Sasa ni wakati wa wabunge kurudi kwa wananchi

Na MHARIRI - MWANANCHI

Imepakiwa - Friday, July 7   2017 at  18:20

Kwa Mukhtasari

Mkutano wa Saba wa Bajeti mjini Dodoma ulihusisha wabunge waliojadili na hatimaye kupitisha bajeti ya Serikali inayokadiriwa kuwa TSh31.7 trilioni.

 

MKUTANO wa Saba wa Bajeti umemalizika mjini Dodoma.

Ni mkutano uliowachukua wabunge takriban miezi mitatu wakijadili na hatimaye kupitisha bajeti ya Serikali inayokadiriwa kuwa TSh31.7 trilioni.

Kumalizika kwa mkutano huo kunatia fursa kwa watendaji katika vyombo mbalimbali vya Serikali kujipanga katika kutekeleza miradi ya maendeleo kama ilivyoidhinishwa na wabunge.

Aidha, hiki ndicho kipindi ambacho wabunge wanatarajiwa kurudi majimboni mwao ili kutoa mrejesho kwa wananchi kuhusu kile walichokuwa wakikifanya kwa muda  wote huko bungeni.

Tunatambua wabunge hawana vifungu vya fedha kama watu binafsi yaliyopitishwa  katika bajeti kwa ajili ya shughuli za maendeleo lakini bado wanaweza kupaza  sauti  na kutoa vilio  ili mamlaka zenye fedha  ziwajibike kwa ajili ya kuwaletea  wananchi maendeleo.

Nje ya kazi za bungeni kama vile kushiriki kutunga sheria kuisimamia na kuishauri Serikali, wabunge ndio wapiga debe wa wananchi, ni  wawakilishi wa kero na masaibu yote wanayokumbana nayo wananchi majimboni.

Ni kwa sababu hii tunalazimika kuwasihi wabunge kufanya hima sasa na kurudi majimboni kukaa na wananchi na kujadili kwa pamoja  namna ya kuleta maendeleo.

Tunasema hivi kwa sababu imekuwa ada kwa miaka nenda rudi wakiishi nje ya majimbo yao  lakini hata wale wanaoishi majimboni  hutumia muda mwingi nje ya majimbo yao.

Uzoefu unaonyesha aghalabu wabunge wengi wanapotoka mjini Dodoma hukimbilia na hata wengine kulowea kabisa mjini Dar es Salaam.

Bunge limekwisha, mengi yamejiri ambayo wananchi majimboni hawakubahatisha kuyasikia au kuyaona hasa baada ya kusitishwa kwa matangazo ya moja kwa moja ya vikao vya Bunge.

Huu ndio wakati kwa wabunge kurudi majimboni na kuwaeleza kinagaubaga yale yote ambayo wananchi walitakiwa kuyasikia kutoka kwa wawakilishi wao.

Muda huu ni fursa nzuri kwao kufanya vikao vya ndani na hata mikutano ya hadhara kuwaeleza wananchi ni nini inafuata kwa mustakabali wao baada ya mkutano mrefu  wa kujadili na kupitisha bajeti inayohusu maisha yao ya kiuchumi, kisiasa na kijamii.

Wabunge watambue kuwa wanapaswa kuwaelimisha wananchi kuhusu kile walichoahidi kuhusiana na bajeti waliyopitisha ili wajue maana ya vikao na hasa bajeti.

Shughuli za maendeleo ni pamoja na kuwaelewesha wananchi mikakati iliyopo na nini wanatakiwa wafanye ili wabadilishe maisha yao.

Kimsingi, hali ya maendeleo kwenye majimbo mengi si mzuri na miongoni mwa majimbo hayo ni pamoja na ya wabunge waliojipambanua kama hodari wa kujenga  hoja bungeni. Wananchi wanataka kujua uhodari huo wa kujenga hoja unamaanisha nini katika kuwaletea wananchi maendeleo na umefanikisha vipi kuboresha maisha yao.

Hata wale ambao wamekuwa wapongezaji wanalo jukumu la kuwaelimisha wananchi kuwa mambo waliyopongeza yanamaanisha nini kwa mwananchi wa kawaida na yamewasaidia vipi kuboresha maisha yao.

Sasa ni jukumu la wabunge kurudi majiMboni na kuwaunganisha wananchi.