Serikali yashtushwa na pombe kuitwa 'Shetani, Demoni' Kirinyaga

Na MWANGI MUIRURI

Imepakiwa - Wednesday, January 30  2019 at  13:30

Kwa Muhtasari

(Santanna Ice ndiyo wanaita Shetani nayo Diamond ikiitwa Demoni)

 

KATIBU maalum katika Wizara ya Usalama na Masuala ya Ndani, Karanja Kibicho Jumatano ametoa amri msako kulenga pombe maarufu miongoni mwa wakazi kama Shetani na Demoni ziandamwe katika eneo la Mlima Kenya.

Amesema kuwa pombe hizo zinauzwa katika baa za eneo hilo na ambapo kando na kuwa na madhara kiafya kwa walevi wa eneo hilo, zinawageuza vijana kuwa mabwege.

"Ni pombe ambazo wanawake wanateta kuwa zinawafanya waume wao kulemewa na majukumu ya kuendeleza vizazi na pia kuwageuza kuwa vikojozi kitandani," akasema.

Akiandamana na Naibu Kamishna wa Ndia katika Kaunti ya Kirinyaga, Moses Ivuti katika uwanja wa Kiangwaci, katibu huyo alisema madhara ya pombe hizo ni sawa na majina yao.

"Unatarajia nini ndani ya mwili wako unapojitojeza katika baa na kuagiza kileo kwa jina Shetani na Demoni?" akahoji.

Mkutano huo wa kiusalama ulikuwa wa kuhamasisha wenyeji kushirikiana na maafisa wa kiusalama kuzima visa vya wizi wa mifugo katika eneo hilo la Kiangwaci.

"Katika kipindi cha miezi miwili sasa, ng'ombe 75, mbuzi 203 na punda 54 wameibwa na kupatikana wamechinjwa vichakani. Huo sio utamaduni wa Mlima Kenya," akateta.

Wanawake wa eneo hilo waliochangia mkutano huo waliteta kuwa wezi wamegeuza vijiji vya Kiangwaci kuwa himaya yao kwa kuwa inajulikana wanaume wao huwa hawajielewi kufuatia ulevi wa pombe hizo za demoni na Shetani.

"Mwanamume aliyerejea nyumbani jioni akitembea kwa magoti na Mara moja akaingia kwa kitanda akiwa hajaoga atazima wizi namna gani? Wakati wezi wanaiba mifugo ambayo sisi wake wao ndio wameyanunua, ndio wanaume hawa wetu wanang'orota wakikojoa vitandani. Tuko na shida," akalalama Bi Irene Wakuthii.

Aliongeza kuwa mifugo hao huibwa baada ya wezi kuwanunulia wanaume wao pombe hizo ambazo bei yazo huwa ni Sh100 kwa lita moja.

Bw Kibicho alitoa amri pombe zote za mauti eneo hilo ziwindanwe nazo, akionya maafisa wa kiusalama dhidi ya kuchukua hongo ili kuwakinga washirikishi wa biashara ya pombe hizo.

Alisema kuwa hatachelea kuwafuta kazi hadharani maafisa ambao watapatikana wakikosa uwajibikaji dhidi ya mabaa kukiuka masaa ya kisheria kuhudumu na pia ulanguzi wa mihadarati na wauzaji wa pombe za sumu vichakani.

Alisema kuwa licha ya vita vilivyozinduliwa  2015 na Rais Uhuru Kenyatta vya kupambana na upikaji, utengenezaji na uuzaji wa pombe za sumu, biashara hiyo imerejea kwa nguvu ikiratibiwa na matapeli, maafisa wa polisi na wafanyabiashara wafidhuli.

Biashara haramu

Kwa mujibu wa aliyekuwa kinara wa mamlaka ya kupambana na biashara ya ulevi na mihadarati (Nacada) Bw John Mututho, ni ukweli kuwa biashara hizo haramu zimerejea kwa fujo.

“Ulegevu uko katika utekelezaji sheria ambapo ufisadi umepewa kipau mbele na maafisa wengi. Wakati vita hivyo vilizinduliwa, kuna baadhi ya maafisa ambao hawakuonyesha kujitolea kwao kikazi na sasa ndio wameanza kurejesha wapikaji pombe hizo sokoni,” akasema.
 Anasema kuwa haswa upikaji wa chang’aa umeibuka kuwa sekta inayojivunia mamilioni ya pesa huku ikiwa kama mwajiri rasmi wa baadhi ya maafisa wa usalama.
“Ukweli ni kwamba, wengi wa maafisa hao wamejigeuza kuwa matajiri kupindukia kupitia kulinda wafanyabiashara wa vileo hivyo hatari katika kingo za mito ya hapa nchini na pia kunyapara mabaa yanayouza pombe hizo za sumu ili yasiathirike kupitia kuandamwa kisheria,” anasema Bw Mututho.

Bw Kibicho alisema kuwa waliofeli katika majukumu yao ni raia wa maeneo yanayoshuhudia kurejea kwa pombe hizo.

“Ni jukumu la raia kuzusha na kuandamana ikihitajika wakiwataka maafisa wa polisi katika eneo hilo wawajibike. Ikiwa wao wananyamaza tu; basi ni kumaanisha wanafurahia kufanyiwa biashara ya mauti,” akasema.

Bw Mututho analia kuwa baadhi ya pombe hizo zinapikiwa katika mazingara duni ya uchafu na ni hatari kwa afya ya umma.

“Ni suala la kusikitisha kuwa maafisa wa polisi wanaoelewa kuhusu biashara hiyo na hatari iliyoko ndani ya pombe hizo wanaenzi ufisadi kuliko kutunza afya ya raia nchini,” anasema.

Anasema kuwa baadhi ya pombe hizo hutengenezwa kwa misingi ya ushirikina na zingine huwa na kemikali hatari zinazoweza kuathiri wateja hao kwa kuwaambukiza watumizi ugonjwa wa saratani.

Bw Mututho alnafichua kuwa baadhi ya kemikali hizo ni aflatoxin ambayo hupenyezwa ndani ya pombe hizo kupitia utumizi wa nafaka iliyooza kama malighafi ya kuunda pombe hizo.

“Kemikali zingine ambazo tumekumbana nazo katika uchunguzi wa maabara ni zile za kuhifadhi maiti katika mochari, fatalaiza aina ya Ammonia na pia maji ya makonge,” anasema.

Anaongeza kuwa kemikali zile hatari zaidi ambazo zimekuwa zikijulikana na wakenya wengi ni aina ya Methanol ambayo ni kemikali inayotumika katika viwanda vya vyuma na pia hutumika kama mafuta ya ndege.
 Bw Mututho anasema kuwa kuna zaidi ya makampuni 1,000 ambayo hutengeneza pombe haramu hapa nchini huku baadhi ya maafisa wa usalama wakiwafungia macho chini ya shinikizo za kupongezwa hongo.
 Bw Mututho aidha analalamika kuwa wafanyabiashara wanaondeleza upishi wa pombe hizo hatari wako na ushawishi mkubwa wa kisiasa na pia rasilimali za kutosha kuandaa vita vya kisiasa na vya mahakamani dhidi ya yeyote anayejaribu kuwazima.