Ripoti za wanaume kuuawa Kirinyaga zasababisha hofu

Na MWANGI MUIRURI

Imepakiwa - Friday, September 14  2018 at  11:30

Kwa Muhtasari

Katika kipindi cha miezi minne iliyopita, ripoti za maafisa wa polisi zinatofautiana na zile za watetezi wa haki za kibinadamu, huku maafisa wakitangaza kuwa katika kaunti ya Kirinyaga, wanaume 91 wameuawa nao watetezi wakisema ni 107.

 

KIRINYAGA, Kenya

VISA vya vijana wa kiume kupatikana wameuawa na miili yao kukutwa imetupwa vimezua hofu katika baadhi ya maeneo ya Kaunti ya Kirinyaga, huku wanawake wakiteta kuwa matukio hayo yanawapunguzia matumaini ya kuolewa.

Katika kipindi cha miezi minne iliyopita, ripoti za maafisa wa polisi zinatofautiana na zile za watetezi wa haki za kibinadamu, huku maafisa wakitangaza kuwa wanaume 91 wameuawa nao watetezi wakisema ni 107.

Maafisa hao wanasisitiza kuwa sio vijana wote ambao walikufa katika kipindi hicho ambao walikuwa waathiriwa wa uvamizi huo, kuwa wengine waliaga dunia kupitia ajali na maradhi.

"Idadi kamili ambayo imerekodiwa rasmi ni kuwa wanaume 91 wameaga dunia katika visa vya kuuawa. Lakini ukijumuisha hata mauti mengine kwa vijana, idadi hiyo inaweza kufika hata 500," akasema kamanda wa Polisi wa Kaunti hiyo Bi Christine Mutua.

Mauti hayo yanasingiziwa kutokana aidha na misako ya polisi pamoja na makundi ya kijamii dhidi ya uhalifu, mauaji katika sakata za mapenzi au ung'ang'aniaji wa mali.

Kisingizio kingine kinachozuka katika hali hiyo ni kuwa, miongoni mwa jamii ya Kaunti hiyo kuna umang'aa wa kutojari na ukichochewa na utumizi wa mihadarati, pombe haramu za vichakani na kisha mapenzi ya kiholela, mauti yanajiangaza.

Hali hiyo imezua hali ya taharuki katika Kaunti hiyo huku serikali ya Kaunti na ile kuu zikionyesha wazi kuwa hazina uwezo wa kukomesha mauaji hayo.

Mwakilishi wa Wanawake katika kaunti hiyo Bi Wangui Ngirichi anasema kuwa hali hiyo imezua hisia za kuchanganyikiwa miongoni mwa wadau mbalimbali kiasi cha kusingiziwa ni mauaji ya kishirikina.

"Unashindwa kuelewa ni jinsi gani mauaji yazuke mara moja katika kaunti na wanaolengwa ni wanaume. Wanawake wetu wanazidi kuachwa mayatima huku walio na matumaini ya kuolewa na wanaume wa Kaunti hii wakizidi kupoteza matumaini hayo," akasema Bi Ngirichi.

Alisema kila wiki ni lazima kuripotiwe mauaji ya kati ya vijana watatu na watano wa kiume na miili yao huwa inatupwa kando mwa barabara, ndani ya mito au vindimbwi huku wenginewakitupwa katika mashamba ya mpunga.

"Kisa cha hivi karibuni na ambacho kimezua wasiwasi mwingi ni kile cha wanaume watatu ambao walipatikana wameuawa kwa njia ya kipekee na miili yao kutupwa katika mashamba ya mpunga," akasema.

Alisema kuwa vijana hao walikuwa wametolewa nguo na kubakishwa uchi wa mnyama, wakatolewa kila mmoja viatu na kuachwa na soksi moja, wakagongwa kwa kifaa butu kwa vichwa na kisha kuumizwa sehemu zao za siri.

Ujumbe

Bi Ngirichi alisema kuwa aina hiyo ya mauaji sio ya kawaida na inaashiria kuwa wauaji wanaotekeleza visa hivyo wako na ujumbe fulani wanaopitisha kwa wenyeji.

Bi Mutua alisema kuwa uchunguzi wa maafisa wake umetambua kuwa baadhi ya mauaji hayo huanzia na uvamizi wa genge likiwa na gari na kisha huwakamata waathiriwa na baada ya kuwaingiza kwa magari na kutoweka nao, hatimaye hupatikana wameuawa.

