http://www.swahilihub.com/image/view/-/4108328/medRes/1131187/-/wt0dk8z/-/DNCOASTTB2509C%25282%2529.jpg

 

Tuungane dhidi ya magonjwa yanayoambukiza

Kampeni dhidi ya Kifua Kikuu

Millicent Mugo wa Wizara ya Afya aonyesha utaratibu wa kufanyiwa uchunguzi wa X-ray wakati wa uzinduzi wa utafiti wa ueneaji wa ugonjwa wa Kifua Kikuu (TB) 2015/2016 eneo la Mshomoroni, Mombasa Septemba 25, 2015. Nchini Tanzania kuna ufanisi mkubwa; kuna aina nyingi za panya ambao ni pamoja na Zucker wanaotumika kwenye maabara. Picha/KEVIN ODIT 

Na MHARIRI - MWANANCHI

Imepakiwa - Friday, June 29  2018 at  09:27

Kwa Mukhtasari

Magonjwa ya kuambukiza ni kama vile Ukimwi na Kifua Kikuu.

 

KWA mujibu wa takwimu mbalimbali za kitabibu duniani, magonjwa yasiyoambukiza yamekuwa yakichangia vifo vingi vya watu kutokana na jamii nyingi kutojua namna ya kujikinga au kukabiliana nayo.

Tafiti zinaonyesha watu wengi wanayapa kipaumbele kikubwa magonjwa yanayoambukiza, huku wakisahau kuwa yale yasiyoambukiza pia ni hatari kwa afya zao.

Moja ya mambo yanayochangia kuongezeka kwa magonjwa haya ni mabadiliko ya mitindo ya kimaisha inayohusisha matendo yanayoweza kusababisha ugonjwa.

Mitindo hii ni pamoja na kutofanya mazoezi au kushiriki michezo, ulaji usiofaa wa vyakula kama kula zaidi ya mahitaji ya mwili, kutokula vyakula jamii ya mbogamboga na matunda na kula nafaka zilizokobolewa.

Sababu nyingine zilizotajwa ni pamoja na matumizi ya pombe, uvutaji wa tumbaku, matumizi ya dawa za kulevya na msongo wa mawazo.

Tukikopa maneno ya Mkurugenzi wa Huduma za Kinga kutoka Wizara ya Afya, Dkt Leonard Subi, kuna vifo vingi nchini vinavyotokana na magonjwa yasiyoambukiza, hivyo mapambano yanahitaji ushiriki wa watu wote kwa kuwa ni vita ya kila Mtanzania.

Kwa nafasi yetu kama wadau muhimu wa maendeleo tumeamua kuendesha mjadala wa kitaifa kuhusu changamoto zinazotokana na magonjwa haya.

Mjadala huu chini ya kaulimbiu ya ‘Afya Yetu, Mtaji Wetu’ ni sehemu ya mpango ujulikanao kwa jina la Jukwaa la Fikra unaoratibiwa na Kampuni ya Mwananchi Communications Ltd kwa kushirikiana na wadau wengine. Sisi tumeanza, wito wetu kwa watu binafsi, mashirika, kampuni, asasi na vikundi ni kuelekeza nguvu katika kupambana na magonjwa haya ambayo siyo tu yamekuwa mzigo mkubwa kwa Serikali, lakini yanaathiri nguvu kazi katika Taifa letu.

Kwa ngazi ya mtu binafsi, ni wakati sasa kwa kila Mtanzania kujiepusha na magonjwa haya kwa kutekeleza mambo yanayoshauriwa na wataalamu wa afya.

Mambo hayo ni pamoja na kuzingatia kanuni za ulaji bora, kufanya mazoezi au kazi zinazotoa jasho angalau kwa muda wa nusu saa kwa siku, kuepukana na ulevi, kudhibiti msongo wa mawazo na kupima afya mara kwa mara hasa kuchunguza uzito wa mwili na dalili za magonjwa kama kisukari, shinikizo la damu ili yadhibitiwe mapema.

Kwa upande wa Serikali, pamoja na jitihada kubwa za kuendeleza sekta ya afya tunaisihi iendelee kuwekeza zaidi kwa kuongeza bajeti katika eneo hili, wataalamu na vifaa tiba pamoja na kuhakikisha huduma za afya zenye uhakika zinatolewa katika ngazi mbalimbali za mfumo wa afya nchini.

Ni wakati wa Serikali kuonyesha dhamira yake ya kusaidia mapambano dhidi ya magonjwa haya, kwa kuwa ipo minong’ono kutoka kwa baadhi ya wadau wa masuala ya afya kuwa jitihada kubwa za Serikali zimekuwa zikielekezwa kwenye magonjwa ya kuambukiza kama vile Ukimwi na Kifua Kikuu.

Tanzania mpya ya viwanda na yenye dhamira ya kuwa na uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025 inahitaji pamoja na mambo megine nguvu kazi ya watu wenye afya bora. Hatua yoyote ya kuyapa kisogo magonjwa yasiyoambukiza, kutafifisha dhamira na jitihada za kuiendeleza nchi yetu.

Tahariri ya Mwananchi,

Mwananchi Communications Limited (MCL)

S.L.P. 19754 Dar es Salaam-Tanzania

SIMU +255222450875 au +255754780647