http://www.swahilihub.com/image/view/-/3406064/medRes/1168738/-/3t9je1/-/MagufuliRais.jpg

 

Tumuunge mkono Rais ulinzi wa rasilimali za Taifa

Rais John Magufuli akitoa hotuba

Rais John Magufuli akihutubu awali. Picha/AFP 

Na MHARIRI – MWANANCHI

Imepakiwa - Friday, September 8  2017 at  11:40

Kwa Mukhtasari

Rais John Magufuli alipokea ripoti kuhusu madini ya almasi na tanzanite iliyoonyesha kuweko kwa dosari zinazosababisha nchi kupoteza mapato mengi.

 

ALHAMISI, Rais John Magufuli alipokea ripoti kuhusu madini ya almasi na tanzanite iliyoonyesha kuweko kwa dosari zinazosababisha nchi kupoteza mapato mengi.

Ripoti hiyo inatokana na kamati mbili zilizoundwa na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Tanzania Job Ndugai kuangalia mfumo wa uchimbaji, udhibiti, usimamizi na umiliki wa madini hayo.

Kama tulivyoripoti katika taarifa tuliyochapisha Alhamisi gazetini, hii ni ripoti inayoonesha hali ya kusikitisha kuhusu wizi unaofanywa nchini katika sekta ya madini na kibaya zaidi wizi huo ukiwa na baraka za Watanzania wenzetu waliopewa jukumu la kusimamia maliasili ya taifa.

Kilichoibuliwa na kamati za Bunge kinaandika historia mpya katika taifa letu kwa namna ufisadi ulivyokubuhu katika sekta ya madini.

Ingewezekana wajumbe wa kamati wangepindisha ukweli wa waliyobaini.

Haikuwa hivyo.

Wamedhihirisha ukweli mchungu ambao baadhi ya Watanzania wenzetu wasingependa uwekwe hadharani.

Tunawapongeza wanakamati kwa kuweka mbele maslahi ya Taifa.

Tunalazimika pia kumpongeza Rais kwa hatua ambazo amekuwa akizichukua katika siku  za hivi karibuni za kupambana na watu wanaohujumu sekta ya madini.

Kama ambavyo amekuwa akisema mara kwa mara nchi yetu iko katika vita vikali vya kupambana na mabaradhuli wa ndani na nje ya nchi ambao kwa muda mrefu waliigeuza nchi yetu kama mahali rahisi pa kuchuma.

Tukubali tumefanya makosa lakini kwa kupitia Serikali yetu ya Awamu ya Tano Watanzania katika kila ngazi tunapaswa kuamka na kuzillinda rasilimali  zetu ili zitunufaishe sisi na vizazi vijavyo.

Tusirudie makosa yaliyokwishafanywa na baadhi yetu waliokosa uzalendo  kwa nchi yao na hata kukosa huruma kwa wananchi ambao kama Rais alivyosema wamekuwa wakikosa huduma nyingi kwa sababu ya ukosefu wa fedha.   

Ili tusirud tulikotoka  tumewasikia viongozi wakiagiza kupitiwa upya kwa sheria zetu kama moja ya mikakati ya  kupambana na vita hii. Hata hivyo, tunapopitia upya sheria zetu na hata kuzibadili.

Mchakato huu uende sambamba na upitiaji upya wa mikataba yote katika sekta ya madini ili kubaini ile ambayo isiyokuwa na tija  kwa Taifa na hatimaye kutafutiwa njia sahiha ya kuachana nayo.

Kwa muda mrefu kilio cha Watanzania wengi ni usiri mkubwa wa mikataba hasa inayohusu maliasili muhimu kama madini.

Kama viongozi wakuu wa nchi wanakiri kuwa tumedhulumiwa na kuibiwa kwa muda mrefu.

Wakubali pamoja na mikakati mingine kuweka utaratibu wa mikataba ya Taifa kuwa mali ya umma na si mali ya watu binafsi wachache serikalini.

Kuanzia sasa tunapendekeza  mikataba yote ipelekwe bungeni na kuridhiwa na wawakilishi wa wananchi.

Kamati hzi za Bunge pamoja na zile za awali zilizoundwa na Rais kuhusu mchanga wa dhahabu ni  dalili tosha kuwa Serikali imeamua kwa dhati  kuikomboa nchi kutoka mikononi mwa watanzania walafi wanaoshirikiana na wageni kuifilisi nchi.

Tunaunga mkono juhudi za Serikali ambayo kwa hakika imeshajipambanua vya kutosha kwa dhamira yake ya kulinda mali za Taifa.

Wakati wa kuzuia wizi wa mali za nchi yetu ni sasa.

Wakati wa kuona maliasili zinanufaisha nchi hii ni sasa.

Tanzania ya uchumi wa kati inawezekana kama tutajipanga kuziba mianya yote inayotoa fursa kwa watu wachache kunufaisha kwa migongo ya Watanzania wengi.

Tahariri ya Mwananchi,

Mwananchi Communications Limited (MCL)

Tanzania.