http://www.swahilihub.com/image/view/-/4755602/medRes/2107219/-/wnv87sz/-/mkitikiti.jpg

 

Mkulima anayetambua thamani ya tikitimaji Pwani

Zachariah Onchuru

Picha ya mnamo Septemba 7, 2018, Bw Zachariah Onchuru almaarufu 'Ken Kilifi' mtaalamu na mkulima hodari wa tikitimaji Pwani, Kenya na Afrika Mashariki kwa jumla. Picha/ SAMMY WAWERU 

Na SAMMY WAWERU

Imepakiwa - Wednesday, September 12  2018 at  11:15

Kwa Muhtasari

Zachariah Onchuru ni mmoja wa wakulima wa matikitimaji Pwani ambaye amepata ufanisi mkubwa wa kuhakikisha anapata mavuno mazuri na kuwauzia wateja matunda yenye afya.

 

BW Zachariah Onchuru ni mmoja wa wakulima wa matikitimaji Pwani ambaye amepata ufanisi mkubwa katika juhudi zake.

Katika kijiji cha Chakama, eneobunge la Magarini kilomita 70 hivi kutoka mji wa Malindi kaunti ya Kilifi ndiko kijana huyu hufanya kilimo cha matunda hayo.

Kilimo chake ni cha kipekee na ambacho kimemvunia sifa chungu nzima si tu katika kaunti ya Kilifi, ila kote nchini na katika Ukanda wa Afrika Mashariki kwa sababu ya utaalamu na uhodari wake katika kukuza tikiti maji.

Onchuru almaarufu 'Ken Kilifi', alianza kulima tikitimaji mwaka 2013, na ni baada ya kupitia pandashuka zisizomithilika. Akiwa mwanambee katika familia ya watoto watano, Onchuru anasema maisha hayakuwa mteremko kama alivyotarajia. "Mimi ndiye kifungua mimba, na shida zilinilaki pindi tu nilipozaliwa. Mama alikuwa mkulima wa mahindi na nyanya, japo alizipanda kwenye shamba ndogo na zilizomsaidia kutukimu riziki na kunilipia karo pekee," anaeleza.

Barobaro huyu ambaye ni mcheshi na mkwasi wa ukarimu na kila aongeapo hakosi mambo yenye busara hasa kwa vijana ambao nusra wakate tamaa maishani, anasimulia kwamba alilelewa katika familia ya uchochole, kwa kuwa mama yake ndiye alikuwa mzazi wa kipekee (singo matha) na hakuwa na uwezo kifedha.

"Sitasema nilipitia maisha ya umaskini, kwa kuwa maskini ana uwezo wa kuwekelea tonge la mlo mezani. Uchochole ulihamia na kupiga kambi kwetu kiasi kuwa siku nyingi ni tulizolala njaa," afafanua.

Onchuru anakumbuka kana kwamba ilikuwa jana tu, kisa kimoja yeye na kaka zake, waliposingiziwa na majirani kuwa wao ni wezi wa mahindi. Anasema shuleni majina ya wenye deni la karo yalipotajwa, alikuwa wa kwanza kwenye orodha hiyo.

"Wanafunzi wenza wangeita jina langu hata kabla sijatajwa," adokeza.

Akiwa katika kidato cha pili 2005, mama yake alipata jeraha la mkono lililomlazimu kulazwa hospitalini kwa muda wa mwaka mmoja, ikawa pigo na sawa na kutia msumari moto kwenye kidonda kinachouguza. "Jeraha hilo lilinishurutisha kuwa mama na baba wa familia, na mama wa mama yangu," anasema.

Anasema alianza kupika mutura ili akimu familia yake, pamoja na kujilipia karo. Mungu si Athumani, licha ya muda wake kusoma kuathirika na kuongezeka, 2008 alikamilisha masomo ya upili ambapo alifanya mtihani wa kitaifa wa kidato cha nne, KCSE na kuzoa alama C+. Kwa kuwa yeye ndiye alikuwa tegemeo kwa familia, alianza uchuuzi wa tikitimaji Malindi. "Nilijisajili kusoma taaluma ya utangazaji na uandishi wa habari lakini sikukamilisha kwa sababu ya upungufu wa pesa," asema.

