http://www.swahilihub.com/image/view/-/4882278/medRes/2189575/-/urv5a5/-/sukumawiki.jpg

 

MAPISHI: Sukumawiki

Sukumawiki

Sukumawiki. Picha/SAMMY WAWERU 

Na SAMMY WAWERU

Imepakiwa - Wednesday, December 5  2018 at  11:41

Kwa Muhtasari

Sukumawiki ni aina ya mboga yenye matawi mapana na yanayokuwa kwa haraka.

 

MAPISHI: Sukumawiki

Sukumawiki ni aina ya mboga inayoliwa kwa kuandamanisha na vyakula mbalimbali kama; ugali, wali, chapati, matoke, au chakula kinginecho kulingana na mapenzi ya mlaji.

Walaji: Watu wawili.

Muda wa maandalizi ya viungo na kukatakata sukuma wiki ni dakika 20, mapishi yake dakika 10.

Vinavyohitajika

  • Vifungu sita vya sukumawiki
  • Nyanya tatu za wastani
  • Kitunguu kimoja
  • Mafuta
  • Chumvi

Namna ya kuandaa

Kagua kila kipande cha sukumawiki ili kuondoa wadudu wanaoweza kuwepo, kisha osha matawi hayo kikamilifu kabla ya kukatakata. Shughuli hii itachukua karibu dakika 15. 

Muda wa dakika tano unatosha kuchambua kitunguu na kukikatakata pamoja na nyanya, mchanginyiko huo uutie kwenye bakuli. Injika sufuria ama kikaangio mekoni, halafu umiminie mafuta kiasi, yashikapo moto weka mchanganyiko wa viungo; nyanya na vitunguu.

Hata hivyo, njia mbadala unaweza kutia viungo vile kikaangioni kisha umiminie mafuta. Geuzageuza viungo hivyo viive kwa kubondeka; dakika nne zinatosha.

Kamua sukuma wiki ulizoandaa kwa maji, uzitie kwenye kikaango kile, zigeuzegeuze hadi zichanganyike na viungo, mpishi asisahau kutia chumvi na awe makini asizidishe.

Muda wa dakika sita unatosha kustimu mboga hizi; ziepue. Ili kuongeza ladha ziandalie vipande kadha vya nyanya. Mboga tayari kuliwa kwa ugali.