambo hilo liliwakera maseneta, ambao walilalama kwa Spika, Bw Ekwee Ethuro kwamba walilazimishwa kuacha magari yao na kutembea. Pia walilalama kwamba hawakualika maafisa hao kutoa ulinzi wowote.

Hata kiongozi wa wengi katika bunge hilo, Profesa Kindiki Kithure, alishangaa kuwa mtu mmoja au watu serikalini, waliamua kutuma maafisa hao wa usalama katika majengo ya bunge kana kwamba kulikuwa na ghasia.

Tabia hii ya kuwatumia polisi vibaya inafaa kukoma.

Waziri wa Usalama wa Ndani, Jenerali Joseph Nkaissery anapaswa kutafakari kazi halisi ya polisi.

Kuwatuma maafisa hao kwenda nje ya majengo ya bunge la Seneti wakati ambapo maseneta wanajadili suala lililoibua utata, ni sawa na kufanya wananchi waamini kuwa sheria inayojadiliwa ni mbaya na lazima ipite 'wapende, wasipende'.

Kerio Valley

Kama alivyosema Seneta wa Pokot Magharibi, Profesa John Lonyangapuo, Kenya inakumbwa na utovu wa usalama maeneo ya Bonde la Kerio, Baringo na hata kwenye kaunti za mpaka na Somalia.

Maafisa wetu wa usalama wanastahili kuwa katika maeneo kama hayo, na wala si kuwatumia kuwatisha wabunge ambao wamekomaa na wanaelewa kazi yao.

Aidha, uamuzi wa Spika Ethuro kuwahusisha wananchi kwenye mjadala wa sheria hiyo kupitia kamati ya Seneta Amos Wako, unastahili kupongezwa.

Kama wanavyosema Waswahili, kawia ufike, hakuna haja ya kuharakisha kupitisha sheria ambayo inazua utata.

Hata hivyo, ni matumaini ya wengi kwamba seneti haiwashirikishi wananchi kwa kutaka sifa tu. Ni sharti maoni yatakayotolewa na wadau waliofika mbele ya Bw Wako yazingatiwe kwa makini na yale yatakayokuwa na uzito yahusishwe kwenye mjadala.

Ni kupitia uzingatiaji wa sheria kuhusu kushirikisha umma, ambapo tutakuwa tukiunda sheria zitakazokubaliwa na wote.