http://www.swahilihub.com/image/view/-/3887460/medRes/2050284/-/2m6w16/-/kesa.jpg

 

Serikali ijitahidi kuwapa walimu motisha

Kalamu

Baadhi ya wahitimu wa kidato cha sita wa Shule ya Sekondari Jangwani 

Na TAHARIRI YA MWANANCHI

Imepakiwa - Friday, February 9  2018 at  09:09

Kwa Mukhtasari

Hatimaye kilio cha muda mrefu cha walimu kutopandishwa vyeo kimesikika.

 

HATIMAYE kilio cha muda mrefu cha walimu kutopandishwa vyeo kimesikika.

Juzi, Naibu Waziri, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Joseph Kakunda alisema Serikali imeshamaliza mchakato wa mapitio ya upandishaji madaraja walimu uliokuwa umesimamishwa kwa muda mrefu.

Kakunda alitoa kauli hiyo bungeni mjini Dodoma alipokuwa akijibu swali la nyongeza la mbunge wa Viti Maalumu Susan Lyimo (Chadema), aliyetaka kujua hatima ya mchakato wa kupandisha walimu madaraja aliosema umekwama kwa siku nyingi.

Walimu pamoja na mambo mengine wamekuwa wakilalamika kuhusu kusitishwa upandishwaji wa madaraja jambo ambalo kwa wengi lilikuwa ikiwavunja moyo wa uwajibikaji.

Hii bila shaka ni habari njema kwa walimu ambao siyo tu kwamba watapumua kwa kupandishwa madaraja lakini pia Serikali imeeleza kuwa walimu hao watapandishwa madaraja kwa mserereko ili kusiwepo urukwaji wa madaraja kwa wahusika. Tunapongeza hatua hiyo ya Serikali kwa kuwa inaleta faraja kwa walimu ambao sasa tunaamini kuwa siyo tu watafarijika  lakini pia hatua hiyo ni motisha kwao ya kuwajibika zaidi.

Pamoja na usemi kuwa ualimu ni wito lakini kiukweli moyo wa uwajibikaji kwa walimu hukua zaidi pale mwajiri wao anapowathamini ikiwamo kuwapandisha madaraja.

Tafiti na uzoefu vimeonyesha kuwa walimu wakipewa motisha kwa namna mbalimbli, ari yao ya kufundisha huongezeka na hivyo kuleta matokeo chanya katika ufundishaji na ujifunzaji shuleni.

Mathalan repoti ya utafiti wa kujifunza iliyotolewa na Shirika la Twaweza mwishoni mwa mwaka 2017 ilionyesha kuwa asilimia 91 ya walimu waliohojiwa walikiri kuwa motisha kwao inachochea kiu ya kufundisha na mwishowe kufaulisha wanafunzi.

Tunaamini upandishaji wa madaraja ni mfano mmoja wa aina za motisha ambazo Serikali inapaswa kutoa kwa walimu tena mara kwa mara.

Serikali ikiwa mwajiri wa walimu haina budi kukumbuka kuwa kusitisha upandishaji wa madaraja, na kulimbikiza stahili zao ni vichocheo vya kukwaza jitihada za walimu ambao kimsingi hapa nchini bado wanafanyakzi katika mazingira magumu. Serikali inaweza kukwama kuwajengea walimu nyumba, ikashindwa kuwaendeleza kielimu lakini inapojihimu kuwapandisha madaraja na kuwalipa stahili zao kunawapa walimu ari ya kuwajibika.

Hatuna budi kukubali kuwa kiuhalisia katika shule nyingi, uwajibikaji wa walimu sio wa kuridhisha na ndio kwa kiwango kikubwa unachangia kuporomoka kwa kiwango ha kujifunza na mwishowe elimu yetu kwa jumla.

Tunaishauri Serikali kuwa hatua hii ya kupandisha madaraja iwe mwanzo wa kuzifanyia kazi kero mbalimbali zinazowasibu walimu nchi nzima.

Inatia moyo kwa mfano kuona Serikali ikilipa malimbikizo ya walimu ambapo hadi Juni 2017 Waziri Kakunda alisema Serikali ilishalipa 14,236 bilioni kati ya TSh69,461 bilioni ambazo walimu walikuwa wakiidai Serikali hadi kufikia mwaka 2015/16.

Hata hivyo, Serikali isiishie kulipa malimbikizo au kupandishwa madaraja pekee. Ni lazima iendelee kuwatazama walimu kwa jicho la karibu kama kada muhimu ya utumishi wa umma na mhimili wa maendeleo ya Taifa letu.

Tahariri ya Mwananchi,

Mwananchi Communications Limited (MCL)

S.L.P. 19754 Dar es Salaam-Tanzania

SIMU +255222450875 au +255754780647