http://www.swahilihub.com/image/view/-/4725262/medRes/2087213/-/oickqlz/-/mambosasa.jpg

 

Polisi wetu wasijiingize katika siasa

Lazaro Mambosasa

Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa. Picha/MAKTABA  

Na MHARIRI - MWANANCHI

Imepakiwa - Tuesday, December 4  2018 at  07:52

Kwa Muhtasari

  • Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Isaya Mwita mwishoni mwa wiki alikamatwa na kuwekwa ndani kwa madai kuwa alifanya maandamano bila kibali
  • Tunahitaji Jeshi la Polisi linalotenda haki na kuadhibu wakosaji, lisiloingiza siasa katika utekelezaji wa majukumu yake

 

DIWANI wa Kata ya Vijibweni ambaye pia ni Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Isaya Mwita mwishoni mwa wiki alikamatwa na kuwekwa ndani kwa madai kuwa alifanya maandamano bila kibali.

Kamanda wa Polisi wa Kanda ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa alisema meya huyo alikuwa akishikiliwa katika kituo cha polisi cha Chang’ombe na kwamba upelelezi ukikamilika atafikishwa mahakamani.

Katika ufafanuzi wake, Mambosasa alisema diwani huyo alikuwa anaongoza maandamano bila kutoa taarifa polisi.

Mwita anadaiwa kukamatwa wakati alipokuwa anakwenda kutekeleza jukumu la kuzindua kisima cha maji katika moja ya miradi iliyopo kwenye kata anayoiongoza.

Kamanda Mambosasa alidai baada ya kumhoji Mwita alisema alikuwa anakwenda kuzindua kisima ambacho kilijengwa na Serikali kupitia kwa mkuu wa wilaya aliyehamishiwa Ruangwa.

Mambosasa alisema “sasa yeye (Mwita) alikuwa anataka kupora mradi ule ili kutafuta sifa kwamba alijenga yeye wakati mradi ni wa Serikali na aliokuwa amewaalika walikimbia wote”.

Maelezo ya Mambosasa yanathibitisha kwamba meya alikuwa anakwenda kuzindua kisima na hakuwa anafanya vurugu au kuondoa amani, bali kuleta faraja kwa wananchi wake.

Pia anakiri mradi wa kisima ambao meya alikuwa anakwenda kuzindua uko kwenye kata yake.

Hivi mkuu wa mkoa anaweza kwenda mahali asiwepo mkuu wa wilaya husika? Na au mkuu wa wilaya anaweza kuanzisha mradi wowote ule katika kijiji bila mbunge au diwani wa eneo husika kuwepo?

Je, kuna miradi ambayo si ya Serikali au polisi wanajenga dhana kwamba upinzani ni Serikali? Maana tujuavyo Serikali inaongoza kwa kutumia ilani ya uchaguzi na sera ya CCM, hivyo hata kama baadhi ya kata au majimbo yameshikwa na upinzani ukweli ni kuwa mjenzi anabaki kuwa Serikali ya CCM. Tunasema hivyo kwa sababu miradi yote hugharimiwa kwa fedha za Serikali. Iwe barabara, reli, visima, mifereji, umeme au shughuli nyingine za maendeleo, zote hutekelezwa kwa fedha za Serikali ya CCM.

Kwa hiyo kwa Mambosasa kusema meya alikuwa anataka kupora mradi wa mkuu wa wilaya ni kujiingiza katika siasa bila ya sababu. Diwani ambaye mradi uko kwenye kata yake anawezaje kuupora?

Mfano, mradi wa mabasi yaendayo kasi jijini Dar es Salaam (Dart) ulijengwa na Serikali wakati halmashauri ya jiji ikiwa chini ya CCM, lakini leo jiji liko chini ya upinzani. Sifa zote za mradi zinabaki kuwa za Serikali.

Dhana hii ya polisi dhidi ya meya haina tofauti na kilichotokea jijini Arusha Mei 18, 2017 wakati viongozi wa dini, meya, madiwani na wanahabari walipokamatwa na kuwekwa ndani walipokuwa wakitoa rambirambi katika Shule ya Awali na Msingi ya Lucky Vincent kutokana na ajali ya gari iliyotokea Mei 6 na kuua wanafunzi 32, walimu wawili na dereva.

Wengine waliokamatwa siku hiyo ni viongozi wa Shirikisho la Wamiliki na Mameneja wa Shule na Vyuo Binafsi (Tamongsco) Kanda ya Kaskazini. Ikiwa watu kushiriki katika matukio haya ya kijamii ni kosa, basi Jeshi la Polisi lifafanue sheria zinazoongoza uzinduaji wa miradi inayojengwa kwa fedha za umma ili ijulikane ni watu gani wanastahili kuizindua au kuitembelea.

Tunahitaji Jeshi la Polisi linalotenda haki na kuadhibu wakosaji, lisiloingiza siasa katika utekelezaji wa majukumu yake.

Tahariri ya Mwananchi,

Mwananchi Communications Limited (MCL)

S.L.P. 19754 Dar es Salaam, Tanzania

SIMU +255222450875 au +255754780647