http://www.swahilihub.com/image/view/-/4550338/medRes/2123127/-/xtot4t/-/endokasi.jpg

 

Ukaguzi wa mabasi vituoni usiwe kero

Basi la mwendokasi

Basi la mwendokasi. Picha/HISANI 

Na MHARIRI – MWANANCHI

Imepakiwa - Tuesday, September 11  2018 at  08:14

Kwa Muhtasari

Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano nchini Tanzania, Atashasta Nditiye alitangaza katika kipindi cha wiki mbili zijazo ratiba ya usafiri wa abiria waendao masafa marefu itabadilika kuruhusu mabasi kuanza safari saa 11:00 alfajiri badala ya saa 12:00 asubuhi kama ilivyo sasa.

 

KATIKA kipindi cha wiki mbili zijazo ratiba ya usafiri wa abiria waendao masafa marefu itabadilika kuruhusu mabasi kuanza safari saa 11:00 alfajiri badala ya saa 12:00 asubuhi kama ilivyo sasa.

Mabadiliko hayo yalitangazwa wiki hii na Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Atashasta Nditiye alipozungumza na wadau wa sekta ya usafirishaji wa abiria kwamba mabasi yaendayo mikoani kutoka Dar es Salaam na yatokayo mikoani mfano Mwanza, Mbeya na Dodoma na Arusha kwenda Dar es Salaam yatahusika na mabadiliko hayo.

Wadau mbalimbali wa usafirishaji abiria wakiwamo wa Chama cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania (Taboa), wamefurahishwa na mabadiliko hayo ya ratiba wakisema itawawezesha kukabiliana na changamoto mbalimbali kuanzia wanapoondoka hadi wanapofika vituo vya mwisho.

Kwa kuwa hicho kilikuwa kilio cha muda mrefu cha wadau wa sekta hiyo na kwa kuwa hata baadhi ya wafanyabiashara wamekuwa wakihitaji mabadiliko ya ratiba yatakayowapa unafuu kuwahisha bidhaa zao tunaamini matakwa yao pamoja na changamoto mbalimbali kwa abiria zitakuwa zimezingatiwa.

Hata hivyo, tunapenda kukumbusha kwamba hapo zamani mabasi yaendayo mbali, mfano yatokayo Dar es Salaam kwenda mikoani na mikoani kwenda Dar es Salaam au kutoka mkoa mmoja kwenda mingine ya mbali yalikuwa yakianza safari kati ya saa 10:00 alasiri na saa 12:00 jioni. Mabasi yalikuwa yakisafiri usiku kucha.

Mwaka 1990, kutokana na kushuhudiwa ajali nyingi za usiku, majambazi kuteka mabasi kisha kupora fedha na mali za abiria, Serikali iliamua kubadili ratiba na kuyataka mabasi kusafirisha abiria kuanzia saa 12:00 asubuhi hadi saa 4:00 usiku.

Mabadiliko mengine muhimu ni yaliyolazimisha mabasi yaendayo mbali kuwa na maderava wawili ili mmoja akichoka mwingine akae kwenye usukani lengo likiwa kuwapa abiria uhakika wa safari. Hata Serikali ilipoagiza kila basi kuwa na kidhibiti mwendo lengo lake lilikuwa kunusuru maisha ya wasafiri.

Tunafahamu pia kwa miongo miwili iliyopita Serikali imefanyia kazi changamoto nyingi mfano imeboresha miundombinu ya usafiri ambapo sasa barabara nyingi ni za lami, imeweka ukomo wa mwendokasi kuwa kilomita 80 kwa saa, imeweka askari wengi wa usalama barabarani kufuatilia madereva wasiotii sheria lakini bado zipo nyingine ikiwemo ya ukaguzi wa mabasi kwenye vituo ili kuhakikisha yanayosafiri ni yale yenye idhini.

Katika hili tunashauri askari wa ukaguzi wahakikishe wanayakagua mabasi yanapofika au saa kadhaa kabla ya kuondoka ili kuondoa usumbufu kwa abiria asubuhi. Maana kama mabasi yamelala kituoni, kwa nini askari wanasubiri kukagua yanapotoka kwenye lango kuu tena kwa kugombania asubuhi?

Ukaguzi wa asubuhi ndio umekuwa ukisababisha magari mengine kukawia kuruhusiwa au kuzuiwa kusafiri dakika za mwisho wakati abiria hawawezi kupata basi mbadala.

Laiti ukaguzi huo ungekuwa unafanyika mapema abiria wa basi linalozuiwa kusafiri wangeweza kukata tiketi katika mabasi mengine.

Tunafahamu hatua ya kuzuia kusafiri basi lenye makosa ni kwa usalama wa abiria, lakini inakera abiria kulazimika kuahirisha safari kwa sababu ya ukaguzi uliocheleweshwa.

Pia tunashauri mabasi yanayokuwa yamekaguliwa Dar es Salaam kwenda mikoani au mikoani kwenda Dar es Salaam yaandikiwe hati ili kuondoa usumbufu njiani maana utakuta kwa Dar es Salaam pale Ubungo umefanyika ukaguzi, lakini likifika Kibaha askari wanalikagua tena na kila likisimamishwa askari wa usalama barabarani hutaka kujiridhisha.

Tahariri ya Mwananchi,

Mwananchi Communications Limited (MCL)

S.L.P. 19754 Dar es Salaam-Tanzania

SIMU +255222450875 au +255754780647