http://www.swahilihub.com/image/view/-/3887460/medRes/2050265/-/2m6vyf/-/kesa.jpg

 

Sharti tuwape moyo wanafunzi

Kalamu

Baadhi ya wahitimu wa kidato cha sita wa Shule ya Sekondari Jangwani 

Na TAHARIRI YA TAIFA LEO

Imepakiwa - Friday, December 22  2017 at  12:14

Kwa Mukhtasari

Wanafunzi waliopokea matokeo ya chini kwenye Mtihani wa Kitaifa wa Shule za Upili (KCSE) wiki hii wanafaa wapewe ushauri nasaha ili kulinda maisha yao ya sasa na ya baadaye.

 

WANAFUNZI waliopokea matokeo ya chini kwenye Mtihani wa Kitaifa wa Shule za Upili (KCSE) wiki hii wanafaa wapewe ushauri nasaha ili kulinda maisha yao ya sasa na ya baadaye.

Ni wazi kwamba maelfu kati yao hawakutarajia matokeo mabaya kama yalivyotangazwa na Waziri wa Elimu, Dkt Fred Matiang’i.

Wengi hawaelewi jinsi walipata matokeo mabaya ilhali kwa miaka yote waliyokuwa katika shule ya upili, na pengine hata kuanzia wakati walipokuwa katika shule za msingi walikuwa wakipata matokeo bora zaidi.

Kisa ambapo mwanafunzi wa kike alijitoa uhai katika Kaunti ya Migori baada ya kupata alama ya C- hakifai kupuuzwa.

Wakati huu kuna uwezekano mkubwa kwamba watoto wengi wanatatizika kiakili kwani hawaelewi jinsi walivyokosa kupata matokeo bora kwenye mitihani hiyo.

Itakuwa vyema kuweka mikakati inayofaa ili watoto hao washauriwe hasa na wazazi na walimu wao kabla tushuhudie visa vingine aina hiyo.

La muhimu zaidi, inahitajika ushauri uwe ukitolewa mara kwa mara shuleni hata kabla mitihani hiyo ifanywe ili wanafunzi waelewe kwamba kuanguka katika mtihani haimaanishi hakuna matumaini tena maishani.

Hii haimaanishi wanafunzi waruhusiwe kuwa wazembe katika masomo yao, bali wahimizwe kuelewa wana uwezo wa kufanikiwa maishani kwa njia zingine tofauti ambazo zinategemea talanta zao na wala si matokeo katika mitihani pekee.

Katika hali hii, inahitajika pia Wizara ya Elimu na wadau wengine katika sekta ya elimu watathmini upya jinsi matokeo ya mitihani ya mwisho hasa katika shule za msingi na upili yanavyoamuliwa.

Tumekuwa tukitegemea matokeo ya mtihani wa mwisho pekee kwa miaka mingi na ni wakati mwafaka wa kubadilisha hili.

Kwa msingi huu, juhudi za serikali kutaka kurekebisha mfumo wa elimu kwa awamu tofauti kuanzia mwaka ujao zinafaa kuungwa mkono na kila mmoja wetu.

Kama ni kweli kwamba matokeo bora ambayo tulikuwa tukishuhudia katika miaka iliyotangulia yalikuwa yanatokana na udanganyifu, hiyo inamaanisha mfumo wetu wa elimu una tatizo kubwa linalohitaji kurekebishwa.

Hivyo basi ni vyema kila mmoja wetu ajitolee kushirikiana ipasavyo na wadau wengine ili tuwe na mfumo wa elimu ambao utaashiria uwezo halisi wa watoto wetu bila kudhuru maisha yao ya sasa na baadaye.