http://www.swahilihub.com/image/view/-/4101938/medRes/1223807/-/7v2lbvz/-/BDLABOURDAY0105VV.jpg

 

Sokomoko la Sonko kugeuzwa vibonde naye akijibu mipigo

Mike Sonko

Gavana wa Nairobi Mike Sonko akihutubu awali. Picha/SALATON NJAU 

Na MWANGI MUIRURI

Imepakiwa - Friday, May 18  2018 at  09:20

Kwa Mukhtasari

Alhamisi yote ulishamiri mjadala motomoto wa kuamkia habari kuwa Gavana wa Nairobi, Mike Mbuvi Sonko, alikuwa amemteua Wakili Miguna Miguna kuwa Naibu gavana wake.

 

ALHAMISI yote ikiwa ni jana ilikuwa na mjadala motomoto wa kuamkia habari kuwa Gavana wa Nairobi, Mike Mbuvi Sonko, alikuwa amemteua Wakili Miguna Miguna kuwa Naibu gavana wake.

Kwa wakati huo wa uteuzi, Miguna Miguna alikuwa amekwama katika taifa la Canada ambako serikali ya Kenya ilikuwa imemtimulia kimabavu ikidai sio raia wa Kenya.

Miguna alikuwa amepania kurejea nchini kwa mara nyingine tena Jumatano lakini serikali ikasimama kidete kuwa haikuwa inatambua urejeo wake kwa kila njia au namna, na ingembidi tu kujisajili rasmi kama Mkenya.

Usijali kuwa kuna maagizo kadhaa ya mahakama ya kushinikiza serikali imkubalie Miguna kurejea nchini katika hali yoyote ile ili awasilishwe mahakamani kusikizwa kwa kesi kadhaa ambazo amewasilisha akidai anahujumiwa haki zake za msingi na pia nayo serikali ikiwa na kesi za kupinga.

Sonko akifahamu vyema, au akiwa hafahamu katika hali ambayo inaweza ikamwangazia kama juha mkuu wa kisiasa, akamteua Miguna kuwa naibu wake kujaza wadhifa huo ulioachwa wazi kupitia kujiuzulu kwa Polycarp Igathe.

Ingawa hakuna uhakika wa uhalali wa barua hiyo ya uteuzi iliyokuwa ikitandazwa mitandaoni na wengi wakiwemo wakili wa Miguna, Cliff Ombeta na Naibu wa Mkurugenzi wa mawasiliano katika serikali ya Kaunti ya Nairobi, Elkana Jacob, spika Beatrice Elachi akasema sahihi chini ya barua hiyo ni ile ya Sonko.

Sokomoko likazuka, huku Elachi akisisistiza kuwa uteuzi huo ulikuwa haramu kwa kuwa Miguna sio Mkenya, usijali kuwa  huyu asiye Mkenya alikuwa amewania ugavana wa Nairobi 2017 akiwa ameidhinishwa na taasisi zote husika za Jamuhuri ya Kenya kama Mkenya.

Swali kuu ni: Mbona Sonko akaamua kuchezea Wakenya mchezo wa hisia na ambao uliishia kuzua mjadala mkuu badala ya kuzua ule uwiano wa kimaoni kuwa amejaza wadhifa unaohitaji kujazwa?

Jibu ambalo linazuka kutoka kwa wadadisi wa masuala ya kisiasa ni kuwa Sonko anacheza siasa kali za kujiokoa baada ya kujipata akigeuzwa kuwa vibonde kutoka kila pembe ya siasa zake Jijini.

“Kuna maafikiano ya wapiga kura wengi kuwa Sonko alikuwa chaguo mbovu Nairobi. Kila yeyote aliyemuunga mkono ameanza kujiuliza kama kwa kweli alifanya maamuzi ya busara katika kumpa kura na kwa sasa ndoto ya sonko na mwenge wake wa kisiasa ni taabani ya maangamizi,” asema mhadhiri, Gasper Odhiambo.

Kutengwa

Anasema kuwa Sonko amekuwa akitengwa kila uchao na mrengo wake wa Jubilee kiasi kwamba ni wakati wowote kuwe na uwiano wa kimaoni kuwa ni aidha Sonko ang’atuliwe au serikali yake ivunjwe na Rais.

“Rais mwenyewe amezomea Sonko hadharani kuwa amelemewa na kusafisha Jiji la Nairobi. Waziri wa Mazingira, Keriako Tobiko, ameonekana wazi kumhujumu Sonko katika hafla ya Rais. Wapiga kura Nairobi wanalia kuwa kungezuka uchaguzi mdogo Nairobi, wa kwanza kutimuliwa atakuwa Sonko,” asema Odhiambo.

