http://www.swahilihub.com/image/view/-/4054894/medRes/1727389/-/yca6q9/-/ushindi.jpg

 

Wengi wafika Ichaweri kusherehekea ushindi wa Uhuru Kenyatta

Jubilee

Rais Uhuru Kenyatta na Naibu wake William Ruto waonesha vyeti vyao baada ya matokeo rasmi ya kura za urais kutangazwa na Mwenyekiti wa IEBC, Wafula Chebukati Agosti 11, 2017 katika ukumbi wa Bomas, Nairobi. Picha/JEFF ANGOTE 

Na MWANGI MUIRURI na SAMMY WAWERU

Imepakiwa - Saturday, August 12  2017 at  15:05

Kwa Mukhtasari

Kwa sasa watu wanaokisiwa kuwa zaidi ya 5,000 wamekongamana kwa sherehe ya ushindi wa Rais Uhuru Kenyatta katika uchaguzi wa Agosti 8, 2017, nyumbani kwao katika Kaunti ya Kiambu.

 

KWA sasa watu wanaokisiwa kuwa zaidi ya 5,000 wamekongamana kwa sherehe ya ushindi wa Rais Uhuru Kenyatta katika uchaguzi wa Agosti 8, 2017, nyumbani kwao katika Kaunti ya Kiambu.

Mtandao wa Swahilihub umetembelea eneo hilo katika kijiji cha Ichaweri ambapo ni boma la wazazi wa Rais Kenyatta na kushuhudia uchinjaji wa fahali saba, upishi wa mapochopocho ukiendelea chini ya ujima wa baadhi ya wanakijiji.

Kwa mujibu wa mjombake Rais Kenyatta, kwa jina George Muhoho, Wakenya walifika bila mwaliko na wakatueleza kuwa wapo hapa kusherehekea ushindi wa rais Kenyatta kwa siku tatu zijazo. Tukawakumbatia kama wageni wetu na kwa sasa ni jukumu letu la kuwafaa.”

“Tumeguzwa nyoyo zetu na upendo wa watu hawa ambao wamejumuika kutoka maeneo jirani, wengine wakiwa wametoka Kaunti ya Kirinyaga, Kaunti ya Machakos, Nairobi na Murang’a na kujumuika na wengine wa hapa kwetu katika Kaunti ya Kiambu,” amesema Muhoho.

Amesema kuwa haijalishi kuwa aidha walikuwa wamejipanga mapema au wameingia hapo bila kushirikishwa wajitokeze.

Akasema: “Kile tunachojua ni kuwa wako hapa, ni wageni wetu na tumewakumbatia jinsi mgeni anafaa kupokelewa. Wamekuja hapa kwa nia
njema, wanasherehekea jinsi hata sisi familia ya Rais Uhuru Kenyatta tunasherehekea ushindi wake, na kwa pamoja tukimshukuru Mwenyezi Mungu
kwa neema hiyo yake ya baraka kwetu, tujumuimuike pamoja kwa sherehe hizi.”

Wenyeji wa maeneo mengi ya Mlima Kenya tayari wanaendelea kusherehekea Ijumaa kuanzia saa nne na dakika 18 ambapo tume huru
ya uchaguzi na mipaka (IEBC) ilitangaza Rais Kenyatta kama mshindi wa kura ya urais akizoa asilimia 54.27 ya kura zilizopigwa Agosti 8, 2017.

Katika barabara nyingi za eneo hilo, makundi ya watu wakiabiri magari, pikipiki na hata baiskeli yalijumuika hadharani ndani ya giza kusherehekea kupitia nduru za ushindi, kelele za shangwe na kupuliza honi wakiwa barabarani.

Waliamshana, wakitoa matamshi ya kejeli kwa wenzao kuwa watokee hadharani ili wasihesabiwe kama waliokuwa wakipinga ushindi wa Rais Kenyatta.

Picha halisi mambo yalivyokuwa Kiambu

Ijumaa Agosti 11, 2017 saa nne na nusu za usiku kumbu kumbu zilinakiliwa katika historia ya Kenya Rais Uhuru Kenyatta wa mrengo wa Jubilee alipotangazwa kuwa mshindi wa uchaguzi mkuu uliofanyika mnamo Agosti 8, 2017 kote nchini, hivyo basi kuhifadhi kiti chake kwa awamu ya pili na ya mwisho na kuwa rais wa tano wa Jamhuri ya taifa hili.

Katika ukumbi wa Bomas of Kenya, mwenyekiti wa tume huru ya uchaguzi na mipaka IEBC Bw Wafula Chebukati, alitoa rasmi tangazo hilo baada ya shughuli za uchaguzi kutia nanga.

