http://www.swahilihub.com/image/view/-/2850168/medRes/1104816/-/ng3oxcz/-/DNCOASTDP2508J.jpg

 

Kiwango cha ushawishi wa Ruto nje ya mipaka ya Kenya kikoje?

William Ruto

Naibu Rais William Ruto akihutubu awali. Picha/WACHIRA MWANGI  

Na MWANGI MUIRURI

Imepakiwa - Friday, November 9  2018 at  12:41

Kwa Muhtasari

Siasa hasa kwa mgombea wa urais, huhitaji mtandao wa kidiplomasia ndani na nje ya mipaka ya nchi ili kuleta ushawishi mkubwa.

 

NAIBU Rais William Ruto sasa anakabiliwa na hatari ya kipekee ya kuonekana mdhaifu katika ushawishi kwa washirika wa mataifa ya kigeni na ambapo anaonekana kulemewa bila shaka na mpinzani wake mkuu, Raila Odinga ambaye ameteuliwa kuwa balozi wa kitengo cha miundombinu katika umoja wa mataifa ya Afrika (AU).

Hatari ni kuwa, DP Ruto ameonekana kama mwanasiasa wa hadhi nchini Kenya ambaye hachukuliwi kwa umuhimu nje ya nchi hasa katika mirengo ya kidiplomasia ya mataifa yaliyostawi.

Wakati Raila huonekana katika viwanja vya ndege kama jambo la kawaida akielekea katika mataifa ya kigeni na ambapo hupokelewa vyema na hata kupewa mialiko ya kutoa hotuba katika taasisi muhimu huko ng’ambo, Ruto hajaonekana katika ushirika wa kukumbatiwa kwa dhati nje ya nchi.

Wachanganuzi wanamuonya Ruto kuwa ni lazima atilie maanani uhusiano wake na mataifa hayo ikiwa ako na matumaini ya kumenyana na kinara huyo wa ODM, ambaye bila shaka ni maarufu katika mataifa mengi ya Ulimwengu.

Mjadala huu umezuka baada ya mbunge wa Homabay Mjini, Peter Opondo Kaluma kukejeli Ruto kwa msingi kuwa “ambia huyu Ruto kuwa yeye hachezi katika ligi moja na Raila.”

Opondo anasema ni kawaida sana Raila kuzuru mataifa ya kigeni; hali tofauti kabisa na Ruto.

Hali hii imesemwa kuwa kwa muda imekuwa ikimtatiza Ruto kwa kiwango kikuu katika siasa zake na ambapo amekuwa akifadhili kichinichini uteuzi wa mabalozi ambao ni wandani wake wa karibu ili wakazindue “mradi wa mauzo” wa kumpa ushawishi Ulaya.

Hatari nyingine katika njama hii ya Ruto ya kutuma wandani wake wakamtafutie ushawishi katika safu ya KIdipolomasia imeonekana kuhujumiwa na mkubwa wake ambaye ni Uhuru Kenyatta.

Kwa mujibu wa mchanganuzi wa masuala ya kidiplomasia, Prof Macharia Munene wa chuo kikuu cha USIU, mbinu hii ya Ruto ya kusukuma wandani wake wa karibu waingie katika siasa za kidipolomasia kwa manufaa yake zinaonekana kutoungwa mkono na Rais.
 “Haya ndiyo mambo madogomadogo ambayo yanatoa taswira kuwa ni kama rais anamtenga Ruto polepole. Wakati wa kuteua mabalozi wapya, rais alichukua wandani wa Ruto lakini pia akawateua wandani wa Raila. Ni kama rais Uhuru anawagonganisha Ruto na Raila kimakusudi akijua vizuri mdogo wake atalemewa kisiasa,” asema Prof Munene.

Katika orodha ya hivi majuzi ya teuzi hizo za ubalozi, Ruto anasemwa kuwa alisukuma kukubalika kwa aliyekuwa mwenyekiti wa tume ya kutathmini mishahara na marupurupu ya utumizhi kwa umma (SRC), Bi Sarah Serem na aliyekuwa mbunge wa Ainamoi, Benjamin Langat.

Washirika wengine wa Ruto katika orodha hiyo wanasemwa kuwa aliyekuwa mkurugenzi wa upelelezi wa Jinai (DCI), Ndegwa Muhoro na msemaji wa Ikulu, Manoah Esipisu ambaye Rais Uhuru alimtema na kujaza nafasi yake na mtangazaji, Kanze Dena.

Pia, kuna Luteni Jenerali mstaafu Samuel Thuita ambaye anaripotiwa alipigiwa debe na Ruto aorodheshwe kama balozi nje ya nchi ili akafae mrengo wake katika siasa za kidiplomasia.

Shida na kero kwa Ruto ni kuwa, orodha yake ilikubaliwa, lakini naye Raila akatwaa kuteuliwa kwa aliyekuwa waziri wa Kawi, Ochilo Ayacko (lakini ambaye sasa atatolewa kwa kuwa ametwaa Useneta wa Migori katika uchaguzi mdogo wa hivi majuzi, na aliyekuwa mbunge wa Kasipul Kabondo, Paddy Ahenda na Peter Nicholas Ogego.

Prof Munene anasema kuwa timu ya Ruto inaonekana wazi kuwa inapigwa vita katika pande zote “sio tu hapa nchini, bali hata mataifa ya ng’ambo.”

