http://www.swahilihub.com/image/view/-/3815398/medRes/1565500/-/buibhq/-/kissa.jpg

 

Kijana stadi wa kurekebisha vifaa vya kielektroniki

Gleen Washington Kisanya

Fundi chipukizi wa kukarabati vifaa vya kieletroniki, Gleen Washington Kisanya,10, mwanafunzi wa darasa la tano. Picha/PATRICK KILAVUKA 

Na PATRICK KILAVUKA

Imepakiwa - Thursday, February 16  2017 at  14:22

Kwa Mukhtasari

Hakuna mja aliyezaliwa akiwa na uwezo wa kujua kila kitu au kutenda ila kwa kujifunza au kuruzukiwa kitalanta na Mwenyezi Mungu!

 

HAKUNA mja aliyezaliwa akiwa na uwezo wa kujua kila kitu au kutenda ila kwa kujifunza au kuruzukiwa kitalanta na Mwenyezi Mungu!

Ndivyo anavyoamini fundi chipukizi wa kukarabati vifaa vya kieletroniki Gleen Washington Kisanya,10, mwanafunzi wa darasa la tano.

Yeye ni kifungua mimba wa familia ya Bw Alex Masha na Millicent Nerima.

Ukimwona ni mtoto wa kawaida mtaani; hutajua ana kipawa adimu.

Wakati mwingine ukimwona na vifaa vya kielekroniki hasa simu ama ilivyotupwa au kuharibika, saa, redio, kisengeretua (remote control) na kadhalika, unaweza ukadhani ni mzaha tu wa kitoto anafanya.

Sivyo unavyodhania; ukimwona akiviunganisha na kuvikarabati hapo ndipo utang'amua kwamba, usimtukane mkunga uzazi ungalipo!

Ana uwezo wa kukarabati au kuunganisha kifaa akitumia ujuzi wa kuzaliwa kwani hamna aliyemfunza kazi hii.

Yeye anasema ni maarifa ya ajabu ambayo amejaliwa na Jalali kuweza kukarabati vifaa.

"Nilianza kwa kukarabati redio ya nyanyangu ilipokuwa imeharibika," anasema Kisanya ambaye anafanya ukarabati huu kwa umakini.

Isitoshe, stima ikipotea kwao, yeye hakai gizani au kulalamika kampuni ya usambazaji stima kuwaweka gizani ila, anasema yeye huunganisha betri zake na taa kutoa mwangaza ili kuendelea kufurahia mwangaza awe mashambani au jijini. 

Mzazi ampa sapoti

Ingawa mzazi wake alikuwa na roho ya ati ati wakati alipokuwa anaanza kukarabati vifaa hivi, sasa anampa msukumo zaidi wa kuimarisha talanta yake kwani ametambua kwamba, bahati au nyota ya mja saa nyingine haijulikani kule itakapochipukia! 

"Babangu alikuwa akiliona kama sio jambo la kawaida ninalolifanya. Kwake ilikuwa kama nilikuwa ninajihatarishia maisha wakati ninapotumia vitu hivi. Kadri dira yangu ya kujua mengi kuhusu taaluma hii ilivyozidi kuimarika katika umri wangu huu bila kukata tamaa, ndivyo naye yeye alizidi kutafakari kuhusu msimamo wake na sasa ameniunga mkono kikamilifu katika juhudi zangu za kuendelea kuyajua mengi kuhusu fani hii," anaeleza Kisanya ambaye angependa kujinoa zaidi kwa kusomea taaluma ya masuala ufundi wa kielektroniki alivyo mjomba yake anayemtaja kwa jina moja tu Lumbasi.

Ingawa ana changamoto za kununua vifaa anavyovihitaji, hakati tamaa kwani anajua fika kwamba, siku njema yaja.

Ushauri wake kwa wazazi ni kwamba, wawashe moto vipawa vya watoto wao kama njia ya mbadala ya kujikimu maishani mwao kwani, yeye anajua kwamba kupalilia kipaji chake kutamwezesha kuvuna jasho lake usoni.