"Hatujaelewa ni kina nani ambao hutekeleza mashambulizi yao kwa njia hiyo lakini uchunguzi unaendelea. Kila mmoja wetu amewekwa katika hali ya tahadhari kujaribu kutatua shida hii," akasema.

Hata hivyo, makundi ya kutetea haki za binadamu yalidai kuwa hiyo ni kazi ya kikosi spesheli cha polisi ambacho kimeundwa katika eneo hilo kukabiliana na ujambazi.

"Mengi ya haya mauaji hutekelezwa na  maafisa wa polisi ambao wametumwa katika Kaunti hii kuzima visa  vilivyokuwa  vimekithiri vya magenge kuhangaisha wenyeji na usalama wa eneo," akasema mwenyekiti wa Kirinyaga Human Rights Outreach Programme (KHROP) Bw Silas Muriuki.

Bw Muriuki alisema kuwa nusu ya mwezi wa Julai pekee, miili 12 ilikuwa imepatikana katika maeneo tofauti ya Kaunti hiyo, yale yamezidiwa yakiwa ni Nguka, Kiangai, Kimbimbi, Kagio na Kutus.

Aliongeza kuwa visa hivyo ni sawa na zile zilizoshuhudiwa mwaka wa 2007 ambapo serikali ilikuwa ikipambana na genge haramu la Mungiki na ambapo miili ya vijana iliyokuwa imefungwa kwa kamba ilikuwa ikipatikana imetupwa kiholela katika vidimbwi na misitu.

Hata hivyo, Kamanda wa Polisi katika eneo la Mwea Magharibi ambapo miili mingi imekuwa ikipatikana Bw Mohammed Huqka alikanusha kuwepo na kikosi maalum cha kuua vijana.

"Sisemi eti hatukabiliani na majambazi. Vita dhidi yao inaendelea hadi mwisho. Lakini vikosi vyetu havihusiki kamwe na mauaji ya aina hii," akasema.

Alisema kuwa visa hivyo vinakabiliwa kama ujambazi wa mauaji na genge lisilojulikana, huku akisema uchunguzi dhidi ya mauaji hayo umeanzishwa.

Sadfa ni kwamba, Agosti 2018, Kamishna wa Kaunti hiyo Bw Joseph Keter alitangaza siku 21 za makabiliano makali na magenge nya ujambazi ambayo yalikuwa yamekita mizizi katika eneo hilo.

Katika kipindi hicho, wadau katika usalama waliagizwa wahakikishe kuwa visa hivyo vimethibitiwa na kisha wahalifu wote wanaohusishwa na kuzorota kwa usalama wa eneo hilo waandamwe kwa mujibu wa sheria.

"Tangu siku hizo zianze kuhesabiwa, ndipo visa vya miili ya vijana na ambao wamekuwa wakitambuliwa na wenyeji kama washukiwa wa ujambazi ilianza kupatikana imetupwa katika maeneo mbalimbali," akasema Bw Muriuki.

Huku ukweli wa mambo ukizidi kuwahepa wenyeji, serikali imekuwa ikitoa kila aina ya tahadhari kwa jamii haswa kuhusu visa vya wenyeji kujiteka nyara hivyo basi kuzua uhasama dhidi ya jamii na washukiwa.

Mkuu wa kitengo cha upelelezi katika Kaunti hiyo Bw Julius Rutere alisema kuwa kumeripotiwa visa vingi vya wanandoa kutoa vizingizio vya kutekwa nyara ili wapate nafasi ya kuzini nje ya ndoa.

"Makundi ya kijamii kuhusu usalama huanza kusingizia wengine katika kutekeleza utekaji nyara huo na kuzindua misururu ya kuwaua washukiwa," akasema.

Kamanda wa askari tawala Bw Zachary Mbugua alisema kuwa visasi vya kuharibiwa ndoa bado vinachangia mauti hayo.

Alisema visa kama hivyo vimekuwa vya kawaida katika eneo hilo, hali ambayo imepea Kaunti hiyo jina mbovu.

Aliwaomba watakaoathirika wasichukue sheria mikononi mwao mbali wawe wakipiga ripoti kwa maafisa wa polisi.