Aidha Rais Kenyatta na Naibu wake William Ruto ndio wataongoza taifa hili kwa kipindi cha miaka mingine mitano ijayo baada ya kuzoa kura 8,203,290 ikiwakilisha asilimia 54.24 na kinara wa muungano wa National Super Alliance (Nasa) Raila Odinga akipata kura 6,762,224 ikiwa ni asilimia 44.92 kwa jumla ya kura 15,073,662 zilizopigwa na kuwakilisha asilimia 78.91 ya wapiga kura 19,687,563 waliosajiliwa na tume ya IEBC.

Bw Raila (Odinga) aliwania kiti hicho akisaidiwa na mgombea mwenza Kalonzo Musyoka (Wiper Party).

"Ninachukua fursa hii kumtangaza mheshimiwa Uhuru Kenyatta kuwa Rais wa tano wa Jamhuri ya Kenya akisaidiwa na mgombea mwenza William Ruto kama Naibu Rais," akasema Chebukati baada ya kutangaza alama ambazo kila kinara alizoa katika kila kaunti.

Ni kufuatia tangazo hilo wananchi kutoka ngome za Jubilee kote nchini walielekeza furaha zao barabarani na kushagilia kwa shangwe, vifijo na nderemo kwa ushindi wa Rais Kenyatta na Naibu wake Ruto.

Kaunti ya Kiambu alikozaliwa Rais Kenyatta, wananchi hawakujali iwapo giza lilitanda  au la, ila sharti wangeonyesha hisia zao kwa kushabikia ushindi huo waliohoji ni wa 'nchi nzima'.

Sawia na Kiambu, jimbo la Kati mlima Kenya kwa jumla, Bonde la Ufa ikiwemo Kaunti ya Nakuru na Uasin-Gishu Wakenya, na maeneo mengine nchini waliungana kwa pamoja kushangilia.

"Huu si ushindi wa Rais Kenyatta na Naibu wake Ruto, ila ni ushindi wa Kenya nzima," mwananchi mmoja akaeleza Swahilihub mtaani Githurai 45 Kiambu Ijumaa usiku ilipokita kambi kushuhudia hali halisi ilivyokuwa.

"Tunaomba wenzetu katika upinzani waungane nasi tukuze taifa hili, Kenya ni moja tudumishe amani," akaongeza Mkenya mwingine.

Kauli ya wananchi waliojitokeza kuhubiri kudumisha amani wakisherehekea ufanisi wa Jubilee, aidha ilitiliwa mkazo na Rais Kenyatta dakika chache baada ya kutangazwa mshindi.

"Serikali yetu itahudumia watu wote milioni 45 kwa usawa bila ubaguzi. Ni haki ya kila mwananchi kuhudumiwa na serikali," akasema Rais akihutubia taifa katika ukumbi wa Bomas of Kenya na kuradidi ujumbe huo baadaye katika ukumbi wa KICC.

"Kenya itasalia kuwa moja. Tukashifu ghasia na ukabila. Tudumishe amani na tuishi kama jirani wema, ndugu na dada," akaongeza.

Rais Kenyatta ana siku 14 kutoka siku aliyotangazwa mshindi ili aapishwe. Tangazo hilo aidha litachapishwa kwenye gazeti la serikali, kwa mujibu wa katiba.

Hata hivyo kitendawili ambacho kinasalia pasi kuteguliwa ni; Iwapo muungano wa Nasa utakubali ushindi wa Jubilee, baada ya kushikilia kuwa matokeo hayo si halali.

Vinara wa Nasa akiwemo Raila anasema kuwa mitambo ya IEBC ilidukuliwa ili kumsaidia Kenyatta kuibuka mshindi, jambo ambalo tume hiyo imekanusha na kupinga vikali.

Ijumaa jioni Seneta wa Siaya James Orengo na kinara mwenza katika Nasa, wote ambao ni maajenti wakuu wa muungano huo walisema kwamba hawaafikiani na matokeo hayo, huku wakiitaka tume ya IEBC kutangaza Raila ndiye mshindi.

Aidha Nasa ilisema haitakata rufaa mahakamani, ikihoji kuwa wananchi ndio watakuwa korti ya maamuzi.

Wachunguzi wa kimataifa kutoka miungano/mashirika ya: AU, EAC, Jumuiya ya Madola ya Common Wealth, IGAD na wengineo, walidokeza kuwa shughuli hiyo ya uchaguzi ilikuwa ya huru, haki na wazi.