http://www.swahilihub.com/image/view/-/4843828/medRes/2165060/-/xcxxhtz/-/ikoa.jpg

 

Unyunyuziaji maji mashamba kwa mifereji unavyoleta tija

Bi Judith Nduva

Bi Judith Nduva (kushoto), mkulima katika kaunti ya Kajiado anayetumia mfumo wa Drip Iirrigation kunyunyizia mimea maji, akiwa na mfanyakazi wake wakiangalia hali ya mifereji. Picha/SAMMY WAWERU 

Na SAMMY WAWERU

Imepakiwa - Friday, November 9  2018 at  11:23

Kwa Muhtasari

Unyunyuziaji maji mashamba umesaidia pakubwa kugeuza hata maeneo kame kuwa ngome za uzalishaji wa vyakula.

 

WAKULIMA wengi, hasa wa matunda, mboga, nyanya na vitunguu Nyeri, Kirinyaga, Uasin Gishu na Nyandarua wamekumbatia mfumo wa kunyunyizia maji mashamba kwa mifereji.

Aidha, mfumo huu umerahisisha shughuli za kilimo ikizingatiwa kuwa si lazima mkulima ategemee mvua. Itakumbukwa kwamba kilimo ni uti wa mgongo wa taifa hili, ambacho licha ya kulilisha kimekuwa kitega uchumi na kubuni ajira.

Ni kupitia mfumo huu ambapo baadhi ya maeneo yasiyopokea mvua ya kutosha yameweza kutambulika kwa kufanya zaraa. Kajiado ni mojawapo ya kaunti zinazoorodheshwa miongoni mwa zile kame nchini, huku wengi wa wakazi wakifanya ufugaji.

Jamii ya Maasai ndiyo inaishi Kajiado, na hufanya ufugaji wa kuhamahama. Hata hivyo, dhana ya ufugaji inaonekana kutupiliwa mbali wakazi wakipevuka na kuzamia kilimo. Mbali na kutegemea msimu wa mvua, wanaoendesha kilimo wamekumbatia mfumo wa kunyunyizia maji mashamba kwa mifereji ili kuafikia ari yao.

Bw Joseph Naipande, ni mkulima wa vitunguu ‘vyekundu’ vya mviringo eneo hilo, na anasema mfumo huu umefanikisha juhudi zake kwa kiasi kikubwa. Mkulima huyu anasema anatumia mfumo wa kisasa maarufu kwa Kiingereza kama ‘Drip Irrigation’.

Drip Irrigation ni mfumo ambapo mifereji yenye mashimo huwekwa kwenye mashina ya mimea na maji yanapopampiwa hupenyeza moja kwa moja ardhini.

“Kazi huwa kudhibiti kiasi cha maji na kufungua mashimo yaliyoziba,” anaeleza mkulima Bw Naipande, ambaye pia ni afisa wa polisi.

Anaongeza: “La busara kwa mfumo huu ni kwamba hauna machovu. Kazi huwa kupalilia mimea na kuipulizia dawa za magonjwa na wadudu.”

Kulingana na Naipande ni kuwa wakulima wengi Kajiado wametambua madhumuni ya Drip Irrigation na ndio maana inageuka kuwa kapu la kilimo nchini.

Maji

Bi Judith Nduva, ni mkulima mwingine anayetumia mfumo huu kufanya kilimo katika mtaa wa Korrompoi, Kajiado.

Aidha, Bi Nduva ana shimo la urefu wa futi 150 na amesindika matangi ya maji juu yake, ambapo huyapampu kwa stima.

“Anayekumbatia mfumo huu anafaa kununua hifadhi nyingi za maji (matenki) ili maji yanapopungua atakuwa na ya kutosha kuendeleza kilimo,” anashauri mkulima Nduva.

Nduva hukuza mboga za kienyeji, nyanya na vitunguu.

Mkulima huyu anasema endapo maeneo kame nchini yatatumia mfumo huu, yatageuka kuwa bustani ya kilimo sawa na Kajiado.

“Kaunti ya Kajiado maeneo mengi ni kame, lakini maeneo hayohayo ndiyo tunafanya kilimo kupitia Drip Irrigation,” anasema.

Kuwekeza katika mfumo huu pamoja na kuchimba shimo, Nduva aligharamika karibu Sh100,000.

Samuel Mwaniki ambaye ni mkulima wa nyanya, vitunguu na Maharagwe ya Kifaransa (French Beans) Joska kaunti ya Machakos, hutumia mfumo huu, japo hunyunyizia maji kwa mifereji mwenyewe (kwa mujibu wa picha inayoandamana na makala hii akinyunyia French Beans maji).

Hata hivyo, kwa kuwa ni ya plastiki mifereji hii huharibika kwa kupasuka inapoachiliwa kucharazwa na miale ya jua.

Vilevile, inapokanyagwa huwa katika hatari ya kuvunjika. Wakulima hawa wanashauriwa haja ya kuipa matunzo ya hali ya juu.