http://www.swahilihub.com/image/view/-/4744910/medRes/2100390/-/kjvknhz/-/gerewa.jpg

 

Tunahitaji mkakati kwa masomo yenye hisabati

Charles Msonde

Charles Msonde, Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani Tanzania. Picha/MAKTABA 

Na MHARIRI - MWANANCHI

Imepakiwa - Monday, January 28  2019 at  08:17

Kwa Muhtasari

Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Mitihani (Necta), Dkt Charles Msonde amesema ufaulu wa Hisabati kitaifa licha ya kuongezeka mwaka 2019 ikilinganishwa na mwaka 2018, bado somo hilo linaendelea kuwasumbua wanafunzi wengi.

 

Baraza la Mitihani la Taifa (Necta) lilitangaza matokeo ya mtihani wa kidato cha nne ambayo yalikuwa na viashiria tofauti vya maendeleo ya elimu na kushuka katika baadhi ya vipengele.

Tumeona jinsi shule binafsi zilivyoendelea kufanya vizuri katika matokeo hayo huku zile shule tulizoamua ziwe za vipaji maalumu zikishindwa kuonyesha umaalumu wao kwa jumla ingawa moja imetoa mwanafunzi aliyefanya vizuri kitaifa.

Hata hivyo, kitu ambacho kinaonekana kuwepo kwa tatizo sugu ni upande wa masomo yanayohusisha hisabati, ambako wanafunzi wameendelea kufanya vibaya na hakuna dalili za unafuu.

Akitangaza matokeo hayo mjini Dodoma mwishoni mwa wiki iliyopita, katibu mtendaji wa Necta, Dkt Charles Msonde alisema licha ya ufaulu kwa jumla kuongezeka kwa asilimia 1.29, masomo ya hisabati na yale yanayohusisha hesabu yameendelea kuwaweka watahiniwa katika hali ngumu.

Dkt Msonde alisema ufaulu wa hisabati kitaifa umeongezeka ikilinganishwa na mwaka jana, lakini akasema bado somo hilo linaendelea kuwasumbua wanafunzi wengi.

Alisema mwaka huu ufaulu ni asilimia 20 ambao ni ongezeko la chini ya asilimia moja ya ufaulu wa mwaka 2018 uliokuwa asilimia 19.19.

Alisema ufaulu huo mdogo pia unajumuisha masomo mengine yanayohusisha hesabu.

Dkt Msonde alisema juhudi za makusudi zinahitajika kwa ajili ya kuinua kiwango cha ufaulu wa masomo yote ikiwa ni pamoja na kuongeza idadi ya watahiniwa kwenye madaraja ya ufaulu ikiwemo masomo hayo.

Katika matokeo ya kidato cha nne 2017, Necta ilieleza kuwa ufaulu wa watahiniwa wa shule katika masomo ya uraia, historia, baiolojia, hesabu na biashara ulipanda kwa kati ya asilimia 1.07 na 9.85 ikilinganishwa na 2016.

Mwaka 2017 ufaulu wa juu kabisa ulikuwa wa somo la Kiswahili uliokuwa asilimia 84.42 na watahiniwa wote wa shule waliofanya somo hilo walifaulu huku ufaulu wa chini ukiwa ni wa somo la hesabu uliokuwa asilimia 19.19 ya watahiniwa wote wa shule.

Hii si ishara nzuri kwa taifa kwa ujumla. Umuhimu wa masomo yanayotumia hisabati si katika elimu tu, bali katika maisha kwa ujumla hasa wakati huu wa maendeleo ya kasi ya sayansi na teknolojia.

Ni dhahiri kuwa kwa sasa Taifa linaandaa wasomi wa baadaye ambao watakuja kuendeleza haya ambayo tunayafanya sasa na kuyafikishwa katika kiwango cha juu zaidi ili maisha ya Watanzania yawe bora zaidi.

Hata hivyo, ubora huu utategemea sana jinsi wanafunzi hawa wa leo watakavyopokea elimu wanayoipata, kuielewa na kuweza kuitumia wakati watakapokuwa tayari kushika nchi.

Serikali ya Awamu ya Tano inaendeleza sera yake ya uchumi wa viwanda ifikapo mwaka 2025. Yaani Taifa liwe linategemea uchumi wa viwanda ambao utalifanya Taifa liwe na uchumi wa kati na hivyo maisha ya Watanzania kuwa bora zaidi.

Hata hivyo uchumi wa viwanda hautategemea watu waliojifunza vyema historia, Kiswahili, uraia na jiografia pekee, bali - na tunaona ni muhimu zaidi—masomo mengine yanayotumia hesabu kama hisabati, fizikia na kemia.

Masomo hayo kwa pamoja ndiyo yanayoweza kuwandaa vizuri watoto wa leo kuwa tayari kuendeleza uchumi wa viwanda unaojengwa hivi sasa kwa kuwa utaweza kuwaandaa wasomi waliobobea katika masuala kama uhandisi wa nyanja zote, famasia, watawala, jiolojia, na mengine mengi.

Neta na wizara kwa ujumla hazina budi kuandaa mkakati mahususi kwa ajili ya kuboresha ufundishaji wa masomo hayo yenye ufaulu wa chini ili wataalamu wetu wa baadaye wawe ni wale walioelimika kikamilifu na si nusunusu.

Tahariri ya Mwananchi,

Mwananchi Communications Limited (MCL)

S.L.P. 19754 Dar es Salaam-Tanzania

SIMU +255222450875 au +255754780647