http://www.swahilihub.com/image/view/-/3843270/medRes/1584452/-/ftoqv1z/-/mkukusu.jpg

 

Serikali igeukie rasilimali misitu

Mkukusu

Mkukusu wenye urefu wa mita 81.5 ndiyo mti mrefu zaidi Barani Afrika. Picha/DKT ANDREAS HEMP 

Na TAHARIRI YA MWANANCHI

Imepakiwa - Wednesday, December 6  2017 at  09:57

Kwa Muhtasari

Ilipoingia madarakani, Serikali ya Awamu ya Tano ilianza mara moja kupambana na mambo mengi ambayo huko nyuma yalikuwa yakiachwa yatawale na hivyo kuathiri maisha ya wananchi kwa njia moja ama nyingine.

 

ILIPOINGIA madarakani, Serikali ya Awamu ya Tano ilianza mara moja kupambana na mambo mengi ambayo huko nyuma yalikuwa yakiachwa yatawale na hivyo kuathiri maisha ya wananchi kwa njia moja ama nyingine.

Mathalan Serikali hiyo ilianza na wafanyakazi hewa waliokuwa wakitafuna takriban Sh17 bilioni za walipakodi bila uhalali wowote kama mishahara yao huku ikirejesha nidhamu ya utendaji kazi serikalini iliyokuwa kwa kiasi fulani imeporomoka.

Baada ya hapo ilikuwa ikishughulikia  rasilimali za wananchi ambayo kwa miaka mingi wageni walikuwa wamegeuza kuwa sawa na haki yao wakijipangia namna ya kuyafaidi bila kuguswa.

Ingawa zipo changamoto mbalimbali za kiutendaji zilizojitokeza za hapa na pale, hatuna budi kuipongeza Serikali kwa kusimamia msimamo thabiti wa kuwahakikisha Watanzania wanafadika na madini yao.

Itakumbukwa kwamba wakati wa utawala wa Serikali ya Awamu ya Kwanza, chini ya Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere, iliwahi kujiweka kando na suala la madini mpaka hapo kizazi cha Watanzania wazalendo watakapokuja kuyachimba kwa manufaa ya wote na si wachache.

Tunafurahi juu ya Serikali kudhibiti utoroshaji wa madini kwenda nje ya nchi na uboreshaji wa sheria ya madini na majadiiano na wawekezaji katika msimamo iliouonyesha tangu ilipoanza  majadiliano na wawekezaji katika sekta hiyo ikitaka Taifa linufaike, lakini bado kuna rasilimali nyingine inazopaswa kuziangalia ikiwamo misitu.

Tofauti na Madini ambayo wngi wanalalamikia kutoktenda haki kwetu ni wageni hili la misitu ni sisi wenyewe. Misitu inaharibiwa kwa kasi na inatishia kutoweka iwapo hatua madhubuti hazitachukuliwa. Zipo taarifa kwamba kila mwaka ekari 372,000 zinaharibiwa.

Uharibifu huu wa misitu unatokana na uvunaji holela, uchomaji mkaa  na kilimo cha kuhamahama ambavyo katika maeneo mengi nchini vimeshamiri. Bahati mbaya ni kwamba kilio cha uharibifu wa misitu ni mamlaka chache zinazokiangalia kwa jicho la pili ili kukabiliana nacho na kuna kila dalili kwamba zinategeana  kuchukua hatua kuwabana wahusika.

Tukiondoa Jamhuri ya Kidemokraia ya Kongo (DRC), Tanzania ni miongoni mwa nchi chache kusini mwa Jangwa la Sahara zenye uoto mzuri wa asili unaolindwa kutokana kuwepo kwa misitu lakini hili linatishiwa na uharibifu unaofanyika.

Hivi ni kweli kwamba mamlaka zimeshindwa kukomesha kilimo cha kuhamahama? Wameshindwa kutokomeza uchomaji wa mkaa? Nani atamaliza kukomesha haya ikiwa wahusika wamekaa kimya?

Ziko taarifa kwamba mkaa na kuni kutoka Tanzania umekuwa ukisafirishwa kwenda nchi za Uarabuni na biashara hiyo imekuwepo kwa miaka mingi. Je, imeshindikana kukomeshwa? Au kuna wahusika mamlakani wanaofaidika na biashara hii? Hapana. Taifa hili ni letu. Tunataka mvua na maji ili tuishi kwani hatuna mahali pa kukimbilia iwapo tutakosa maji kwa ajili ya uhai wetu.

Kama alivyosema Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Gelastus Byakanma juzi,  inabidi kuangaliwa utaratibu mpya wa utoaji wa vibali vya uvunaji wa mazao ya misitu na wasiopanda miti kwanza kabla ya kukata ni vyema wasipewe vibali.

Ni lazima tubadilike sasa. Haiwezakani  mtu avune asichopanda. Hata Maandiko Matakatifu yanakataza kula asichokitafuta mtu. Hivyo, mtu asipewe kibali cha kuvuna mkaa endapo hatakuwa na shamba la miti.

Tahariri ya Mwananchi,

Mwananchi Communications Limited (MCL)

S.L.P. 19754 Dar es Salaam-Tanzania

SIMU +255222450875 au +255754780647