Anaongeza kuwa wawekezaji Jijini wanalia kuhusu barabara mbovu na ukosefu wa usalama, Sonko akituhumiwa kwa kugeuza Nairobi kuwa himaya ya magenge, kisa cha hivi majuzi kikiwa ni 'washirika wake wanane' (ingawa alipinga kuwa walifanya kwa niaba yake) kusakwa na polisi kufuatia shambulio dhidi ya mfanyabiashara Timothy Muriuki aliyekuwa akijiandaa kutoa taarifa ya kukashifu utendakazi wa Sonko.

Siasa hizo zikiendelea kuchezwa, Sonko akaamua kusaka usaidizi kutoka kwa mrengo wa upinzani ambapo alionekana akisalimiana na kinara wa Ford Kenya, Moses Wetang’ula na kusaka uungaji mkono katika serikali yake, ikiwa wazi kuwa ndani ya Jubilee hakuna kwa kujikinga ngarika ya siasa za kukataliwa.

Katika maombi kwa waathiriwa wa mkasa wa bwawa la Patel katika Kaunti ya Nakuru, Sonko akaonekana wazi akisusia salamu za Rais Uhuru Kenyatta, ishara kuwa sasa ni Sonko dhidi ya Jubilee, upinzani kukiwa kimya kwa kuwa kinara wao, Raila Odinga tayari anashirikiana na Kenyatta kiutawala.

Odhiambo anauliza: “Mambo yakifika hapo, Sonko amegeukia kulia kuwa anahujumiwa na Katibu maalum katika wizxara ya usalama wa ndani, Karanja Kibicho kwa nmiaba ya serikali. Ni kweli?”

Anaongeza la pili: “Sonko anasema kuwa Kibicho anatekeleza mradi pana wa washirika ambapo nia ni kuvuruga uwezekano wa Naibu wa rais William Ruto kupata usaidizi wa Sonko katika kutwaa urithi wa uirais 2022. Ni kweli?”

Mwishowe, anauliza swali ambalo anasema linaleta maswali hayo yote mawili pamoja: “Kuna mengine fiche ndani ya siasa ambazo zinaelekezwa Sonko?”

Odhiambo anasema kuwa Sonko ana ushawishi katika jumuia ya vijana hapa nchini na hatari kuu ni kuwa amekuwa akitangaza hapa na pale kuwa huenda awanie urais 2022.

“Je, kuna uwezekano kuwa kunaye amebabaika na angetaka kuzima ushawishi huo mapema kupitia kumwangamiza kisiasa Sonko?” auliza.

Odhiambo anasema kuwa huyu Sonko licha ya kuorodheshwa na shirika la TIFA kama aliye mbutu zaidi kiutendakazi kati ya magavana 47, ni yeye pia ambaye ameimarisha ukusanyaji ushuru Nairobi, akazima migomo ya jadi ya wafanyakazi wa Jiji na hospitali za Kaunti hii ziko na dawa.

Anasema kuwa huyu Sonko ndiye amekuwa akipambania Jubilee Ukambani na ushawishi wake umekuwa ukimfaa kwa kiwango muhimu ushindi wa rais Kenyatta katika chaguzi za 2013 na 2017.

“Hapo ndipo uteguzi wa kitendawili hiki cha masaibu ya Sonko kitateguliwa. Ni wazi kuwa kunao wameamua kuona tu mabaya ya Sonko licha ya kuwa ako na mazuri, na ambaye katika kupambana na majanga ya mafuriko Nairobi ananyimwa ile haki kuwa hata serikali kuu inafaa kuchangia. Kuna vita kamili vimeelekezwa Sonko nay eye anajibu mipigo hiyo,” asema.

Anasema kuwa bado ni mapema kujua vita hivi vitaishia wapi, lakini ni wazi kuwa jinsi na vile aliye na nia ya kumwangamiza mbwa huanza kwa kumharibia sifa mtaani, tuko katika awamu ya "kumharibia Sonko jina na sifa”.

Aliyekuwa Mbunge wa Starehe, Bw Maina Kamanda leo hii akiwa mbunge maalum anarejelea kauli yake kuwa alionya watu wa Nairobi wajitenge na Sonko katika kura ya mchujo lakini wakapuuza ushauri huo.

Kimafumbo, anasema kuwa sasa ndio mkoko unaalika maua, kuwa “ngojeni tu na mtakuja kuelewa maana ya kiini cha pingamizi zangu kwake”.

Hafichui anavyomaanisha hasa lakini kwa aliye na ufahamu wa kadiri kuhusu siasa, taswira ni kuwa unayoyaona katika ulingo wa siasa hizi dhidi ya Sonko sio nia kamili, bali kuna matokeo pana yanayolengwa kuafikiwa na hadi sasa, bado ni mapema kupata taswira kamili.

Wachanganuzi wanaonya Sonko kuwa njia ambayo amechukua ni hatari kwa siasa zake kwa kuwa amejiangazia kama anayemenyana na serikali yote akiwa kivyake, hali ambayo ameonyeshwa kuwa ni hatari kwa kuwa imejibu kwa kumpokonya walinzi.