Aliyekuwa mbunge wa Maragua, Elias Mbau anasisitiza kuwa tangu Ruto aandaliwe kesi ya uhalifu wa kibinadamu katika mahaka 2007, lakini ikasambaratika, hata wakati aliishia kuchaguliwa kama Naibu Rais, aliendeleza 'uongozi wa shaka' ambapo amehusishwa na madai kadha ya ufisadi.

Bw Mbau anasema kuwa mataifa yaliyostawi “huonekana yakimchukulia Ruto kama kiongozi ambaye hana ule uvutio wa kimataifa, bali huonekana kama aliyebahatika tu kuvutia jamii yake mashinani na akazidisha manufaa hayo kwa kujiunga na jamii nyingine kubwa na akaibuka kuwa kiongozi wa kitaifa bila kuwekeza katika muundo mbinu wa kimataifa.”

Mbau anasema kuwa kinyume na Raila, Naibu Rais ameonekana akiwa na tope la kudhaniwa ndiye shida kuu ya uwiano kati ya utawala  wa Jubilee na upinzani na huwa hana ule uwezo wa kudhibiti hisia ili kuwekeza katika siasa za kuunganisha taifa.

Anasema kuwa hatua ya Raila ya kukubali kusahau alikuwa na kesi halali ya kudai ushindi katika uchaguzi wa 2017 na ambapo ametoboa kujiangazia kama aliyeibiwa ushindi, akaamua kuridhiana na kushirikiana na utawala wa Uhuru Kenyatta, ‘uzalendo’ huo umempa ufuasi mkuu katika safu ya kidiplomasia ulimwenguni.

“Kinyume na Ruto ambaye hakuonekana kuwa tayari kukumbatia maridhiano ya kisiasa, Raila alijitokeza kama sura ya mapenzi kwa usalama na uthabiti wa taifa, suala ambalo hata limefungua milango ya mataifa muhimu ulimwenguni kutuma ujumbe wa kusaka ushirika wa kimaendeleo na Kenya,” anasema.

Anasema kuwa Raila alijipa ‘bonga pointi’ muhimu za kisiasa ulimwenguni kwa kukumbatia uwiano, huku Ruto wakati mmoja akilalamika kwamba yumkini nia ya 'maridhiano' ni kuyumbisha Jubilee.

“Uliza Ruto ni kwa nini haonekani akialikwa katika makongamano ya kimataifa na ni mara yake ya mwisho lini alihudhuria hafla ya hadhi na ya kikazi katika taifa la Ulaya au Asia. Hii ni hatari kubwa sana kwake ikizingatiwa kuwa anayemenyana naye kufa kupona kwa sasa ni Raila Odinga ambaye huonekana akiwa na ushawishi mkuu na ushirika wa dhati na mataifa mengi ya ng’ambo,” anasema mchanganuzi 'mbishi', Mutahi Ngunyi.

Anasema kuwa ikiwa uchaguzi utaandaliwa leo na wa kupiga kura ya urais wawe ni washirika muhimu wa kimaendeleo kutoka mataifa ya Ulaya, basi Ruto atashindwa vibaya na Odinga.

Ushirikiano

Bw Ngunyi anasema kuwa siasa hutegemea sana jinsi mgombea wa urais atapokelewa na mataifa mengine kwa kuwa utawala huhitaji ushirika wa mirengo ulimwenguni ili usionekane kuwa kama kisiwa kilichojitenga.

Aliyekuwa mbunge mwakilishi wanawake wa Nyeri, Bi Priscilla Nyokabi na ambaye huonekana akiegemea mrego wa Naibu Rais anasema kuwa “mkono wa Rais Uhuru Kenyatta katika changamoto hii ya Ruto ya kidiplomasia unaonekana kwa uwazi.”

Anasema kuwa rais Uhuru ndiye hutoa majukumu ya kutekelezwa na Naibu Rais “na ikiwa hamjengi Ruto kwa kumpa majukumu ya kuhudhuria makongamano ya kimataifa au kushiriki mazungumzo ya kimataifa kuhusu masuala muhimu na wadau muhimu katika jukwaa la kimataifa, basi anamumaliza.”

Bi Nyokabi anasema kuwa shida kubwa kuhusu ushindani na Raila ni kuwa, “amejijenga (Raila) kwa muda, familia yake imekuwa na mizizi ya kihistoria nje ya nchi na washirika wa mashujaa kama marehemu Jaramogi Oginga Odinga (babake Raila) wametapakaa kote ulimwenguni.”

Anasema kuwa Ruto asiposaidiwa kujijenga katika safu hiyo ya Kidiplomasia, atakuwa na shida kubwa sana ikizingatiwa kuwa ako na mpinzani mwingine katika ngome ya Bonde la Ufa ambaye ni Seneta wa Baringo, Gideon Moi.

Bi Nyokabi anasema kuwa Moi akiwa ni mtoto wa Rais Mstaafu Daniel Moi aliyeongoza taifa hili kwa miaka 24 (1978-2002) na ambapo mizizi yake ya kidiplomasia iko sambamba na ya Raila.

“Gideon Moi na Raila wameonekana kuwa na ushirika wa kisiasa wakimpinga Ruto. Katika safu ya kidiplomasia, mrengo huo wa Raila na Moi uko na ubabe kuliko wa Ruto na hapo ndipo hatari kuu iko kwa siasa za Naibui Rais katika azma yake ya kuingia Ikulu,” anasema.