Tanzania tujiondolee aibu hii ya watoto kula mwande

Na MHARIRI - MWANANCHI

Imepakiwa - Tuesday, May 15  2018 at  09:44

Kwa Muhtasari

  • Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,Wazee na Watoto imezindua ripoti ya utafiti ambapo katibu mkuu Sihaba Nkinga anasema kuna kila sababu ya kutafakari ongezeko la watoto wa mitaani
  • Asema watoto hao si wa Serikali, wala taasisi za kiraia, bali jamii kwa ujumla na kutaka wote kushirikiana katika kutafuta suluhisho

 

WIZARA ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,Wazee na Watoto imezindua ripoti ya utafiti unaoonyesha kuwa idadi ya watoto wanaoishia na kufanya kazi za mitaani imeongezeka.

Utafiti huo uliosimamiwa na shirika linalopambana na tatizo la watoto wa mitaani ulifanywa katika mikoa ya Dar es Salaam, Iringa, Mbeya, Mwanza na Arusha.

Ripoti hiyo imebaini kuwa idadi ya watoto wa mitaani nyakati za mchana ni 6,393 wakati nyakati za usiku ni 1,385.

Kama zilivyo ripoti nyingine zilizowahi kutolewa huko nyuma, sababu kubwa za ongezeko la watoto wa mitaani ni kuvunjika kwa ndoa, umaskini na ukatili wa majumbani unaofanywa ama na wazazi au ndugu wa watoto hao.

Wakati akizindua ripoti ya utafiti huo, katibu mkuu wa Wizara ya Afya, Sihaba Nkinga alisema kuna kila sababu ya kutafakari ongezeko hilo la watoto wa mitaani. Alisema watoto hao si wa Serikali, wala taasisi za kiraia, bali jamii kwa ujumla na kutaka wote kushirikiana katika kutafuta suluhisho.

Ilielezwa katika uzinduzi huo kuwa watoto hao hufanyishwa kazi mitaani na wengine wako katika mazingira hatarishi kutokana na kulazimishwa kufanya ngono na hivyo kuwa hatarini kupata magonjwa au ujauzito kabla ya umri muafaka.

Tatizo la watoto wa mitaani limekuwa kubwa katika miji mikubwa kama iliyofanyiwa utafiti na likiongezeka linakuwa hatari pia kwa usalama wa wananchi wengine kwa kuwa kadri wanavyoshindwa kupata mahitaji yao ya msingi, hulazimika kutumia mbinu za ziada kupata fedha, kama vile uporaji na wizi.

Pia, ili kukabiliana na hali ngumu ya maisha, watoto wa mitaani hujikuta kwenye matumizi ya dawa za kulevya na wale wasioweza kuzipata, huvuta petroli kwa ajili ya kuuburudisha mwili na kuufanya usihitaji chakula kwa muda mrefu.

Pia watu wasio wema huweza kuwatumia kirahisi katika vitendo viovu, kama ujambazi, wizi na biashara haramu kama ya dawa za kulevya au uuzaji miili.

Kwa hiyo, kunapokuwepo na taarifa kuwa kuna ongezeko la watoto wa mitaani, ni sawa na kuliambia Taifa kuwa kuna uwezekano mkubwa wa kuibuka majanga tofauti yanayoweza kusababishwa na ongezeko hilo.

Kama Nkinga alivyosema, suala hilo si la wazazi wa watoto hao, Serikali au taasisi zinazoshughulika nao, bali la jamii kwa ujumla kwa kuwa madhara yake si kwa Serikali, wazazi au taasisi hizo bali watu wote.

Jamii bado ina jukumu la kuhakikisha kuwa vitendo vya ukatili wa majumbani vinakomeshwa. Vitendo hivi vinafanyika machoni pa jamii. Wako wanaoona kuwa katika nyumba jirani kuna watoto wanafanyiwa ukatili, lakini hawaripoti sehemu husika au kushauri wanaofanya vitendo hivyo, waache.

Wapo wanaoona watoto wa jirani hawapelekwi kuandikishwa shuleni, hali wakijua kuwa hilo ni kosa na sasa elimu inatolewa bure, lakini hawaibui masuala hayo kwenye vikao vya vijiji, kata au hata kuwaripoti wanaofanya hivyo.

Suala la umaskini pia hutokana na baadhi ya watu kutojishughulisha na shughuli za uzalishaji na kutegemea misaada zaidi na hivyo wakijikuta wakiongeza umaskini unaosababisha watoto kukimbia makazi na kwenda kutafuta unafuu unaowatumbukiza katika maisha ya mitaani. Kwa hiyo, ripoti ya utafiti huo iwe angalizo kwa jamii nzima kutafakari maisha yetu kama yanalenga kusaidiana ili kuliepusha Taifa na matatizo kama hayo ya kijamii.

Tahariri ya Mwananchi,

Mwananchi Communications Limited (MCL)

S.L.P. 19754 Dar es Salaam-Tanzania

SIMU +255222450875 au +255754780647