http://www.swahilihub.com/image/view/-/4758762/medRes/2109276/-/r2nai8z/-/nene.jpg

 

Tunahitaji mfumo wa uratibu wa uingizaji na usafirishaji mazao

Mathew Mtigumwe

Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo nchini Tanzania, Dkt Mathew Mtigumwe. Picha/MWANANCHI 

Na MHARIRI - MWANANCHI

Imepakiwa - Friday, September 14  2018 at  09:12

Kwa Muhtasari

Taarifa kuwa nchi yetu sasa ina hazina ya kutosha ya mchele, inaleta matumaini.

 

TAARIFA kuwa nchi yetu sasa ina hazina ya kutosha ya mchele, inaleta matumaini.

Ni matumaini haya ambayo yameisukuma Serikali kutoa tamko la kusitishwa kwa uagizwaji wa bidhaa hiyo kutoka nje ya nchi.

Akizungumza juzi na wakulima wa mpunga kutoka mikoa mbalimbali mjini Moshi, Kilimanjaro, Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Dkt Mathew Mtigumwe alisema mahitaji ya mchele nchini ni tani 900,000, lakini sasa kuna tani za ziada zaidi ya 1.2 milioni.

Bila shaka kiasi hiki kikubwa mchele kilichopo sasa ni matunda yatokanayo na watu wengi zaidi kuhamasika kulima mpunga, lakini pia matumizi ya njia za kisasa katika uzalishaji.

Leo tunaposikia ushuhuda kutoka kwa mkulima kuwa ameweza kuzalisha mpunga kutoka magunia matatu kwa ekari hadi 56, lazima tukiri kuwa kuna jitihada za dhati zimefanyika na ndio maana leo tunaringa kuwa na hazina ya kutosha ya bidhaa hiyo.

Tukiwa sehemu ya wadau wa kilimo na maendeleo ya nchi kwa jumla, agizo hili la Dkt Mtigumwe ambalo kwa hakika linabeba mtazamo wa Serikali, linatufanya tufikiri kwa mapana.

Ikiwa leo imetoka kauli ya kuzuia uingizwaji wa mchele kutoka nje, hatujui lini kauli nyingine ya kuruhusu au kutilia mkazo kauli ya sasa itatoka na kama itatoka itawapa kicheko au kilio wadau wa mchele na mazao mengine kwa jumla?

Tunalazimika kufikiri hivi kwa kuwa kwa muda mrefu kumekosekana mfumo madhubuti unaoweza kuratibu uingizwaji au usafirishaji wa mazao ya kilimo.

Uzoefu wetu unaonyesha mara nyingi kauli zinazotolewa na viongozi wa juu serikalini ndizo zinazoamua kama bidhaa hizo ziingizwe nchini au zisafirishwe nje ya nchi. Ni kauli ambazo mara nyingi hupokewa kwa miguno kutoka kwa wafanyabiashara wa mazao, kwa kuwa wakati mwingine zinakinzana na hali halisi ya soko la mazao husika ndani na nje ya nchi.

Hatua tuliyofika ambapo Watanzania wengi sasa wanakichangamkia kilimo na hivyo kuhitaji masoko yenye tija kwao, matamko pekee tena baadhi ya nyakati yakiwa na msukumo wa kisiasa, hayatosaidia katika kuendeleza sekta ya kilimo na hatimaye kuwakomboa wakulima.

Tukiwa na mfumo unaoratibu hali ya uzalishaji na masoko, Watanzania hawatohitaji matamko. Ni mfumo ndio utakaoonyesha kama sasa nchi ina hazina ya kutosha ya mazao kama vile mahindi au mchele kama ilivyo sasa, hivyo kutohitaji uingizwaji wa bidhaa hizo kutoka nje.

Hata hivyo, pia ni mfumo huohuo utakaokuwa na utaratibu wa kuonyesha ni wakati gani wafanyabiashara wasafirishe mazao nje ya nchi.

Hatuwezi kujisifu kwa kuwa na hazina ya ziada ya mchele katika maghala yetu, lazima mamlaka husika ziweke utaratibu wa kuruhusu wafanyabiashara kusafirisha ziada hiyo katika masoko ya nje ambayo kwa wengi yamekuwa yakiwalipa.

Mathalan, tunataraji kuona kipindi hiki cha neema wafanyabiashara wakisafirisha mchele nje ya nchi kwa utaratibu ambao hautoweza kuathiri mahitaji ya ndani ya tani zile 900,000 alizosema Dkt Mtigumwa.

Hili hata hivyo, halipaswi kusubiri kiongozi mmoja asimame jukwaani na kutoa ruhusa bali ni mfumo pekee unaoweza kuratibu mambo haya.

Tahariri ya Mwananchi,

Mwananchi Communications Limited (MCL)

S.L.P. 19754 Dar es Salaam-Tanzania

SIMU +255222450875 au +255754780647