http://www.swahilihub.com/image/view/-/4917194/medRes/2212626/-/11xi6gb/-/murithi.jpg

 

Mzee Kiguta asema tahadhari ni muhimu maishani

Juma Kiguta

Mzee Juma Kiguta, 78. Picha/MWANGI MUIRURI 

Na MWANGI MUIRURI

Imepakiwa - Tuesday, January 1  2019 at  12:38

Kwa Muhtasari

Ni muhimu kuzoea kuweka akiba.

 

MZEE Juma Kiguta, 78, ni afisa wa polisi mstaafu na ambaye ana mazoea kuanzia saa tatu asubuhi hadi saa 12 jioni anakuwa katika mji wa Maragua ulioko ndani ya Kaunti ya Murang’a.

Alikuwa akisoma katika darasa moja katika Shule ya Sekondari ya Dagoretti na aliyekuwa Mkurugenzi wa mpango wa Usalama wa Nyumba 10, Joseph Kaguthi na ambapo hata leo hii, huwa wanawasiliana wakijuliana hali.

Sio eti hupatikana mjini humo akishiriki lolote la uwekezaji au la ajira, bali huwa anapatikana katika mtaa huo akisaka raha yake kwa kuwa akisema, hawezi akatulia nyumbani kwa kuwa hawezi akashiriki kazi ngumu.

“Mimi sasa sina lingine ambalo linanipa tahadhari maishani. Mimi yangu ni kuamka, nioge, nijipe kiamsha kimya na kisha nitembee umbali wa kilomita tano hadi Mji wa Maragua kutoka boma langu lililoko katika kijiji cha Gakoigo,” anasema.

Anasema habari motomoto kumhusu kwa sasa hakuna, labda ziwe ni kuhusu kuondoka kwa walio hai kwenda zao kuzimu...

Anasema kuwa alipokuwa katika ajira, hakuna aliyempa ushauri wa kuchukulia maisha yake kwa uzito unaofaa na ajiweke chonjo kwa maisha ya baada ya maisha ya ajira.

“Mimi sikutoka katika ajira hiyo nikiwa na akiba yoyote au uwekezaji wowote. Nilistaafu miaka 23 iliyopita na nikapewa marupurupu yangu ya Sh400,000. Hizo ndizo pesa nilikuja nazo nyumbani zikiwa ndani ya akaunti yangu ya benki. Kila mwezi huwa napewa pensheni Sh7,000 na serikali na hiyo ndiyo pesa ambayo nimekuwa nikitumia kujikimu kimaisha,” anasema.

Ajabu ni kuwa, huyu mzee hajawahi kuoa lakini ana shamba la urithi kutoka kwa babake mzazi ambalo ni la ekari tano.

Malisho

Halilimi na huwa limegeuka malisho ya mifugo ya ndugu wake wengine watatu na hajali mpangilio huo.

Hata hivyo, anakusihi wewe ukiwa katika maisha ya ujana uchukulie maisha yako kwa uzito unaostahili.

“Usiige mfano wangu wa kimaisha. Ni vyema uanzishe familia yako na ukiwa na pato kwa sasa, wekeza ili maisha yako ya baadaye yasiiishie kuwa kama yangu,” anasema.

Anasema kuwa maisha yake kwa sasa ni yale tu ya kusukuma siku iende aamkie nyingine, akingojea tu mauti yakampe upumziko wa milele.

“Siwezi nikakutamania maisha kama hayo. Ingawa kwangu sasa ni raha kwa kuwa nimeyazoea, jihadhari sana usije ukaishia kama mimi. Sina wa kunirithi bali mali yangu itatwaliwa na ndugu zangu. Nishawaambia kuwa sina shida na wao kunirithi bali wasije wakaanza kupigania mali hiyo na ambayo ni shamba langu tu,” anasema. Na mbona asioe kwa kuwa waume husemwa hawazeeki hasa wakiwa na pato la kutegemewa hawawezi wakakosa wa kuwapenda hata wawe wenye sura sawa na kifaru cha kijeshi? Anakucheka akikuuliza kwa sasa ataanza kuzalisha namna gani na itakuwaje katika miaka hii yake aanze kujifahamisha na maisha ya kusumbuana na mwanamke akifahamika kama bibi yake?

Anasema kuwa angerudishiwa ujana wake leo hii, kabla ya kustaafu kutoka kazini, angekuwa amewekeza katika sekta ya hisa, mashamba na manyumba na  hatimaye akistaafu, arejee nyumbani kushiriki kilimo biashara akiwa anajibeba na gari lake na ambapo angefurahia kuona wajukuu wake akiwahadithia stori za enzi zake ujanani.

“Mimi nilirejea nyumbani nikiwa nimeabiri gari la umma. Afisa wa polisi mstaafu ambaye alikuwa katika kiwango  cha Inspekta akiwa hakuwa na uwezo hata wa kujinunulia baiskeli... Na sio eti sikuwa na uwezo huo, bali mtazamo wangu wa maisha ya baadaye ulikuwa na ubutu wa kiwango cha juu,” anasema.

Anakueleza kuwa shida yake kuu ilikuwa kujihisi kuwa bado alikuwa kijana hata wakati miaka yake ilitinga 40, akajipa tulizo kuwa bado kulikuwa na nafasi ya kukimbizana na maisha na ndipo alipofikisha miaka 50 na akajipata anaelekea kustaafu, akajipa moyo kuwa angetumia marupurupu yake kukimbizana nay ale ambayo hakuwa ameafikia.

Anasema kuwa alipostaafu, alijiuliza alikuwa awekeze katika safu gani, akitafutia nani urithi au malezi kwa nani, na alipogundua tu alikuwa peke yake katika maisha, akaamua pesa zake zilikuwa na uwezo wa kumgharamia maisha ya kila siku.

“Usiwahi ukatamani maisha haya yangu. Jijenge wakati una nguvu za kupambana kimaisha. Imajin ningekuwa sina pesa za mshahara wa mwisho wa mwezi na pia yale marupurupu yangu ya kustaafu… Ningekuwa ombaomba mitaani. Mimi niko sawa na usinihurumie, lakini wewe hautakuwa sawa ukifuata mkondo wangu wa kimaisha kwa kuwa unafaa kuwa na familia, ujijenge ukiijenga ukistaafu, uwe na maana ya kutulia ushuhudie matunda ya jasho lako la miaka mingi,” anasema.