http://www.swahilihub.com/image/view/-/3033326/medRes/1228352/-/2sd5psz/-/DNCOASTIDPS1401C.jpg

 

Suala la IDPs latajwa kuathiri urithi Jubilee ifikapo 2022

IDPs waandamana Mombasa

Baadhi ya wakimbizi wa ndani kwa ndani (IDPs) washiriki maandamano barabara ya kuelekea Ikulu ya Mombasa wakitaka wakutane na Rais Uhuru Kenyatta Januari 14, 2016. Picha/KEVIN ODIT 

Na MWANGI MUIRURI

Imepakiwa - Friday, September 14  2018 at  13:54

Kwa Muhtasari

Suala la IDPs baada ya ghasia za uchaguzi wa 2007 limetajwa kama dondandugu ambalo litaathiri siasa za urithi 2022 ikiwa halitatafutiwa suluhisho la haraka.

 

SUALA la wakimbizi wa ndani kufuatia ghasia za uchaguzi wa 2007 limetajwa kama dondandugu ambalo litaathiri siasa za urithi 2022 ikiwa halitatafutiwa suluhisho la haraka.

Huku wengi wwa wahanga hao wakibakia katika hali ya kusikitisha baada ya kusambaratishwa kiuchumi na kijamii, wadadisi wa masuala ya kisiasa wameafikiana kuwa Rais Uhuru Kenyatta hana lingine ila tu kulitatua suala hilo kwa weledi na umakinifu wa kisiasa.

Tishio lingine ni kwamba, kwa sasa hakuna mtuhumiwa yeyote wa ghasia hizo ambaye amekabiliwa kisheria na adhabu ya kukomesha matukio kama hayo kuchipuka tena kuandaliwa dhidi ya washukiwa.

Kesi katika Mahakama ya Kitaifa kuhusu uhalifu dhidi ya binadamu (ICC) ilisambaratika na kukawa hakuna aliyepatikana kwa hatia ya kuzindua njama hiyo ya ghasia huku vitengo vya kiusalama ambavyo vilitarajiwa kuandaa mashataka dhidi ya wahusika wa ngazi za chini katika ghasia hizo vikikosa kuwajibika.

Kwa mujibu wa mchanganuzi wa masuala ya kijamii na kisiasa Bw Ngugi Njoroge, serikali imekuwa ikifanya mzaha na suala hilo, huku kejeli kubwa ikiwa ni kuunda wakimbizi wengine kufuatia kutimua maskota na kubomoa makazi na biashara za wengine.

"Kumekuwa na ripoti za serikali kuwa wakimbizi hao wamepewa mashamba na wengine kufidiwa kwa pesa taslimu. Lakini ukweli ni kwamba, wengi wao wamesahaulika na wanaendelea kuteseka pasipo sababu," akasema Bw Njoroge.

Alisema kuwa wakimbizi hao sio wale tu wa 2007, mbali wanajumuisha hata wale walioathirika katika ghasia za kikabila kupitia misukumo ya siasa kuanzia 1992.

"Wakimbizi wale tulio nao hapa nchini sio wale ambao wamekuwa wakitanjwa mara kwa mara na ripoti za serikali. Ukweli ni kwamba, tuko na zaidi ya wakimbizi 200, 000 wa miaka ya 1992, 1997, 2002 na 2007," akasema.

Alisema kuwa wengi wao wameachwa wakitafuta haki katika mahakama, akitaja kundi moja la wakimbizi wa Enosopukia katika mwaka wa 1992 kama waliochoka kungoja na kutatuliwa shida zao na serikali na wamewasilisha kesi mahakamani," akasema.

Kesi hizo zimeandaliwa katika msingi wa kikatiba ambapo  sheria nashinikiza serikali kuheshimu haki za kimsingi za binadamu ambapo ni lazima ihakikishe kila mtu ako na makao.

Mkurugenzi wa Shirika la Kenya Grassroots Network Organisation (Kengo) Bi Alice Njeri Mbatia alisema kuwa mwaka wa 2007 serikali ilitoa bajeti ya Sh177 Billioni ya kuwafidia waathiriwa wote wa ghasia za kisiasa na kikabila.

"Hata hivyo, kamati zilizoundwa kutekeleza bajeti hiyo zilitumia fursa hiyo kujitajirisha kwa njia haramu na ambapo mikakati mathubuti ya kuwapa makao na fidia hayakutimizwa," akasema.

Alisema kuwa kuchaguliwa kwa rais Kenyatta pamoja na William Ruto kama Naibu wake 2013 na 2017 kulikuwa na matumaini kuwa suala hilo lingetatuliwa mara moja.

