Serikali iwasaidie wakulima kuisaidia Tanzania ya viwanda

Na MHARIRI - MWANANCHI

Imepakiwa - Tuesday, August 8   2017 at  10:11

Kwa Mukhtasari

Katika miaka ya hivi karibuni tumewasikia baadhi ya wanasisasa wakitoa maoni tofauti juu ya matumizi ya mbegu zinazozalishwa kwa kutumia teknolojia ya uhandisi jeni (GMO).

 

KATIKA miaka ya hivi karibuni tumewasikia baadhi ya wanasisasa wakitoa maoni tofauti juu ya matumizi ya mbegu zinazozalishwa kwa kutumia teknolojia ya uhandisi jeni (GMO).

Baadhi yao ambao sauti zao husikika zaidi kuliko hata watafiti wetu, wamekuwa wakisema kuwa mbegu za GMO ni nzuri kwa uzalishaji wa mkubwa kwa mazao ya chakula na biashara lakini wengine wanasema wamekuwa wakipinga, siyo uwezo wake bali athari kwa utafiti wa ndani.

Msimamo wa Serikali katika hili haukuwa wazi hadi hivi karibuni wakati wa uzinduzi wa maonyesho ya Sikukuu ya Wakulima Nane Nane, Waziri Profesa Jumanne Maghembe aliposema Tanzania itapiga hatua kubwa katika uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara iwapo wakulima na wadau wengine wa kilimo wataondokana na dhana potofu ya kukwepa matumizi ya mbegu zinazozalishwa kwa kutumia teknolojia ya GMO.

Akitumia kaulimbiu ya mwaka 2017, "Zalisha kwa tija mazao na bidhaa za kilimo, mifugo na uvuvi ili kufikia uchumi wa kati.”

Profesa Maghembe alisema sekta ya kilimo ndiyo itakayowezesha upatikanaji wa mahitaji ya malighafi kwa viwanda na matumizi ya mbegu bora zinazotokana na teknolojia ya GMO ndiyo pekee itakayowezesha kufikiwa malengo hayo na pamoja na kumwogezea mkulima tija.

Alitolea mfano wa kilimo cha zao la pamba kwamba kwa kutumia mbegu za kawaida uzalishaji wake ni mdogo na hauma tija kwa mkulima tofauti na mbegu za GMO ambazo zinaonyesha uwezo mkubwa wa uzalishaji

Wanaotoa angalizo kuhusu mbegu za GMO wanasema nchi zitakazoingia kwenye mtego wa GMO ikiwamo Tanzania zitakuwa tegemezi na hazitakuwa na mbegu zake tena zaidi ya kulazimika kuziagiza kutoka nje kwenye kampuni kubwa.

Kwa maoni ya teknolojia hiyo, itaweka mfumo wa kudhibiti uzalishaji wa chakula kwa mataifa maskini na kufanya bidhaa hiyo imilikiwe na mataifa machache.
Tunahisi kuwa angalizo hilo lina mashiko lakini ikiwa kwa kauli ya Profesa Maghembe Serikali tayari imefanya utafiti na kujiridhisha kuhusu teknolojia hiyo, basi kazi kubwa iwe kuwaelimisha wakulima manufaa ya teknolojia hiyo mpya kuelekea mapinduzi ya kilimo.

Mambo mengi mazuri huonekana au hufanyika wakati wa sherehe mijini tu na siyo vijijini. Wakulima ni zaidi ya asilimia 75 ya Watanzania na wanaishi vijijini ambako hawafikiwi na tafiti hizi kwa sababu ya uhaba wa maofisa ugani.

Kuendana na teknolojia

Maofisa hawa ni muhimu sana na wanapaswa kukaa karibu na wakulima ili kuwafundisha, kuwaelekeza na kubadili fikra zao katika uendeshaji wa kilimo ili kiendane na teknolojia mpya, mabadiliko ya tabia nchi na hali ya mvua.

Wakulima wanahitaji elimu hasa kwa zile mbegu za aina hiyo imeelezwa zinastahimili magonjwa ya aina mbalimbali, ikawamo na kuongeza uzalishaji wa mazao.

Kwa kuwa lengo la Serikali ni kuhakikisha wakulima wanaongeza uzalishaji wa mazao basi waanzishiwe pia masoko ili kuwawezesha wakulima kupata bei nzuri ya bidhaa badala ya kipindi cha mavuno kuwaachia walanguzi.

Tunatoa rai katika kipindi hiki ambacho Serikali inahimiza matumizi ya mbegu za GMO, basi wakulima wapelekewe pembejeo kwa wakati, maofisa ugani nao wajenge utaratibu wa kutoa elimu kwa wakulima

Maofisa ugani nao watafutie wakulima soko la mazao yao ili waweze kuchangia kujenga ujenzi wa Tanzania ya viwanda.