Uchaguzi wabunge wa Jumuiya ya Afrika Mashariki uwakumbushe wabunge wetu ‘Fahari ya Tanzania’

Na MHARIRI - MWANANCHI

Imepakiwa - Thursday, April 6  2017 at  14:32

Kwa Mukhtasari

Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzana juzi jioni walitumia muda mrefu kubishana kuhusu utaratibu wa kuwapigia kura au kuwapitisha bila kupingwa wagombea wawili wa Chadema katika Bunge la Afrika Mashariki (EALA).

 

WABUNGE wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzana juzi jioni walitumia muda mrefu kubishana kuhusu utaratibu wa kuwapigia kura au kuwapitisha bila kupingwa wagombea wawili wa Chadema katika Bunge la Afrika Mashariki (EALA).

Ulikuwa ubishi wa kanuni zinazoeleza utaratibu wa kuwapata wabunge wa Eala kulingana na makundi yao.

Ubishi huo ulitawaliwa zaidi na makundi mawili ya CCM na Chadema.

Tunaamini kubishana kwa hoja kunasaidia kuongeza uelewa wa kufikia mwafaka. Lakini tunathubutu kusema  ubishi katika Bunge la juzi lililofika hadi saa 7.05 usiku wa kuamkia Jumatano haukuwa na hoja za kujenga na kufikia mwafaka.

Tunadiriki kusema wabunge walitawaliwa na mihemko ya kisiasa badala ya kuweka mbele fahari ya Tanzania.

Wabunge wanaokwenda kuwakilisha Eala ni fahari ya Tanzania, hivyo wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wanapaswa kuitetea fahari hiyo kwa kuweka itikadi za kisiasa pembeni, kuacha kujenga umoja wa kukomoa chama fulani badala yake wajenge msingi wa pamoja wa kufanya Tanzania  iwe imara mbele ya mataifa mengine.

Ushahidi wa kukomoana uliotokea kwenye Bunge Maalumu la Katiba ambalo badala ya kushindana kwa hoja, waliingiza itikadi za kisiasa, mipashio na kupitisha mambo kwa ujanja ujanja hali ambayo imeligahrimu taifa kwa kutumia fedha nyingi za walipa kodi na katiba yenyewe haijapitishwa hadi sasa.

Pia ikumbukwe kuwa ndani ya Bunge hili, aliyewahi kuwa mbunge wa Eala Dk Harrison Mwakyembe  wakati wa uchaguzi wa wabunge hao aliwatahadharisha wenzao wapitishe wabunge wenye viwango vya kujenga hoja dhidi ya wabunge wa nchi nyingine wanachama hasa Kenya.

Hoja ya Mwakyembe ilitokana na uzoefu aliokuwa nao kwenye Bunge hilo kwamba wabunge wetu tunaowapeleka huko, wengine hawawezi kujenga hoja  za kuwashinda wabunge wa nchi nyingine kama Kenya na Uganda.

Ukiusikiliza wimbo wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kuna ubeti unaozungumzia uzalendo na mshikamano kwamba ndio msingi wa umoja wetu.

Kwa umoja wetu, uzalendo na mshikamano unapaswa kuanzia nyumbani kama Watannzania ndani ya Bunge letu hawatakuwa na uzalendo na mshikamano, safari ya kufikia malengo tuliyojiwekea itazidi kuwa ndefu kwa kuwa kila panapohitajika uzalendo na mshikamano sisi tunaingiza itikadi za kisiasa.

Tunaomba katika hili la Eala tulitafutie ufumbuzi  kwa masilahi ya taifa, hautakuwa na maana kama wanasiasa  wataamua kuendeleza malumbano huku wakiwachelewesha Watanzania kunufaika na matunda ya Jumuiya.

Tunadhani wabunge weu  wafike  mahali sasa wathamini fahari ya Tanzania, ule utamaduni wa yule ni mwenzetu au kukikomoa chama fulani kwa sababu kinahoji sana mambo ya watawala  hautasaidia  kulijenga taifa letu.

Bunge la Tanzania ni kati ya mihimili mitatu ya dola hivyo matarajio ya Watanzania wengi ni kuona mhimili huu ukifanya kazi  kwa haki na kufuata misingi ya sheria utakaosaidia maendeleo chanya ya taifa hili.

Hatuna nia ya kuwashambulia wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Hoja yetu ni kutetea fahari ya Tanzania.

Chochote  kinacholenga kulitangaza vizuri taifa hili ni fahari yetu sote.   

Tahariri ya Mwananchi,

Mwananchi Communications Limited (MCL)

Tanzania.