"Ukweli mchungu ni kwamba, kuungana kwa Kenyatta na Ruto kulionekana kama dawa ya kudumu ya kuponya utengano ulioshamiri wa jamii zao mbili. Lakini jinsi usukani wao unazidi kuelekea uchaguzi mkuu wa mpwito wa 2022, ni wazi kuwa wao wawili ndio waliungana huku tofauti za jamii zao zikibakia vivyo hivyo," akasema.

Alisema ikiwa watalemewa kutatua shida hilo la wakimbizi, basi watajipata pabaya mwaka wa 2022 kwa kuwa wananchi watashindwa kuwaamini kuwa walikuwa na jibu la kusononeka kwao.

Nia ya kupaa

Bw Njoroge alisema kuwa kwa sasa wanasiasa wamejitambulisha kama walio na nia tu ya kupaa katika ndoto zao za utawala huku wananchi ambao hutumiwa kama vivukio wakiwachwa kuteseka.

"Hii ni serikali ambayo inaelewa kiini cha ghasia hizo na inaelewa tena kuwa kuna waathiriwa wanaongoja kusaidiwa. Ajabu ni kwamba, kuna watu katika utawala ambao wamebobea katika fani ya kuwadaa kuwa mambo yatakuwa shwari bila ya kutoa ratiba ya wakati subira yao itatimia," akasema.

Mbunge wa Bahati Bw Kimani Ngunjiri anasema kuwa jinamizi hilo liko katika eneo la Rift Valley na ndilo kioo tosha cha serikali ya Jubilee.

"Ni katika eneo hilo ambapo kuna jamii zilizoathirika vibaya katika misukosuko hiyo ya kisiasa. Jamii mbili kubwa katika eneo hilo ndizo zinaunda serikali tuliyo nayo. Ni muhimu kwamba wakimbizi wasaidiwe," akasema Bw Ngunjiri.

Aliyekuwa Waziri wa Mipango Maalum wakati bajeti hiyo ya Sh177 billioni ilipendekezwa kuwafaa wahanga hao Bi Esther Murugi anasema kuwa suala hilo lilivurugika baada ya mitandao ya utapeli kuliteka nyara.

"Kulitokea orodha bandia za wakimbizi ambapo wengi wao walilipwa kiharamu huku wale halisi wakiwachwa nje. Aidha, mikakati ya kuwashughulikia wahanga hao ilianza kutwaliwa na kamati kadha zote ambazo zilianza kung'ang'ania hela na kuishia kuwa mradi tata," akasema.

Alisema kuwa juhudi zake zote za kutatua shida hiyo ziliambulia patupu baada ya hujuma za matapeli na wafisadi waliodadia suala hilo.

"Nilipokabidhiwa wadhifa wangu wa kuwa kinara wa suala la wakimbizi hao, niliagizwa na Rais Mwai Kibaki kuwa nisuluhishe suala hilo kabla ya Desemba 2007 ambapo nilitarajiwa kuwapa wakimbizi wote mashamba, wajengewe nyumba na kisha tuwakabidhi vifaa vya kilimo ili waanze kujitafutia riziki," akasema.

Alisema mipangilio ya serikali ya kununua mashamba na pia kupata pesa za kuwajengea ilijikokota kufuatia sheria na utaratibu wa utekelezaji.

"Kwa mfano, tulitakiwa kuwasilisha michoro ya ramani ya nyumba ambazo tulinuia kujenga. Tulisema nyumba za matope hazihitaji ramani hizo kwani zinaweza kujengwa na wenyeji wa maeneo husika, lakini tukaambiwa hiyo ndiyo ilikuwa sheria," akasema.

Aidha, alilalamika kuwa kulichipuka wakimbizi bandia, ukora wa baadhi ya maafisa wa serikali na pia ukosefu wa mashamba mwafaka ambayo yalihitimu mahitaji ya serikali.

Aidha, alisema Wizara yake ilikumbwa na ukosefu wa maafisa wa kutosha kukabiliana na majanga.

"Wizara yote ilikuwa na maafisa 200 ambao hawangetosha katika maandalizi na utekelezaji. Ilitubidi kujihusisha na utawala wa mikoa na mashirika mengine yanayotoa huduma za kibinadamu," akasema.

Alisema wafadhili wa mradi huo walikuwa ni Benki ya African Development (ADB), Benki ya Dunia (WB) na pia serikali ya Kenya (GOK) ikisaidiana na Sekta ya Kibinafsi (Kepsa.)