http://www.swahilihub.com/image/view/-/2945074/medRes/1168738/-/8an8yiz/-/MagufuliRais.jpg

 

Pongezi kwa Rais Magufuli kutimiza miaka miwili

Rais John Magufuli akitoa hotuba

Rais John Magufuli akitoa hotuba jijini Dar es Salaam punde baada ya kuapishwa Novemba 5, 2015. Picha/AFP 

Na TAHARIRI YA MWANANCHI

Imepakiwa - Tuesday, November 7  2017 at  11:10

Kwa Muhtasari

Novemba 5, 2017, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilipata Rais wa Tano tangu kuanzishwa kwake.

 

NOVEMBA 5, 2015, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilipata Rais wa Tano tangu kuanzishwa kwake.

Huyu ni John Pombe Magufuli aliyeapishwa kuwa Rais mpya na kushika hatamu kwa miaka mitano na akishinda tena ataongoza hadi mwaka 2025.

Anafuata nyayo za Rais Julius Nyerere ambaye ni mwasisi wa Tanzania.

Wengine ni Ali Hassan Mwinyi, Benjamin Mkapa na Jakaya Kikwete ambao waliongoza Taifa kwa vipindi viwili mfululizo isipokuwa Mwalimu Nyerere.

Mengi yametokea tangu Novemba 2015 alipoanza urais.

Baadhi yameonekana mapya na mengine yakiwa ni mwendelezo huku baadhi yakifurahisha na ya kutia matumaini, kuhuzunisha, kuchukiza na kupoteza matumaini.

Hii ni kutokana na mapokeo tofauti ya hatua ambazo zimekuwa zikichukuliwa na Serikali ya Awamu ya Tano ambayo imeeleza kuwa imepania kudhibiti matumizi yasiyo ya lazima, kukusanya kodi, kupambana na ufusadi wa kila aina, uzembe, ukosefu wa uwajibikaji ili kujenga nchi yenye uchumi wa kati unaotegemea viwanda ifikapo mwaka 2025.

Ni dhahiri kuwa hatua kadhaa zimechukuliwa na kuonyesha matunda kama vile upunguzaji wa gharama zilizokuwa zikitokana na malipo ya wafanyakazi hewa, kusafisha utumishi wa umma kwa kuondoa wafanyakazi wenye vyeti vya kughushi, wazembe na warasimu kushughulikia wakwepakodi.

Hali kadhalika Serikali imetekeleza mikakati yake kama ya kutoa elimu bure kwa kutenga na kutoa fedha za ruzuku kila mwezi, kuanzisha miradi mikubwa kama ujenzi wa reli, ununuzi wa ndege, ujenzi  wa bomba la mafuta na azma ya muda mrefu ya kuhamisha makao makuu mjini Dodoma.

Katika huduma za jamii, Serikali imejikita katika kuboresha huduma za afya kwa kuongeza fedha  za bajeti, kuanza kutoa vitambulisho kwa wazee ili wapate huduma za afya bure, kuboresha huduma za hospitali kadhaa, kuondoa urasimu katika upatikanaji wa hati za ardhi na mengine mengi.

Tunaipongeza Serikali kwa hatua hizo na ni muhimu kwa wahusika kuanza kutathmini utekelezaji wa mikakati hiyo ili kujua kuna mafanikio gani na kuboresha njia zilizotumika kuyafikia na kujua udhaifu ulipo ili kutafuta njia zilizotumika kuyafikia na kujua udhaifu uliopo ili kutafuta njia za kuuondoa.

Pia kuna masuala ambayo yanaonekana hayajashugulikiwa vizuri na Serikali. Wafanyabiashara bado wanalalamikia mazingira ambayo si rafiki wanayokumbana nayo na ambayo wanaamini yakishughulikiwa yataweza kusaidia biashara kuimarika na hiyo kuwanufaisha wananachi na uchumi kwa jumla.

Pia yamekuwapo na matukio yasiyo ya kawaida kama ya viongozi wa vijiji kushambuliwa huku Jeshi la Polisi likiwa halitoi taarifa ya juhudi zinazofanywa kama kukamata wahusika na kuwafikisha mahakamani, mashambuizi  dhidi ya wanasheria na wanasiasa, utekaji na ukamataji wa wanasiasa.

Haya yamelalamikiwa sana na hayajakuwa na majibu yanayoweza kutosheleza kiasi cha kuwafanya walalamikaji na wanaofuatilia kuona kama kuna kitu kinaendelea ambacho kinaweza kuwahakikishia usalama na amani.

Wanasiasa wanalalamika kukosa mazingira rafiki ya kuendesha siasa ambayo ni pamoja na  kuchukua uozo pale wanapoona unaendelea kukua, kuikosoa Serikali na watendaji wake lakini pia viongozi wa kitaifa wa vyama kukutana na wanahama na wafuasi  wao kwenye mikutano ya hadhara.

Kwa kuwa marufuku iliyowekwa ilikuwa na kusudio maalumu, ni dhahiri kuwa kusudio hilo haliwezi kuwa la kipindi kirefu na hiyo ni muhimu kutathmini hali ya kisiasa na kuondoa marufuku iwapo mazingira yalilazimisha kiwekwe hapo tena.

Tunaamini kuwa Serikali iiyopo madarakani ni sikivu na ustawi wa jamii na hivyo itakuwa  tayari kuendeleza yale mazuri na kuacha yasiyofaa lakini pia kusikiliza wananchi na kufanyia kazi maoni na ushauri wao.

Tahariri ya Mwananchi,

Mwananchi Communications Limited (MCL)

S.L.P. 19754 Dar es Salaam-Tanzania

SIMU +255222450875 au 0754780647