http://www.swahilihub.com/image/view/-/3497628/medRes/1520634/-/8x1ceiz/-/nua.jpg

 

Seneti idhamirie kumaliza mgogoro

Fred Outa

Mbunge wa Nyando, Fred Outa afanya 'mambo yake' barabarani kupinga kupitishwa kwa marekebisho ya sheria za uchaguzi. Picha/MAKTABA 

Na MHARIRI - TAIFA LEO

Imepakiwa - Wednesday, December 28  2016 at  08:07

Kwa Mukhtasari

Maseneta wanakutana kwa kikao cha dharura kujadili sheria ya Uchaguzi iliyopitishwa na wenzao wa Bunge la Kitaifa wiki jana.

 

LEO hii maseneta wanakutana kwa kikao cha dharura kujadili sheria ya Uchaguzi iliyopitishwa na wenzao wa Bunge la Kitaifa wiki jana.

Kwenye kikao hicho, maseneta wa pande zote mbili (Jubilee na Cord) wana uwezo wa kuamua kama sheria hiyo itamfikia Rais Uhuru Kenyatta au wabuni jopo la maridhiano, wakiikataa.

Tayari viongozi wakuu wa upinzani, wameonya kuwa ifikapo Januari 4, wataongoza maandamano kushinikisha sheria hiyo kukataliwa.

Sababu kuu ni kwamba, kimsingi sheria ya Uchaguzi ilianza kutumika Oktoba mwaka huu na kanuni za Bunge ni kwamba, sheria haiwezi kubadilishwa kabla ya kumaliza miezi sita. Kwa hivyo, kama kungekuwa na haja ya kuifanyia marekebisho, wabunge wangelazimika kusubiri hadi Aprili 2017.

Haieleweki ni kwa nini Kiongozi wa Wengi, Aden Duale ambaye si mgeni bungeni, aliamua kupuuza kanuni muhimu za bunge hilo.

Mbunge huyo anayetumikia Garissa Mjini kwa kipindi cha pili, bila shaka alipendekeza mabadiliko hayo akijua kwamba alikuwa akivunja sheria za bunge.

Kwa hivyo, inashangaza kwamba Spika Justin Muturi aliamua kuandika ilani iliyochapishwa usiku wa manane na kisha akasindikizwa na zaidi ya polisi hamsini.

Pili, pingamizi za upinzani yamkini zina mashiko; kwamba mageuzi hayo ya sheria yanapendekeza kuwe na utumizi wa daftari la wapiga kura iwapo mitambo itafeli, kwa lengo la kuiba kura.

Maseneta watakapojadili sheria hiyo, wanapaswa kufahamu kuwa IEBC ilikuwa na miaka mitano ya kununua vifaa hivyo na kuvifanyia majaribio.

Matokeo

Isitoshe, chaguzi ndogo zote zilizopita zilifanywa kutumia mfumo huo na hata eneo la mbali kama Turkana, matokeo yalifika na kutangazwa mara moja.

Kuanza kudhania kuwa mitambo hiyo itafeli Agosti 8 ni kutaka kuiweka Kenya katika hali ya taharuki.

Maseneta kwa muda mrefu wamekuwa wakijibizana na Bunge la Taifa na kudai kuwa wao ndio walio bunge la juu.

Basi fursa hii imejitokeza kwa wao kudhihirishia ulimwengu kwamba kweli wanaongozwa na hekima, na wala si misukumo ya kisiasa.

Kenya ikitumbukia kwenye machafuko yamkini sheria hii ya uchaguzi itakuwa imechangia.