Mahitaji ya wateja wake kwa matunda hayo yalimshinikiza kuanza kilimo chake mwaka 2013. Kwa mtaji wa Sh20,000 alizoweka kama akiba, alikodi robo ekari aliyopanda tikitimaji. Hata hivyo, mwanzo wake ulimpiga dafrau kwa kuwa alipata hasara ya Sh15,000. Matunda hayo hukua kwa muda wa miezi mitatu pekee.

Alijipa breki ya miezi sita ili kusaka pesa zingine arejee kwenye kilimo hicho. Kwa kutumia Sh30,000 alikodi kipande cha shamba chenye ukubwa wa nusu ekari, na Onchuru anasema huo ukawa mwanzo wa ufanisi wake. "Mazao ya shamba hilo yalinipa faida ya Sh70,000 nikapata motisha kuendelea," afichua.

Mwenyezi Mungu alimfungulia milango ya heri na fanaka, ambapo kila msimu wa mavuno wateja walipiga foleni wakitaka tikitimaji zake shambani. Ni kutokana na juhudi zake ambapo alifanikiwa kununua shamba lenye ukubwa wa ekari 10 katika kijiji cha Chakama, Malindi.

La kutia moyo kwa mkulima huyo ni kwamba amegeuza taswira ya eneo hilo kuwa ya kijanikibichi ikizingatiwa kuwa Kilifi ni mojawapo ya kaunti zinazoathirika na baa la kiangazi nchini.

Jua lawaka

Swahili Hub ilifanya ziara kwa mkulima huyo, na miale ya jua kali inayocharaza ardhi Kilifi haijasitisha ari za Onchuru.

Miale ya jua la saa mbili asubuhi ni sawa na ile ya adhuhuri katika eneo hilo. Pwani inajulikana kukuza nazi na korosho, lakini katika shamba la kijana huyu, kinachokukaribisha ni rangi ya kijanikibichi ya tikitimaji. Pembezoni mwa shamba lake mita 700, amepakana na Mto Athi ambapo hutumia maji yake. Zaraa ya matunda hayo imemgeuza kuwa milionea, licha ya masaibu tele aliyopitia.

Hata hivyo, msimu wa mvua ya masika mwaka huu iliyonyea kati ya mwezi Machi-Juni, Onchuru anasema alikadiria hasara ya kima cha Sh3 milioni ambapo matunda yake na vifaa vya kilimo vilisombwa na maji ya mafuriko.

"Shabaha yangu si kuwa milionea. Langu ni kupasha ujumbe wa ukulima maalumu wa tikitimaji ili kupata mazao bora na si tu bora mazao. Pia lengo ni kubuni nafasi za ajira kwa vijana," anaeleza, akiongeza kuwa ana zaidi ya vijana 500 wanaomtegemea kikazi.

Anasema kwamba ameweza kubadilisha dhana ya zamani ya Pwani, kuwa ya kukuza matunda hayo. "Nimetembea karibu kila kona ya Kenya na nchi za Afrika Mashariki kutoa ushauri wa kilimo cha tikitimaji na wengi wamefanikiwa kuzipanda," adokeza.

Bw Onchuru hutumia mitandao ya kijamii kuimarisha maisha ya wenye ari kufanya kilimo cha tikitimaji.

Aidha, kwenye Facebook amefungua kurasa kama Ken Kilifi, The Watermelon Masters na anamiliki tovuti ya www.watermelonmasters.co.ke inayomuwezesha kutoa huduma zake ifaavyo pasi malipo. 

Mkulima huyo anasema ufanisi wake unatokana na juhudi za mama yake kumfariji na kumpa motisha kila alipokufa moyo, kiasi cha kutaka kujitia kitanzi. "Amekuwa nguzo kuu kwa ufanisi wangu, kwa kuwa wakati mmoja nilifikiria kujitia kitanzi lakini akasimama nami kidete," anaeleza.