Udhalilishaji uliofanywa na mwalimu huyu usivumilike

Na TAHARIRI YA MWANANCHI

Imepakiwa - Thursday, November 9  2017 at  09:48

Kwa Muhtasari

Katika toleo la Mwananchi la Jumatano tuliripoti kisa cha mwalimu mkuu wa shule moja ya msingi wilayani Biharamulo, Mkoa wa Kagera aliyeamua kwa kumcharaza viboko mwalimu mwenzake kama njia ya kumrudi.

 

KATIKA toleo la Mwananchi la Jumatano tuliripoti kisa cha mwalimu mkuu wa shule moja ya msingi wilayani Biharamulo, Mkoa wa Kagera aliyeamua kwa kumcharaza viboko mwalimu mwenzake kama njia ya kumrudi.

Kisa hicho kilitokea shule ya msingi Migango ambapo mwalimu mkuu aliamua kumchapa viboko mwalimu mwenzake mbele ya wanafunzi akimtuhumu kwa wizi wa sahani tano pamoja na nusu kilo ya sukari  iliyotolewa kwa ajili ya mahafali ya wahitimu wa darasa la saba.

Taarifa iliyokifikia Chama cha Walimu Tanzania (CWT) Biharamulo zimeeleza kwamba badala ya kufikishwa kwenye vyombo vya sheria, mwalimu mkuu huyo alifuata njia ya kumaliza kesi hiyo kienyeji, hivyo akajipa mamlaka hayo kwa kumfunga kamba chini ya mti ili asifurukute na kisha akamchapa viboko saba.

Tumesikitishwa namna maadili ya uongozi yanavyoporomoka kwa kasi kiasi kwamba watu ambao hawana mamlaka kisheria wanawaadhibu wakosaji au watovu wa nidhamu au wakiukaji wa taratibu za kujichukulia sheria mkononi.

Tumeshuhudia miaka ya hivi karibuni wakuu wa mikoa na wilaya akishindana ama kuwasimamisha kazi watumishi wa halmashauri au kuwaweka ndani viongozi mbalimbali wa Serikali  na vyama vya siasa.

Waziri Mkuu aliwahi kukemea tabia hiyo bila mafanikio. Pia Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma iliwahi kutoa orodha ya watu wenye mamlaka ya adhabu ukiwa ni mwongozo kwamba wale ambao hawakutajwa wasithubutu, lakini juhudi zao hazijazaa matunda.

Sasa tabia hii ya kujichukulia sheria mkononi imeshuka hadi kufikia mwalimu mkuu wa shule ya msingi kujiona ana uhalali wa kuwaadhibu walimu wenzake.

Hii ina maana kwamba mwalimu mkuu huyu hajui mamlaka yake na hajui kumcharaza viboko mwalimu mwenzake mbele ya wanafunzi ni kitendo cha udhalilishaji na ni kinyume cha haki za binadamu.

Hii ina maana kwamba mwalimu mkuu huyu hajui mwizi akikamatwa anapelekwa wapi. Ni kweli mwanafunzi mdokozi huadhibiwa shuleni lakini mwenye mamlaka ya mwisho hata kwa mwanafunzi mwizi, mgomvi, anayejihusisha na mapenzi na makosa mengine makubwa ni bodi ya shule.

Tunajiuliza kwa nini mwalimu mkuu huyu wa shuke ya msingi alijipa mamlaka ya Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC)?

Itakumbukwa kwamba Februari mwaka 2009  aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Bukoba katika Mkoa wa Kagera alifanya kosa kama hili alipomwamuru polisi  mmoja kuwachapa viboko walimu wa shule tatu za msingi  kutokana na wilaya hiyo kuwa ya mwisho katika matokeo ya darasa la saba.

Waliocharazwa viboko ni walimu tisa wa shule ya Msingi ya Katerero, 11 kwa shule ya Kanazi na 12 kutoka Kasenene.

Mkuu huyo wa Wilaya alidhani kwamba uamuzi ule ungesaidia kuwakumbusha walimu wajibu wao ili waache kuchelewa, wafundishe kama inavyopasa ili Wilaya ya Bukoba isiwe ya mwisho kimkoa katika matokeo ya darasa la saba.

Hata hivyo alisahau kuwa hakuwa na mamlaka ya kuwaadhibu walimu hata kama angekuwa nayo.

Adhabu ile haikustahili na ulikuwa ni udhalilishaji mkubwa. Baadaye uteuzi wake ulitenguliwa na mamlaka iliyomteua.

Tunashauri mwajiri wa mwalimu huyu na wengine wa aina yake kuwakumbusha mwisho wa mipaka yao ili kuondoa migongano, usumbufu na udhalilishaji.