http://www.swahilihub.com/image/view/-/4678704/medRes/2055734/-/o5h1o5/-/idala.jpg

 

Uchunguzi ufanyike wanaofia mikononi mwa polisi

Pingu

Pingu. Picha/MAKTABA 

Na MHARIRI - MWANANCHI

Imepakiwa - Monday, October 1  2018 at  08:48

Kwa Muhtasari

Kila linapotokea tukio la mtu kufia mikononi mwa polisi zinaibuka kauli za pande mbili tunazoweza kuzieleza kuwa ni malumbano kuhusu sababu za kifo husika.

 

MATUKIO ya watu kufia mikononi mwa polisi yameendelea kujitokeza katika maeneo mbalimbali nchini licha ya juhudi za kila mara kuyakemea.

Kila linapotokea tukio la aina hiyo zinaibuka kauli za pande mbili tunazoweza kuzieleza kuwa ni malumbano kuhusu sababu za kifo husika.

Ndugu wa marehemu wamekuwa wakidai lao na polisi wakieleza sababu. Maiti kadhaa zimesuswa na ndugu kwa muda kusubiri hatima ya sababu za kifo. Hata pale ambako ndugu hao hulazimika kuendelea na mazishi, manung’uniko huendelea bila kuwapo majibu ya kumaliza tatizo husika.

Tukio la karibuni kabisa ni la juzi ambako familia moja mjini Moshi imekataa kuchukua maiti ya ndugu yao ambaye wanadai alifia mikononi mwa walinzi hao wa raia na mali zao.

Ingawa Jeshi la Polisi linadai mtuhumiwa huyo, Andrew Kiwia ambaye ni dereva alifariki katika jaribio la kujinyonga akiwa mahabusu ya kituo kikuu cha wilaya, familia hiyo haikubaliani nayo kwa madai kuwa maiti ina jeraha kichwani na kwamba kuna uwezekano lilitokana na kipigo cha polisi.

Polisi wanadai Kiwia alifanya jaribio la kujinyonga akiwa mahabusu na walipomchukua ili kumpeleka hospitali kuokoa maisha yake alifariki dunia njiani lakini ndugu wanasisitiza kuwa alifariki kutokana na kipigo.

Tukio hili si la kwanza kutokea nchini. Katika siku za karibuni mkoani Mbeya, ndugu wa marehemu Frank Kapange wamesusa kuchukua mwili wake zaidi ya siku 100 sasa wakiomba Mahakama itoe amri ya kufanyika uchunguzi wa kina kuhusu kifo chake wanachodai kilisababishwa na polisi.

Frank alifariki dunia Juni 4, 2018 na mwili wake umehifadhiwa katika Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya.

Pia lipo tukio la Machi 25 ambalo wakazi wa Kata ya Iyela, Mbeya walizusha tafrani kubwa wakifuatilia kifo cha Allen Mapunda (22), aliyedaiwa kufariki dunia saa chache baada ya kuachiwa kutoka kituo cha polisi alikokuwa akishikiliwa

Hayo yametokea baada ya lile la Aprili 27, mkoani Mara ambako Suguta Chacha (27) alifariki dunia akiwa mikononi mwa polisi na ilidaiwa alichomwa kwa kisu. Pia Julai 27, mkazi wa Kijiji cha Rubambagwe, wilayani Chato, Geita, Pascal Kanyembe (39) alifariki dunia akiwa mikononi mwa polisi baada ya kukamatwa. Pia, Agosti familia nyingine ya Dar es Salaam ilisusa kwa siku kadhaa kuchukua mwili wa ndugu yao, Salum Kindamba aliyeuawa huko Jet Lumo akidaiwa kupigwa risasi na polisi.

Ni bahati mbaya kwamba matukio hayo yanatolewa utetezi na polisi ambao wanatuhumiwa kuyasababisha. Wanakana na suala linaishia hapo. Ni malalamiko ya ndugu na utetezi wa polisi, hakuna mtu wa kati wa kueleza ukweli. Mtu wa tatu pekee anayezungumzia matukio hayo ni Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola ambaye amelieleza Bunge hivi karibuni kuwa suala la mtu kufa halichagui mahali anapotakiwa kufia kwa kuwa kifo ni mtego.

“Wengine wanaweza kufia kwenye magari, bungeni na wengine wanakufa wakifanya mapenzi. Je, huko nako kuna nini?” alihoji. Tunadhani majibu ya Waziri Lugola hayawezi kumaliza tatizo hilo. Tunadhani ni wakati sahihi kwa Serikali ama kuunda chombo kinachoweza kuwachunguza polisi pale wanapotuhumiwa au kuteua tume huru kuchunguza matukio hayo.

Ni kiu yetu kuona ukweli juu ya vifo hivyo unabainishwa ili kama kuna ukweli katika malalamiko ya ndugu za wanaofariki dunia mikononi mwa polisi, hatua za kisheria zichukuliwe bila kumwonea mtu au kumpendelea.

Ni matumaini yetu kuwa endapo tume itaundwa itakuja na mapendekezo yatakayosaidia kuepusha matukio hayo kwa siku za baadaye.

Tahariri ya Mwananchi,

Mwananchi Communications Limited (MCL)

S.L.P. 19754 Dar es Salaam-Tanzania

SIMU +255222450875 au +255754780647