http://www.swahilihub.com/image/view/-/4852928/medRes/2170947/-/12pj0nk/-/lukuvi.jpg

 

Uadilifu katika utumishi wa umma usipuuzwe

William Lukuvi

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi nchini Tanzania, William Lukuvi. Picha/MAKTABA 

Na MHARIRI – MWANANCHI

Imepakiwa - Monday, December 3  2018 at  07:43

Kwa Muhtasari

Serikali ya awamu ya tano Tanzania chini ya uongozi wa Rais John Pombe Magufuli imekuwa ikifanya kila linalowezekana kurejesha uadilifu na maadili miongoni mwa watumishi wa umma.

 

TANGU Serikali ya awamu ya tano iingie madarakani imekuwa ikifanya kila linalowezekana kurejesha uadilifu na maadili miongoni mwa watumishi wa umma.

Katika harakati hizo tumeshuhudia kila mara Rais anapowaapisha wateule wake wakila kiapo cha wazi na kujaza fomu za kiapo hicho hadharani kama ishara ya kuwataka watekeleze majukumu yao kadri sheria za nchi na jinsi maadili yanavyowataka.

Hii haikuishia tu kwa wateule wa Rais, pia imekuwa ikifanyika hivyo kwa watumishi wengine wa ngazi mbalimbali serikalini.

Kutokana na hatua hizo ni dhahiri kuwa kwa sehemu kubwa ya watumishi wa umma sasa wanatambua kuwa suala la uadilifu na maadili katika utumishi si la mzaha tena bali ni suala endelevu linalofuatiliwa kwa ukaribu.

Hata hivyo, pamoja na hatua hizo kuchukuliwa bado wapo watumishi vichwa ngumu ambao hawajatambua nia ya serikali na ndio maana bado tunashuhudia kuwapo kwa kesi zinazohusika na matumizi mabaya ya madaraka, wizi, rushwa na vitendo vingine vinavyokiuka viapo vya uaminifu walivyokula au sheria zinazowaelekeza namna ya kutenda kazi zao.

Mfano wa juzi wa jinsi Waziri wa Ardhi, William Lukuvi alivyofunga ofisi za ardhi na masjala za Jiji la Dar es Salaam akisema anafunga mtambo wa kufyatua migogoro ya ardhi, ndiyo namna iliyobaki inayostahili kwa wale watumishi wasiotaka kubadilika.

Lukuvi aliwataka maofisa wote wa Jiji wakusanye nyaraka za ofisi yao na kuhamia wizarani kwa kuwa hawana cha kufanya eneo hilo na kuwa ameshagundua chanzo chake kinatokea katika ofisi hiyo.

Kwa mujibu wa Lukuvi ofisi hizo ndizo zilikuwa zinatoa hati zisizotambulika kwa kisingizio cha ofa, na papo hapo akatangaza kuwa yeyote mwenye ofa ya kiwanja na ina muhuri wa jiji haitambuliki.

Huo ni mfano mmoja tu wa ofisi za jiji ambalo kimuundo hauna ardhi kwa kuwa iko chini ya manispaa tano. Hapo ndio tunajiuliza hali itakuwaje endapo kila manispaa na halmashauri za wilaya itafuatwa na kuhakiki faili baada ya jingine?

Kila mtu anaona jinsi miji yetu imejengwa holela na kila amejenga jinsi ajuavyo bila kuwekewa utaratibu. Mitaa haijapangwa, miundombinu muhimu haipo kwenye maeneo mengi. Haya yote yanahusishwa na ukosefu wa uadilifu katika utendaji wa watumishi wa umma.

Ukiacha suala la ardhi ambalo migogoro yake imeenea nchini kote, itakuwaje kuhusu ofisi zinazotoa hati na vibali vya aina mbalimbali, vipi kuhusu ofisi za watendaji mbalimbali, vituo vya polisi na maeneo mengine?

Karibu kila eneo ambalo viongozi husika wamejitokeza kufuatilia utendaji kwa karibu limeonekana linahitaji mabadiliko ya msingi.

Mfano, Mwigulu Nchemba akiwa waziri wa Mifugo na Uvuvi aliibua uozo katika machinjio pale alipoyatembelea nyakati wa usiku, Kangu Lugola hakosi kubaini madudu anapotembelea vituo vya polisi kwa ghafla na vivyo hivyo katika maeneo mengine.

Hatuoni sababu ya watumishi wa umma kusubiri kufanya kazi kwa kusukumwa kama inavyoonekana katika baadhi ya maeneo. Kila mmoja atakiwa kufanya kazi kwa hiari, kwa kufuata sheria, kanuni, taratibu na miongozo iliyopo ili kuhakikisha utumishi wa umma unaleta tija iliyokusudiwa.

Tahariri ya Mwananchi,

Mwananchi Communications Limited (MCL)

S.L.P. 19754 Dar es Salaam, Tanzania

SIMU +255222450875 au +255754780647