Tuendeleze vita dhidi ya wasakaji wa albino

Na TAHARIRI YA MWANANCHI

Imepakiwa - Friday, October 6  2017 at  09:32

Kwa Mukhtasari

Wanafanya udhalimi, albino kuwaua,

Mauaji ya albino, acheni mbaya dhamira.

 

WANAFANYA udhalimi, albino kuwaua,

Tuufanye ukarimu ni binadamu sikia,

Haki zao tuheshimu, ni wazawa Tanzania,

Mauaji ya albino, acheni mbaya dhamira.

 

Hiki ni kipande cha ushairi uliotumwa katika gazeti la Mwananchi na Magdalena Mageresi mwaka 2015.

Hicho kilikuwa kipindi ambacho taarifa nyingi katika vyombo vya habari zilikuwa zikitamalaki kwa mauaji au kukatwa viungo kwa watu wenye ulemavu wa ngozi.

Ni hali iliyoifanya Tanzania kuingia katika orodha ya nchi zenye matukio ya aibu na ya kinyama duniani.

Wauaji wa albino wakatupa sifa ya uhayawani Watanzania wote.

Duniani kote Tanzania ikawa si mahali salama kuishi kwa watu wenye ulemavu wa ngozi.

Tunakiri zipo juhudi zilizofanyika na ndio  maana angalau miaka michache iiyopita taarifa za mauaji au watu wenye ulemavu wa viungo kukatwa viungo ilionekana kukoma.

Kukawa na kimya kirefu kuhusu taarifa za matukio haya ya kinyama.

Inasikitisha kuwa leo matukio hayo yameanza kurejea nchini. ‘Kumbe kimya kingi kina kishindo!'.

Kwa mara nyingine vyombo ya habari vimeripoti taarifa ya mkazi mmoja wa Morogoro, Nassoro Msingili (75) kukatwa mkono kisha walioukata wakaondoka nao.

Mkazi huyo mwenye ulemavu wa ngozi alipatwa na kadhia hiyo Oktoba 3, 2017 alipokuwa amelala nyumbani kwake katika Kijiji cha Nyarutanga.

Tukio hili lnatudhihirishia kuwa ‘wasakaji’la wenzetu wenye ulemavu wa ngozi bado wapo na harakati na harakati zao zinaendelea.

Hatua za kuwadhibiti zilizofanywa miaka iliyopita ama zimefeli au zimepungua nguvu. Ndiyo maana tunapaza sauti tukizisihi mamlaka husika kuamka na kulichukulia suala la mkazi huyu wa Morogoro  kwa uzito wa kipekee.

Ni uzito utakaorudisha imani ya wananchi kuwa vyombo vya usalama havijalala na wala havizembei kuwachukulia hatua wasakaji wa watu wenye ulemavu wa ngozi.

Kwetu sisi ufumbuzi wa kadhia hii wanayoipata wananchi wenzetu haipaswi kuishia kaika kusaka watuhumiwa hasa baada ya matukio na kuwachukulia hatua kali kwa mujibu wa sheria.

Hatuna budi kushughulikia sababu znazosukuma baadhi ya watu kuamua mauaji au kukata viuongo vya watu wenye ulemavu.

Kama uzoefu unavyoonyesha, wapo waganga wa tiba za asili wanaochochea vitendo hivi kwa kuagiza viungo vya watu wenye ulemavu kama sehemu ya tiba zao za kishirikina kwa fikra kwa viungo hivyo inasaidia watu kupata utajiri.

Vyombo ya dola vianze kuwashughulikia waganga hawa.

Kinga ni bora kuliko tiba.

Kama leo waganga wenye mitazamo ya kishirikina wanatumika kuagiza viungo vya watu wenye ulemavu wa ngozi na kesho watataka viungo vya watu wanene na wengineo.

Tusifke huko kama Taifa.

Tusimame kidete kupambana na kila aina ya kiashiria kinachochochea matukio ya kiyawahani katika jamii yetu.

Ukiondoa sheria kali dhidi ya watu wanabainika kuwadhuru watu wenye ulemavu ni muhimu kuwapo kwa utoaji wa elimu kwa umma kuhusu haki za binadamu.

Lazima Tanzania tuelewe kuwa kila mtu bila kujali hali yake ana haki yake ya kuishi na wala si utajiri au mafanikio ya kimasiaha hayatokani na mtu mmoja kumdhuru mwingine.

Tahariri ya Mwananchi,

Mwananchi Communications Limited (MCL)

S.L.P. 19754 Dar es Salaam-Tanzania

SIMU +255222450875 au 0754780647