http://www.swahilihub.com/image/view/-/4088422/medRes/1748045/-/p9towg/-/lissu.jpg

 

Uchunguzi wa shambulio la Lissu uharakishwe

Tundu Lissu

Mwanasiasa wa upinzani nchini Tanzania, Tundu Lissu akiongea katika mkutano wa mwaka wa chama cha wanasheria Tanganyika (TLS) Machi 17, 2017 jijini Arusha alipochaguliwa rais wa TLS. Picha/AFP 

Na MHARIRI – MWANANCHI

Imepakiwa - Friday, September 7  2018 at  10:59

Kwa Muhtasari

Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu alishambuliwa huko Dodoma.

 

LEO ni mwaka mmoja tangu mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu aliposhambuliwa huko Dodoma.

Lissu, alinusurika kifo baada ya watu wasiojulikana kumshambulia kwa risasi mchana akiwa ndani ya gari, nje ya nyumba yake katika eneo la Area D, Site 3 mjini Dodoma.

Mbunge huyo ambaye pia ni mwanasheria, alijeruhiwa sehemu mbalimbali za mwili kwa risasi zaidi ya 16 na tangu wakati huo amekuwa akipatiwa matibabu yaliyoanzia katika Hospitali ya Mkoa wa Dodoma, Hospitali ya Nairobi ya Kenya na sasa yupo nchini Ubelgiji.

Tangu wakati huo, vyombo vya dola vimekuwa katika uchunguzi wa tukio hilo na hivi karibuni, Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi alikaririwa akisema kwamba kazi hiyo bado inaendelea.

Profesa Kabudi akiwa Marekani akijibu swali kuhusu suala hilo, alisema uchunguzi wa masuala hayo ni mgumu na huhitaji muda mrefu zaidi kuukamilisha na kwamba hilo si kwa Tanzania pekee.

Mara baada ya tukio hilo, aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Jordan Rugimbana na Kamanda wa Polisi wa mkoa huo, Gilles Muroto waliitisha mkutano wa waandishi wa habari kuzungumzia tukio hilo. Muroto alisema mara baada ya kupata taarifa hizo walifika eneo la tukio na kuanza uchunguzi, “Tunaomba mwananchi wenye taarifa watusaidie. Jeshi la Polisi tumeanza uchunguzi, tumefika eneo la tukio na tunaendelea.” Alisema taarifa za awali zimeeleza kuwa kuna gari lililokuwa likimfuatilia Lissu ni aina ya Nissan la rangi nyeupe.

Imani yetu ni kwamba uchunguzi wa tukio hilo lililoshtua umma unaendelea. Pamoja na imani hiyo, tunavisihi vyombo vyote vinavyohusika kulichukulia suala hili kwa uzito mkubwa ili kuithibitishia dunia kwamba Tanzania inaweza kufanyia kazi matatizo haya na kuhakikisha kwamba hayajirudii.

Sambamba na msisitizo huo, tunavisihi pia vyombo hivyo vya dola kuharakisha uchunguzi wa tukio la kutoweka kwa mwandishi wa habari wa Mwananchi Communications Limited (MCL), Azory Gwanda ambaye mara ya mwisho alionekana huko Kibiti, Pwani Novemba 21, 2017.

Tangu wakati huo, wadau na wananchi mbalimbali wamepaza sauti kutaka wanaomshikilia wamwachie na kama kuna madai yoyote dhidi yake watumie mkondo wa sheria ambao upo imara na madhubuti hapa Tanzania. Pamoja na wito huo, Azory hajapatikana na hakuna taarifa zozote kuhusu mustakabali wake ambazo zimeshatolewa hadi sasa.

Kadhalika, tunavikumbusha vyombo hivyo pia kuharakisha uchunguzi wa tukio la kutoweka kwa Ben Saanane aliyekuwa msaidizi wa Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe.

Novemba 14, 2016 ndiyo iliyokuwa siku ya mwisho kwa Saanane aliyekuwa akimsaidia Mbowe katika utafiti na uchambuzi wa masuala ya siasa na uchumi kuonekana katika ofisi za Chadema Mtaa wa Ufipa, Kinondoni naye hadi leo, mustakabali wa mahali alipo haujulikani.

Tunatamani kuwasikia viongozi wenye dhamana, wakijitokeza na kuzungumzia maendeleo ya uchunguzi wa matukio yanayochunguzwa bila kuathiri mwenendo wa uchunguzi tukiamini kwamba kwa kufanya hivyo, ndugu, jamaa na watu wa karibu wa watapata faraja.

Tahariri ya Mwananchi,

Mwananchi Communications Limited (MCL)

S.L.P. 19754 Dar es Salaam-Tanzania

SIMU +255222450875 au +255754780647