http://www.swahilihub.com/image/view/-/3140968/medRes/1292425/-/bhpdjl/-/sindano.jpg

 

Serikali isivifumbie macho viwanda hivi

Sindano

Mtu akidungwa sindano. Picha/HISANI 

Na MHARIRI - MWANANCHI

Imepakiwa - Thursday, September 6  2018 at  08:42

Kwa Muhtasari

Kemikali aina ya Pseudo-Ephedrine ambayo ni kiambato muhimu katika kutengeneza baadhi ya dawa za binadamu, imekuwa ikichepushwa na baadhi ya viwanda kwa lengo la kutengeneza heroini na cocaine katika maabara za vichochoroni.

 

MAMLAKA ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya Tanzania (DCEA) imebaini kuwa baadhi ya viwanda vya kutengeneza dawa za binadamu nchini, huchepusha kemikali aina ya Pseudo-Ephedrine kwa lengo la kutengeneza dawa za kulevya.

Kemikali hiyo ambayo ni kiambato muhimu katika kutengeneza baadhi ya dawa za binadamu, imekuwa ikichepushwa na viwanda hivyo kwa lengo la kutengeneza heroini na cocaine katika maabara za vichochoroni.

Uovu huo unaohatarisha maisha ya Watanzania uliwekwa hadharani na Kamishna wa Ukaguzi na Sayansi Jinai wa DCEA, Bertha Mamuya kwamba baadhi ya viwanda vya dawa huiondoa au kuipunguza kemikali hiyo katika mchanganyiko wa dawa na matokeo yake, dawa inayotengenezwa inakuwa chini ya kiwango.

Tunaishukuru DCEA kwa kuwafumbua macho Watanzania na mamlaka husika namna afya zao zinavyochezewa na baadhi ya watengenezaji wa dawa nchini, wanaofifisha ubora kwa kuondoa au kupunguza viambato hivyo muhimu.

Afya ya Watanzania ni muhimu katika ujenzi wa Taifa ndio maana Serikali ikaamua huduma ya dawa isimamiwe kwa mujibu wa Sheria ya Chakula, Dawa na Vipodozi Na. 1 ya mwaka 2003 ambayo inaipa TFDA madaraka ya kusimamia shughuli zote zinazohusiana na ubora, usalama na ufanisi wa chakula, dawa, vipodozi na vifaa tiba hapa nchini.

Rai yetu kwa TFDA, kwa kuwa inayo mamlaka ya kisheria ya kusimamia ubora wa dawa nchini, ianze sasa kufuatilia kwa karibu watengenezaji wa dawa za binadamu kwenye viwanda nchini.

Aidha, hao ambao wamebainishwa na DCEA kuhusika katika hujuma hiyo wasionewe huruma wala kupewa msamaha kwa kuwa walichokifanya ni sawa na kutengeneza ‘silaha za maangamizi’ kwa afya za Watanzania.

Dawa zenye ubora hafifu zinaweza kusababisha athari za kiafya kama magonjwa kutotibika, usugu wa dawa na ngozi kuungua au kubabuka. Pia, kwa upande wa kiuchumi tatizo hili humuongezea mgonjwa gharama za matibabu zisizo za lazima.

Kuna wakati Serikali kupitia TFDA iliwahi kuwahakikishia wananchi kwamba dawa zilizopo sokoni zina ubora kwa asilimia 98 na itahakikisha zinaendelea kukidhi vigezo vya ubora.

Ubora wa dawa hizo ulipimwa kwenye maabara ya TFDA inayokidhi ithibati ya Shirika la Afya Duniani (WHO), sasa tunawaomba TFDA waendeleze kasi ya kupima ubora wa dawa kwa sababu kilichogunduliwa na DCEA hakipaswi kuachwa kikaendelea.

Tunafahamu kuwa sheria ni mfumo uliowekwa katika jamii na mamlaka kwa ajili ya kuwaongoza. Pia ni utaratibu unaotengeneza mfumo na mwelekeo wa maisha chini ya mamlaka husika, hivyo TFDA ina kila sababu ya kuitumia ipasavyo sheria iliyowezesha kuwapo kwake kwa kudhibiti na kukomesha tabia hii ya wenye viwanda vya kutengeneza dawa zinazoweza kusababisha athari kwa afya za Watanzania.

Kitendo cha kupunguza ubora wa dawa zinazotumika kutibu magonjwa ya binadamu hakivumiliki, wahusika hawapaswi kuachwa hivihivi na wala jamii ya Watanzania haitarajii kusikia kauli zilizozoeleka kwamba uchunguzi umeanza kufanyika.

DCEA ni mamlaka ya Serikali inayotambulika kisheria, hivyo tunaamini uhalifu uliofichuliwa na chombo hicho utakuwa mwendelezo kwa mamlaka zingine za dola kuchukua hatua za kisheria.

Kwa mantiki hiyo, tunategemea TFDA imeanza kuifanyia kazi suala hili kwa kuvifuatilia viwanda husika na kuchukua hatua stahiki.

Tahariri ya Mwananchi,

Mwananchi Communications Limited (MCL)

S.L.P. 19754 Dar es Salaam-Tanzania

SIMU +255222450875 au +255754780647