Serikali isiwafumbie macho wakunga, wauguzi hawa

Na TAHARIRI YA MWANANCHI

Imepakiwa - Wednesday, February 7  2018 at  08:27

Kwa Mukhtasari

Tumefarijika kusikia Serikali ikikiri kuwapo kwa watumishi ambao walikuwa na matatizo ya kuwanyanyasa wajawazito wanaokwenda kujifungua.

 

TUMEFARIJIKA kusikia Serikali ikikiri kuwapo kwa watumishi ambao walikuwa na matatizo ya kuwanyanyasa wajawazito wanaokwenda kujifungua.

Walalamikiwa wakubwa wa tatizo ambalo limekuwa kilio cha muda mrefu kwa wagonjwa hasa wajawazito ni wauguzi na wakunga wanawake.

Juzi Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt Faustin Ndugulile akijibu swali la nyongeza la mbunge wa Tabora Mjini (CCM) Emmanuel Mwakasuka alilieleza Bunge kwamba, “Ni kweli kuwa wapo watumishi wa kike ambao wamekuwa wakinyanyasa wanawake wanaokwenda kujifungua. Waziri wa Afya alishalitolea kauli suala hilo. Tunawafuatilia na tutashughulika nao.”

Mbunge huyo alitaka kujua kutoka kwa Serikali hatua ambazo inazichukua ikiwa inazo taarifa kuwa watumishi wanawake katika hospitali wamekuwa wakiwanyanyasa wanawake wenzao pindi wanapokwenda kujifungua.

Labda kwa kuwa swali hilo lilikuwa la nyongeza baada ya lile la msingi la mbunge wa Viti Maalumu (CCM) Hawa Mchafu aliyetaka kujua Serikali ilimaanisha nini kusema matibabu ni bure kwa wajawazito na waziri huyo alisema wajawazito ni moja ya makundi maalumu wanaostahili kupata huduma za matibabu kama ilivyo katika mwongozo wa uchangiaji wa mwaka 1997 uliopitiwa mwaka 2009/10 ambako imetamkwa kuwa huduma ya afya kwa wajawazito ni bure.

Tunasema labda ni kwa sababu lilikuwa ni swali la nyongeza kwa sababu kama Serikali inafahamu kuwapo kwa malalamiko haya ambayo si ya mwaka jana wala mwaka juzi ilipaswa kuja na majibu ya hatua kadhaa ambazo imekwisha chukua kukabiliana nalo.

Tulitarajia ikibainisha hatua ilizochukua katika kutoa elimu ya huduma kwa wateja kwa wakunga na wauguzi ili kuwajengea uwezo wa kuwajali wagonjwa wanaowahudumia lakini pia hatua za kinidhamu ilizowachukulia wale ambao wameonekana kuendelea na tabia hiyo hata baada ya kuelimishwa na kuonywa.

Tunaitaka Serikali kuandaa si majibu ya kina tu kuhusu tatizo hili bali kuja na mkakati wenye nuru ambao kila jicho litaona kwamba umedhamiria kumaliza kabisa kero hii kwa kinamama .

Tunasema hivyo kwa sababu kilio cha unyanyasaji wa wakunga na wauguzi sio cha jana wala juzi; kinatoka karibu kila pembe ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Hivi karibuni mathalan baadhi ya wadau wa afya mkoani Arusha walisema tatizo hilo ni kubwa maeneo ya pembezoni yaliwakumba zaidi wanawake wanaotoka katika jamii ya wafugaji.

Pia mwishoni mwa mwaka 2017 Naibu Waziri wa Afya wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) Said Suleiman akizungumza na wauguzi na wakunga wa jadi huko Mnazi Mmoja mjini Zanzibar aliwataka kuacha kutumia lugha chafu akisema zinachangia baadhi ya wananchi wakiwamo kinamama kupoteza imani ya kwenda hospitali kutibiwa na wengine kujifungulia nyumbani.

Hatukaki kuona wananchi wakipoteza imani ya kupata tiba ya kisayansi na badala yake wanakimbilia kwa wakunga wa jadi ambao aghalabu hawana vifaa vinavyoweza kuwahakikishia kinamama wanaojifungua usalama wao na watoto wanaozaliwa.

Hata hivyo, kupoteza huko kwa imani kunaweza kuwa sababu kwa wagonjwa kukimbilia kwa waganga wa kienyeji wengi wao wakiwa ni wapiga ramli chonganishi ambazo zimekuwa chanzo cha migogoro katika jamii.

Tunaitaka Serikali isiwavumilie watumishi hawa wachache kwani wanaweza kuwaambukiza wengine na kusababisha tatizo hili kuwa kubwa na kuleta madhara makubwa.

Tahariri ya Mwananchi,

Mwananchi Communications Limited (MCL)

S.L.P. 19754 Dar es Salaam-Tanzania

SIMU +255222450875 au +255754780647